BATE vs Arsenal-Kazi inaanza sasa

BATE vs Arsenal-Kazi inaanza sasa

Arsenal inaanza hatua ya mtoano ya kombe la Europa League kwa kusafiri kwenda Belarus kucheza na Bate borisov ya nchini humo.

Unai Emery ana kazi moja tu, anatakiwa kwenda hatua moja zaidi ya hatua aliyofikia Arsene Wenger msimu uliopita, Wenger aliishia nusu fainali baada ya kufungwa na timu iliyoenda kuchukua taji hilo, Atletico Madrid.

Lakini uzoefu wa Unai Emery unaweza ukawa chachu kwa Arsenal kupiga hatua moja zaidi na kuingia fainali na hatimaye kubeba ndoo hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya timu.

Arsenal haijawahi kushinda michuano ya kombe la Europa league na ukweli ni kwamba Arsenal haijabeba taji lolote la Ulaya kwa miaka 25 sasa.

Ukichukulia ya kwamba tayari kimahesabu Arsenal haiweza kuchukua kombe la EPL na imetoka katika michuano ya FA na Carabao, hii ni nafasi ya pekee ya Arsenal na Unai Emery kuchukua kombe mwaka huu.

Mimi binafsi ukiniambia nichague kati ya kombe la Europa league na kuingia nne bora nachagua kombe la Europa League.

Unai Emery anatakiwa apange kikosi cha kwanza

Baada ya kutolewa na Machester United katika kombe la FA, Arsenal haitakuwa na mechi yeyote mwisho wa wiki hii hivyo wachezaji watakuwa na muda wa kupumzika kabla ya kurudiana na Bate alhamisi ya wiki ijayo na siku tatu baadaye itacheza na Southampton.

Hivyo ni muhimu kwa kocha kupanga kikosi cha kwanza na kushinda kwa goli nyingi ili katika mechi ya marudio atumie kikosi cha pili huku kikosi cha kwanza kikipumzika kuwasubiri Southampton.

Utabiri wa matokeo

Bate Borisov walikuwa katika kundi moja na Chelsea na walimaliza katika nafasi ya pili pointi saba nyuma ya vijana hao wa darajani.

Kama nikiwa mkweli ni kwamba Bate Borisov sio timu ya kutisha ni timu ambayo ninategemea ya kwamba Arsenal wanaenda kushinda bila matatizo.

Kama Arsenal wakiacha dharau na kucheza na kikosi cha kwanza na kwa kujituma sioni kwa nini Arsenal isiibuke na ushindi mnono.

Naona mchezo huu ukiisha Arsenal 5-1 Bate Borisov

Kwa kifupi siiamini sana safu ya ulinzi ya Arsenal, kwa sasa naamini hawawezi kucheza mchezo bila ya kuruhusu goli ina nina imani kubwa sana na safu ya ushambuliaji na kuna uwezekano mkubwa wa kwamba Özil na Mkhi wakaanza na ikiwa hivyo mkono unawahusu.

Je wewe una mtazamo gani? tupia maoni yako hapa chini.

 

Zech Medley asaini mkataba mpya na Arsenal

Beki kinda wa Arsenal, Zech Medley amesaini mkataba mpya na wa muda mrefu wa kuendelea kuitumikia timu hiyo ya kaskazini mwa london.

Zech Medley asaini mkataba mpya na Arsenal

Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 18 ameishaichezea timu ya wakubwa katika mechi tatu msimu huu, mara mbili katika kombe la Europa league dhidi ya Vorskla na Qarabag, na aliingia kipindi cha pili katika mchezo wa raundi ya tatu ya kombe la FA dhidi ya Blackpool mwezi uliopita.

Akiongea mara baada ya kusaini mtakaba huo, mchezaji huyo ambaye pia ni shabiki wa Arsenal alisema ni furaha na heshima kubwa kusaini mkataba mpya na timu ambayo amekuwa akiishaikia tangu akiwa mtoto.

Arsenal ikiwa na matatizo ya majeruhi katika beki wa kati na pia wachezaji wake wa muhimi kama Nacho Monreal na Laurent Koscienly ambao wote wana miaka 33 na wanaelekea kustaafu, mchezaji huyo anaweza akapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza katika miaka michache ijayo.

