Arsenal Vs Everton-Mambo matano niliyoyaona

Juzi jumapili Arsenal ilipata ushindi wake wa tano chini ya kocha Unai Emery baada ya kuifunga timu ya Everton kwa magoli 2-0.

Katika mchezo huo kuna mambo mengi sana yaliyotokea ila haya mabo matano ndiyo yaliyovuta fikra zangu zaidi.

Petr Cech bado kipa bora

Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakipinga uamuzi wa kocha Unai Emery wa kumuanzisha Petr Cech.

Lakini baada ya kumuangalia Bernd Leno kwenye Europa League na kumuangalia Petr Cech kwenye mechi za msimu huu , naamini kwa sasa Cech ndiye anayeshahili kuwa kipa namba moja.

Leno ni mzuri kwa kucheza mpira kwa miguu lakini Cech ni bora kuliko Leno linapokuja kwenye suala la kuzuia michomo na hicho ndicho mashabiki tunachokitaka.

Na kama kuna siku ambayo angeweza kuwafunga midomo mashabiki wote wanaombeza ni juzi ambapo alicheza kwa kiwango cha hali ya juu.

Aliweza kuokoa magoli ya wazi kutoka kwa washambuliaji wa Everton na pia alikuwa akifanya maamuzi sahihi linapokuja suala la kucheza krosi. Kwangu mimi juzi Petr Cech ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa mchezo.

Lucas Toreira anamfanya Granit Xhaka kuonesha ubora wake

Kwa mara ya kwanza Lucas Torreira alianza katika ligi kuu ya Uingeleza baada ya Matteo Guendouzi kupumzishwa.

Kama alivyofanya katika michezo ya nyuma ambayo alianza kama mchezaji wa akiba, mchezaji huyo alikichangamsha kiungo cha Arsenal na kuifanya timu icheze vizuri.

Cha msingi nilichokiona ni kwamba uwepo wa Torreira ulimpunguzia majukumu Xhaka na kumfanya acheze mpira kwa utulivu mkubwa huku majukumu ya kukaba akiachiwa Torreira na majukumu ya kuanzisha mashambulizi akiachiwa Xhaka.

Pamoja na kupata kadi ya njano mapema katika mchezo huo, Torreira alionesha ukomavu mkubwa na kuweza kuwapokonya mipira maadui bila kuwafanyia faulo.

Binafsi sina matatizo na Matteo Guendouzi ila naamini Torreira na Xhaka wanapaswa kuanza pamoja.

Uelewano kati ya Aaron Ramsey na Mesut Özil

Wakati mchezo ukianza Mesut Özil alianza kama winga wa kulia na Aaron Ramsey alianza kama kiungo mshambuliaji namba 10.

Lakini ukiangalia mchezo huo kwa makini walikuwa wakibadilishana kucheza winga wa kushoto ili kumsaidia Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye alianza mchezo huo kama winga wa kushoto.

Ukiangalia goli la kwanza la Arsenal Aubamayang anacheza kama mshambuliaji wa kati, Lacazette kama namba 10, na Ramsey kama winga wa kushoto.

Kubadilishana namba huko kuliisaidia Arsenal kutawala kipindi cha pili na huku Ramsey akipata asisti mbili katika mchezo huo. Hali hii pia niliiona katika kipindi cha pili dhidi ya Newcastle.

Kwa mtazamo wangu mimi uelewano bado haujawa mkubwa ila kuna kitu Unai Emery anakifanya na muda si mrefu tutaona matunda yake.

Rob Holding alicheza vizuri

Baada ya kuumia kwa Sokratis mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa na wasiwasi kama Arsenal ingeweza kuhimili vishindo vya washambuliaji wa Everton waliokuwa wanalisakama lango la Arsenal mara kwa mara.

Lakini Rob Holding aliweza kuwatuliza mashabiki hao baada ya kucheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu.

Bado Unai Emery anaendelea kuijenga timu

Arsenal Vs Everton-Mambo matano niliyoyaona

Cha msingi ni kukumbuka ya kwamba kila kocha ana falsafa zake na itachukua muda kwa wachezaji hawa kuelewa ni nini hasa mwalimu anataka, kwa sisi tunaoifuatilia Arsenal kwa karibu tumeanza kuona mabadiliko chanya katika uchezaji wa timu, ufanyaji wa mabadiliko na upangaji wa timu, cha msingi tumpe muda kocha Emery.

Hayo ni mambo niliyoyaona katika mchezo kati ya Arsenal na Everton, je wewe uliona nini ? tupia maoni yako hapa chini.

 

Speak Your Mind

*