Arsenal yaishushia kipigo Totenham Hotspurs

Timu ya Arsenal jana ilifanikiwa kuwashinda wapinzani wao wa jadi, Totenham Hotspurs kwa jumla ya magoli 4-2 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika katika uwanja wa Emirates.

Arsenal yaishushia kipigo Totenham Hotspurs

Arsenal iliuanza mchezo wa jana kwa kasi kubwa na kama usingekuwa uwezo wa kipa wa Spurs, Arsenal ingeweza kupata magoli matatu ndani ya dakika 20 za mwanzo.

Arsenal ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli baada ya mshambuliaji Pierre Emerick Aubamayang kufunga goli la kuongoza kupitia mkwaju wa penati baada ya beki wa Totenham kujaribu kuokoa mpira kwa mkono.

Arsenal ikiwa inacheza vizuri, Mike Dean aliwapa Totenham faulo ya utata nje kidogo ya eneo la hatari na Totenham waliitumia kupata goli la kusawazisha baada mpira wa kichwa uliopigwa na Erick Dier kumshinda golikipa wa Arsenal Bernd Leno.

Baada ya goli hilo Totenham Hotspurs walionekana kuamka na walifanikiwa kupata goli la pili dakika moja baadaye baada ya Son kujiangusha ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Mike Dean kuamua kutoa penati ambayo ilifungea kistadi na Harry Kane.

Baada ya Totenham kuwa mbele wachezaji wa Arsenal walionekana kupoteana kwa dakika kama tano hivi ambapo Totenham walionekana kana kwamba wangeweza kuongeza goli la tatu.

Baadaye Arsenal walitulia na kuendelea kucheza vizuri, hadi mapumziko Arsenal 1-2 Totenham Hotspurs.

Kipindi cha pili kilianza kwa mwalimu Emery Unai kufanya mabadiliko matatu,mawili ya wachezaji ambapo Alex Iwobi na Henrikh Mkhitaryan walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Aaron Ramsey na Alexandre Lacazette, badiliko la tatu lilikuwa la kimfumo ambapo Arsenal ilicheza na washambuliaji wawili huku Ramsey akicheza nyuma yao.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Arsenal kwani dakika 10 baadaye ilipata goli la kusawazisha baada ya Pierre Emerick Aubamayang kufunga kwa shuti kali na ka kiufundi kufuatia pasi ya Aaron Ramsey.

Alikuwa ni mshambuliaji wa kifaransa Alexandre Lacazette aliyeipatia Arsenal goli la tatu baada ya kupiga shuti lililombabatiza Eric Dier na kumuacha Hugo Lloris alichupa bila mafanikio, Goli hilo liliibua shangwe na nderemo kubwa kwa mashabiki wa Arsenal duniani kote.

Arsenal v Tottenham Hotspur

Kiungo kutoka Uruguay, fundi wa mpira Lucas Torreira alifanikiwa kufunga goli la nne na kuihakikishia Arsenal pointi tatu muhimu, Torreira alifunga goli hilo kufuatia pasi iliyopigwa na Aubamayang.

Hilo lilikuwa ni goli la kwanza la Torreira katika jezi za Arsenal na kufunga katika mchezo wa wapinzani wa jadi kunafanya liwe ni goli ambalo litadumu katika kumbukumbu zake na za mashabiki wa muda mrefu.

Baada ya ushindi huo Arsenal imefikisha michezo 19 bila ya kufungwa na kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 30 sawa na Totenham lakini Arsenal wapo mbele kwa kuwa na wastani bora wa magoli ya kufunga na kufungwa.

Baada ya mchezo huo leo Arsenal itaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Manchester United utakaofanyika katika uwanja wa Old Trafford jumatano ijayo.

#COYG

Kama unataka kuangalia vipande muhimi vya mchezo huo nimekuwekea video hapo chini

Speak Your Mind

*