Kila la heri Zech.

Rasmi-Aaron Ramsey kujiunga na Juventus

Kiungo wa Arsenal, Aaron Ramsey leo ametangaza rasmi kujiunga na timu ya Juventus ya Italia baada ya kufikia makubariano na kusaini mkataba wa wakali hao wa Turin.

Aaron Ramsey kujiunga na Juventus

Aaron Ramsey mchezaji aliyedumu Arsenal kwa miaka 11 ataondoka kama mchezaji huru baada ya Arsenal kuondoa mezani mkataba kati ya pande hizo mbili ambao kimsingi walishakubaliana, bado hakuna taarifa rasmi kwa nini Arsenal waliondoa mkataba.

Taarifa hizo zilivuja jioni baada ya BBC kuziweka mtandaoni na baadaye Aaron Ramsey alithibitisha kupitia mitandao yake ya kijamii na pia timu ya Juventus imedhibitisha kukamilika kwa usajili huo.

Kwa upande wa Arsenal wao walidhibitisha taarifa hizo kwa kuweka taarifa fupi katika ukurasa rasmi wa timu ambapo kwa kifupi walisema ya kwamba mchezaji huyo ataondoka Arsenal mwishoni mwa msimu huu na wanamtakia kila la heri katika maisha yake mapya ya soka.

Taarifa zaidi zinadai ya kwamba Ramsey atakuwa ndiye mchezaji wa pili kwa kulipwa mshahara mkubwa na timu hiyo ya Italia ambapo atakuwa akilipwa paundi laki 400 kwa wiki nyuma ya Cristiano Ronaldo, hali inayonfanya kuwa mchezaji mwenye asili ya Uingeleza anayelipwa mshahara mkubwa zaidi.

Mashabiki wengi wa Arsenal watamkumbuka Ramsey kwa goli lake dhidi ya Hull City katika fainali ya kombe la FA lililomaliza ukame wa makombe Arsenal.

Kila la heri Aaron Ramsey.

Tetesi-Unai Emery kupewa paundi millioni 45 za usajili Arsenal

Gazeti za daily mail limeandika ya kwamba kocha Unai Emery atapewa paundi milioni 45 tu kwa ajili ya usajili Arsenal.

 

Tetesi-Unai Emery kupewa paundi millioni 45 za usajili Arsenal

Taarifa hizo zinaendelea kuandika ya kwamba kutokana na timu kukosa pesa, kocha Unai Emery atalazimika kubana matumizi na kutumia pesa hizo kukiimalisha kikosi chake.

Habari hiyo inaendelea kueleza ya kwamba Unai Emery ana mpango wa kusajili wachezaji wasiopungua watatu katika dirisha kubwa la usajili.

Anatafuta kipa mwingine baada ya kipa mkongwe Petr Cech kutangaza kustaafu mwishoni mwa msimu, pia yupo sokoni kutafuta beki wa kushoto kwani inasemekana ya kwamba Nacho Monreal hatapewa mkataba mpya.

Pia kuondoka kwa Aaron Ramsey na Danny Welbeck kutafanya Arsenal kuwa pungufu katika nafasi ya kiungo mshambuliaji/winga hivyo atasajili mchezaji mmoja wa kuziba nafasi hiyo.

Ikumbukwe ya kwamba Arsenal ilisajili mchezaji mmoja tu katika dirisha lililopita, ambapo ilimpata kiungo Denis Suarez kutoka Barcelona kwa mkopo.

Kama habari hizo zitakuwa za kweli , litakuwa ni pigo kubwa kwa mashabiki wa Arsenal kwani wengi wao wanajua ya kwamba timu inahitaji kusajili wachezaji bora watakaoongeza ubora wa kikosi hasa katika nafasi za ulinzi.

Ili Arsenal iweze kupambana na timu zilizopo juu yetu ni lazima usajili wa maana ufanyike, kipa , beki wa kulia, beki wa kati, beki wa kushoto, kiungo mchezeshaji na winga. Hivyo wachezaji wasiopungua sita wanahitajika.

Je wewe unaonaje kuhusu taarifa hizi ? ni za kweli ? kama ni kweli unajisikiaje? tupia maoni yako hapo chini.

