Arsenal yapata ushindi wa tano chini ya Unai Emery

Baada ya kuanza ligi kwa kusua sua na kupoteza michezo yake miwili ya mwanzo, Arsenal chini ya kocha Unai Emery inaonekana ya kwamba imeanza kubadika na imefanikiwa kushinda michezo yake mitano, minne ikiwa ni ya ligi kuu ya Uingeleza na mmoja ni kwenye kombe la Europa League.

Arsenal yapata ushindi wa tano chini ya Unai Emery

Katika mchezo wa jana Arsenal iliishinda timu ya Everton kwa jumla ya magoli 2-0, magoli yaliyofungwa na washambuliaji wake hatari , Pierre Emerick Aubamayang na Alexandre Lacazette.

Kama kawaida katika mechi za hivi karibuni Arsenal walianza mchezo huo taratibu sana kiasi cha kwamba kama washambuliaji wa Everton wangekuwa makini wangeweza kupata magoli si chini ya mawili katika kipindi cha kwanza.

Habari mbaya zaidi ilikuwa ni kuumia kwa beki wa kati wa Arsenal, Sokratis na nafasi yake kuchukuliwa na Rob Holding ambaye alicheza vizuri.

Mpaka kipindi cha kwanza kinaisha mchezo huo ulikuwa 0-0.

Kipindi cha pili Arsenal ilianza bila kufanya mabadiliko na wakati Emery akijiandaa kufanya mabadiliko Lacazette alifunga bonge la goli baada ya kupiga mpira kiufundi na kumfanya mlinda mlando wa Everton, Jordan Pickford ausindikize mpira kwa macho wakati ukiingia wavuni.

Wahenga walisema magoli hubadili taswira ya mchezo na hicho ndicho kilichotokea kwani baada ya kuingia kwa goli hilo Arsenal walibadilika na kuanza kucheza soka la uhakika.

Dakika chache baadaye Arsenal ilipata goli la pili kupitia kwa Aubamayang baada ya kupokea pasi kutoka kwa Aaron Ramsey.

Goli hilo limeleta mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya marudio kuonesha ya kwamba mchezaji huyo alikuwa amaotea.

Badda ya magoli hayo timu zote zilifanya mabadiliko lakini mabadiliko hayo hayakuweza kubadili matokeo kwani hadi mwisho wa mchezo Arsenal 2-0 Everton.

Jumatano usiku Arsenal itacheza na Brentford katika mchezo wa kugombea kombe la Carabao.

 

Speak Your Mind

*