Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Arsenal ilicheza soka la kiwango kikubwa katika mchezo ambao uliishia kwa sare ya goli 1-1 dhidi ya Liverpool.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Goli la kusawazisha kutoka kwa mshambuliaji wa Arsenal, Alexandre Lacazette lilimaanisha ya kwamba Arsenal wangeondoka na pointi moja katika mchezo huo uliokuwa mkali na na kusisimua.

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kucheza vizuri lakini Liverpool ndio waliopata nafasi nzuri zaidi za kufunga, kwani walicheza kwa kujihami na kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Kama nilivyosema asubuhi, sehemu ya kiungo ndiyo sehemu ambayo ingeamua matokeo na Lucas Torreira alimpoteza kabisa Fabinho na kutawala eneo la katikati ya uwanja.

Kipindi cha kwanza Liverpool waligongesha miamba mara mbili kupitia kwa wachezaji  Roberto Firmino na Virgil van Dijk.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Arsenal walikianza kipindi cha pili kwa nguvu lakini walikuwa ni Liverpool waliopata goli la kuongoza baada ya golikipa wa arsenal Bernd Leno kufanya makosa ambapo aliutema vibaya mpira na kumkuta James Milner ambaye aliipatia Liverpool goli la kuongoza.

Mabadiliko yaliyofanya na kocha wa Arsenal Unai Emery, ya kumtoka Henrik Mkhitryan na kumuingiza Alex Iwobi yaliisaidia sana Arsenal kwani ilianza kufanya mashambulizi ya hatari zaidi kiasi cha Liverpool kupaki basi.

Alikuwa ni mshambuliaji wa Arsenal,Alexandre Lacazette aliyeipatia Arsenal goli la kusawazisha katika dakika ya 82 baada ya kuwazunguka mabeki wa Liverpool na kupiga shuti kifundi ambalo kipa wa Liverpool,Allison hakuweza kuliona.

Hadi mwisho wa mchezo Arsenal 1-1 Liverpool.

Baada ya kuisha kwa mchezo huo nilifanikiwa kuongea na baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambapo wengi wao walionekana kuridhika na hali ya kujituma kulikooneshwa na timu yao na pia wengi wanaamini ya kwamba Arsenal ilishahili kushinda mchezo huo.

Kwangu mimi Granit Xhaka ndiye aliyekuwa mchezaji nyota katika mchezo wa leo kwani yeye na Lucas Torreira walidhibiti sehemu ya kiungo, Xhaka alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote, aliondoa mipira mingi ya hatari na pia alimsaidia sana Sead Kolasinac upande wa kushoto.

Baada ya mchezo wa leo, Arsenal itaingia dimbani tena Alhamisi ijayo kupambana na timu ya Sporting Lisbon katika michuano ya kugombea kombe la Europa League.

Pia sare ya leo inamaanisha Arsenal imecheza michezo 14 bila ya kufungwa, ikishinda 12 na kutoka sare katika michezo miwili.

Kwa wale ambao hawakuona mchezo huo hapo chini kuna video inayoonesha vipande muhimu vya mchezo huo na magoli yote mawili.

Speak Your Mind

*