Henrikh Mkhitaryan aichezea timu ya vijana

Mchezaji wa kiungo wa Arsenal,Henrikh Mkhitaryan amepona na jana aliichezea timu ya vijana wa Arsenal kwa mara ya kwanza mwaka huu.

Henrikh Mkhitaryan aichezea timu ya vijana

Nahodha huyo wa Armenia aliichezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 katika mchezo dhidi ya timu ya vijana wenye umri kama huyo ya West Ham.

Katika mchezo huo Arsenal ilikuwa ikiongoza kwa ushindi wa goli 3-0 hadi kufikia mapumziko na mchezo haukuweza kuendelea katika kipindi cha pili baada ya mwamuzi kuuhairisha kutokana na hali mbaya ya uwanja.

Mkhitaryan,ambaye alitimiza miaka 30 tarehe 21 ya mwezi wa kwanza alikuwa nje ya uwanja tangu tarehe 19 ya mwezi wa 12 mwaka jana wakati alipoumia katika mchezo wa robo fainali ya kombe la Carabao dhidi ya Tottenham Hotspur.

Kurudi kwa Mkhi ni habari njema kwa timu ya Arsenal kwani katika siku za karibuni imekosa mtu wa kutengeneza nafasi za magoli na hivyo kuifanya safu ya ushambuliaji ya Arsenal kutokufunga magoli mengi.

Arsenal 1 – 3 Manchester City-Nilichokiona

Juzi jumapili Arsenal ilicheza na Manchester City na kufungwa kwa goli 3-1, najua kufungwa ni kubaya lakini baada ya kuangalia tena mchezo ule Arsenal haikufanya vibaya sana.

Arsenal 1 - 3 Manchester City-Nilichokiona

Arsenal walicheza vizuri katika mchezo ule na kuna dakika kama 20 hivi za kipindi cha kwanza nilikuwa nasema kama timu ikiendelea hivi hivi tunaweza kupata matokeo.

Ukiangalia goli la kwanza makosa yalianzia kwa Guendouzi ambaye alimpasia mpira Iwobi na ndani ya eneo la hatari la Arsenal, Guendouzi anaondoka ndani ya eneo akiamini ya kwamba Iwobi atapiga mbele, wachezaji wawili wa City wanamkaba Iwobi, hajui afanye nini, anapoteza mpira timu haijakaa vizuri tumefungwa goli la kwanza.

Arsenal walifanikiwa kuzawazisha goli lile ndani ya dakika chache na kubadilisha kabisa sura ya mchezo.

Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanamlaumu Stephan Lichtsteiner kwa goli la pili,mimi nimeangalia mpira ule kwenye luninga zaidi ya mara tatu,zilipigwa pasi za maana babu wa watu hakujua amkabe nani amuache nani, lile goli hakuna beki pale EPL angeweza kuzuia lisifungwe, kuna wakati lazima tukubali ya kwamba wapinzani ni bora kuliko sisi na juzi city walikuwa bora.

Goli la tatu la Manchester City lilikuwa ni la mkono, Sergio Aguero alikiri hilo baada ya mechi, pamoja na hayo bado lilikuwa goli zuri sana.

Arsenal hawakufanikiwa kipiga shuti hata moja golini katika kipindi cha pili, sio kwamba nawatetea ila naamini goli la tatu la Man City liliwavunja nguvu, naamini ya kwamba ingekuwa 2-1 hadi dakika ya 75 Arsenal wangeanza kuushambulia Man City kwa nguvu zaidi na pengine matokeo yangekuwa tofauti.

Pia kuna watu wanamtupia lawama kocha Unai Emery, binafsi sioni la zaidi ambalo angeweza kufanya, kwa kikosi alichonacho alifanya kila kitu ambacho ningependa kocha afanye. Kuna wataki mambo hayaendi kama unavyotaka na juzi ilikuwa moja ya hizo siku.

Timu bora ilishinda na sisi acha tujenge timu tuangalie kama mwakani tunaweza kuwakaribia, kwa sasa acha tuendelee kupambana na wenzetu akina Chelsea na Manchester United tuangalia kama tutapata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Manchester City Vs Arsenal-Mtazamo wangu

Manchester City Vs Arsenal-Mtazamo wangu

Leo Arsenal itakuwa wageni wa Manchester City katika mchezo wa raundi ya 25 ya ligi kuu ya Uingeleza.

Man City wanaingia katika mchezo huo wakiwa katika nafasi ya pili, pointi tano nyuma ya vinara wa ligi hiyo Liverpool hivyo watataka kushinda ili kuwasogelea Liverpool wanaocheza kesho.

Kwa upande wa Arsenal wao wanaingia katika mchezo huo wakiwa katika nafasi ya tano, pointi tatu nyuma ya Chelsea wanaoshika nafasi ya nne na ya mwisho ya kushiriki ligi ya mabingwa wa Ulaya, ili Arsenal iwapiku Chelsea itabidi ishinde mchezo wa leo kwa goli 5-0.

Hakuna mchambuzi hata mmoja anaeipa nafasi ya kushinda timu ya Arsenal, hata asilimia kubwa ya mashabiki wa Arsenal wanaamini ya kwamba tayari Arsenal imeshapoteza mchezo huu, huku baadhi yao wakisema ya kwamba Unai Emery apumzishe wachezaji wa kikosi cha kwanza kwani matokeo yanajulikana.

Mimi binafsi sikubaliani na hilo kwani naamini ya kwamba japo Manchester City ni bora kuliko Arsenal kwa sasa lolote linaweza kutokea na Arsenal anaweza kushinda mchezo wa leo, siku chache zilizopia Man City hawa hawa walifungwa na Newcastle United moja ya timu mbovu za ligi kuu.

Kwa sasa wapinzani wa karibu wa Arsenal ni Manchester United na Chelsea, Chelsea alishinda jana na ikitokea Man United wakashinda leo ina maana Arsenal watakuwa nafasi ya sita, hilo mimi halinitishi sana kwani baada ya mchezo wa leo Arsenal itakuwa imemaliza mechi katika viwanja vigumu.

Arsenal inasumbuka kupata matokeo viwanja vya ugenini kwa timu za Chelsea, Southampton,Man United,Liverpool Man City na Stoke City. Ukiondoa Stoke City ambao walishuka na Man City tunaocheza nao leo viwanja vingine vyote tumeshaenda na nyumbani huwa hatufungwi kizembe.

Chelsea bado hajacheza na Liverpool, Man City,Man United na Totenham, Man United bado hajacheza na Liverpool, Man City na watakuja Emirates (ingawa wanaweza kutufunga), hivyo timu hizo zitapoteza pointi tu na kuipa nafasi Arsenal ya kuingia nne bora.

Kuhusu kikosi naamini ya kwamba Leno ataanza golini, nasikia Niles hajasafiri na timu, yule babu kutoka Juventus sijawahi kumuamini, ningependa Carl Jenkinson aanze kulia huku Mustafi na Koscienly wakianza kati na kushoto akae Nacho Monreal.

kuna tetesi za kwamba Granit Xhaka atakosa mchezo huu, naamini Aaron Ramsey atanza kama kiungo wa kati akisaidiana na Lucas Torreira na Matteo Guendouzi, huku Mesut Ôzil au Denis Suarez akicheza nyuma ya Auba na Lacazete.

Kama nilivyosema, Man City ni timu nzuri ila inafungika na nina imani ya kwamba leo Arsenal ataondoka na pointi moja hivyo natabiri sare ya goli 2-2.

Je wewe una mtazamo gani kuhusu mchezo huu? tupia maoni na utabiri wako hapo chini.

Tetesi-Granit Xhaka kukosa mchezo wa leo

Tetesi-Granit Xhaka kukosa mchezo wa leo

Kuna tetesi zilizoibuka usiku wa jana ya kwamba mchezaji Granit Xhaka hajasafiri na timu kwenda Manchester na atakosa mchezo wa leo dhidi ya Manchester City.

Habari hizo zilivujishwa na mtandao wa Manchester Evening News ambao waliwapiga picha wachezaji wa Arsenal waliawasili tayari kwa mchezo huo.

Pia katika picha hizo wachezaji wawili, Henrikh Mkhitaryan na Ainsley Maitland-Niles walikosekana kitu ambacho kinaashiria ya kwamba mmoja kati ya tephan Lichtsteiner au Carl Jenkinson atacheza kama beki wa kulia ama beki mshambuliaji wa kulia (itategemea na mfumo atakaotumia mwalimu).

Laurent Koscienly ambaye alikosa mechi iliyopita dhidi ya Cardiff City kutokana na kuumia yupo katika kikosi hicho, pamoja na kiungo Mesut Ôzil ambaye amekuwa hapangwi sana katika mechi za hivi karibuni pia alionekana katika picha hizo.

Arsenal wamerudi katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kuu ya Uingeleza baada ya Chelsea kushinda kwa jumla ya magoli 5-0 jana, ili kurudi nafasi ya nne Arsenal itabidi iifunge Manchester City 5-0 leo, kitu ambacho kinawezekana kabisa.

Usajili wa Arsenal dirisha dogo la usajili-Mtazamo wangu

Dirisha dogo la usajili kwa mwaka huu lilifungwa alhamisi iliyopita na ufuatao ni mtazamo wangu kuhusu usajili wa Arsenal katika dirisha hili.

Usajili wa Arsenal dirisha dogo la usajili-Mtazamo wangu

Baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa Alhamisi iliyopita na Arsenal kufanya usajili wa mchezaji mmoja tu baada ya kiungo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi Denis Suarez akijiunga na timu kutoka Barcelona kwa mkopo wenye dhamani ya paundi milioni 2.

Taarifa zilizopo ni kwamba Arsenal wanaweza kumnunua mchezaji huyo moja kwa moja kwa dau la paundi milioni 18 katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Usajili wa Denis Suarez ni moja ya sajili za akili ambazo timu kama Arsenal inatakiwa kuzifanya, kwani mchezaji huyo akichemka watakua wametumia paundi milioni 2 tu na ikitokea afanya vizuri watampata kwa paundi milioni 20 tu, katika soko la sasa la wachezaji huwezi ukapata mchezaji wa bei poa zaidi ya hapo.

Suarez, mwenye umri wa miaka 25 ni mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi mbali mbali uwanjani, ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na amekuwa akifanya vizuri kila alipopewa nafasi, ingawa hakupata nafasi kubwa katika timu ya Barcelona.

Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanaouponda usajili huo na kudai ya kwamba Arsenal ina wachezaji wengi kwenye nafasi yake na mimi nina neno moja kwao, si kweli. soma sababu hapa chini.

Unai Emery anapenda kubadili mifumo kutokana na mchezo unavyoenda na mara nyingi amelazimika kubadilisha wachezaji wakati wa mapumziko, hii ni kutokana na wachezaji wengi kukosa uwezo wa kucheza nafasi nyingi kwa ufanisi ule ule, kwa mfano kiwango cha Ôzil akicheza kama winga ni tofauti kabisa na kiwango cha Ôzil akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Denis Suarez anaweza kucheza nafasi nyingi kwa ufanisi ule ule.

Pia Arsenal hii haina wachezaji wengi wenye uwezo wa kukokota mpira, kwa sasa ndani ya kikosi cha kwanza ni Alexi Iwobi tu anayeweza kuifanya hiyo kazi, hivyo ujio wa Denis Suarez mwenye uwezo wa kufanya hivyo utabadilisha jinsi Arsenal wanavyofanya mashambulizi.

Hii ndiyo sababu pamoja na Arsenal kuwa na matatizo katika nafasi nyingine lakini walikuwa sokoni kutafuta winga mwingine kama Yannick Carrasco na Ivan Perišić.

Katika dirisha hili la usajili tulishuhudia Arsenal ikijaribu kwa hali na mali kutafuta winga baada ya kuwapo na taarifa za kutaka kuwasajili Ivan Perišić na Yannick Carrasco, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na Arsenal kukosa pesa na hivyo kushindwa kufikia makubariano na timu zilizokuwa zinawamiliki wachezaji hao.

Kama kuna nafasi ambayo mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa wanategemea kuona usajili mpya ilikuwa ni nafasi ya beki wa kati. Kuumia kwa Rob Holding, Sokratis na Koscienly kuliifanya timu kuwa katika hali ngumu, kuongeza mchezaji mpya hata kwa mkopo katika nafasi hiyo kulionekana kama jambo la busara, lakini kulikuwa na sababu ya msingi kwa nini Arsenal hawakufanya hivyo.

Katika mahojiano na waadhishi wa habari, kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery alisema ya kwamba Arsenal ina mabeki wengi ndani ya kikosi hicho, alisema ya kwamba majeraha ya wachezaji wengi yalikuwa ni ya muda mfupi, na kama wangesajili mchezaji mpya na wale wa zamani kupona kila mchezaji angetaka kucheza na hali hiyo ingeleta matatizo mbeleni, ukiisoma hiyo kauli kwa makini utagundua ya kwamba kuna ukweli ndani yake.

Arsenal ina mabeki wa kati sita wenye mikataba mpaka mwaka 2020 au zaidi ya hapo ( hapa tunamhesabia na Calum Chambers ambaye ametolewa kwa mkopo). Hii namba ni kubwa kuliko timu zote 6 kubwa za ligi kuu ya Uingeleza.

Kusajili mchezaji mpya katika kipindi hiki ilikuwa ni vigumu kwa sababu kubwa mbili, moja mshahara na ada ya uhamisho na pia mchezaji mpya angetaka ahakikishiwe nafasi ya kucheza, hivyo walijaribu kutafuta mchezaji ambaye angeweza kuja kwa mkopo hadi mwisho wa msimu na walikosa.

Pamoja na hayo Arsenal watategemea kupona haraka kwa Sokratis na Koscienly kutoka kwenye majeraha ya muda mfupi na kuomba ya kwamba wawe fiti katika mechi zote zilizobakia za msimu huu.Mustafi yupo fiti na Konstantinos Mavropanos ameshapona na yupo tayari kuanza kucheza.

Arsenal hawajatumia pesa nyingi katika  dirisha hili la usajili lakini tukiwa wakweli hakuna timu kubwa iliyotumia pesa( ukiondoa Chelsea ambao nao walimsajili Gonzalo Higuain kwa mkopo).

Usajili wa Denis Unaleta maana ukichukulia na ukweli wa kwamba anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani na pia ana uwezo wa kucheza katika mifumo tofauti ambayo Unai Emery anatumia.

Cha msingi ni Arsenal kuhakikisha inamaliza ndani ya timu nne bora na kupata nafasi ya kushiriki katika ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao, na nina imani kubwa tutaona usajili wa maana hasa kwenye nafasi ya ulinzi katika dirisha lijalo la usajili wakati Arsenal itakapopata pesa.

 

Rasmi-Emile Smith Rowe ajiunga na RB Leipzig kwa mkopo

Mchezaji kinda wa Arsenal, Emile Smith Rowe leo amekamilisha taratibu za kujiunga na timu ya RB Leipzig kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.

Rasmi-Emile Smith Rowe ajiunga na RB Leipzig kwa mkopo

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 amefanya vizuri katika msimu wake wa kwanza katika timu ya wakubwa ya Arsenal baada ya kufunga magoli matatu katika michezo sita msimu huu.

Mchezaji huyo ambaye ni zao la chuo cha soka cha Arsenal, Hale End Academy, alijiunga na chuo hicho mwaka 2016 na mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 2017 alisaini mkataba wake wa kwanza na timu hiyo.

Pia kiungo huyo mshambuliaji alikuwa ni sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Uingeleza kilichotwaa kombe la dunia kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2017.

Tunamtakia kila la heri Emile Smith Rowe katika timu hiyo ya RB Leipzig.

Rasmi-Denis Suarez atua Arsenal

Timu ya Arsenal imetangaza ramsi usajili wa mchezaji wa kiungo wa timu ya Barcelona Denis Suarez kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.

Rasmi-Denis Suarez atua Arsenal

Denis Suarez mwenye umri wa miaka 25 anaungana tena na kocha Unai Emery kwani wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa Sevilla katika msimu wa 2014-2015.

Suarez tayari ameishaichezea timu ya Barcelona mechi 71 akiifungia magoli nane na amewahi kuichezea timu ya taifa  ya Hispania mara moja.

”Tuna furaha kubwa ya kumkaribisha Denis Suarez katika hii timu, ni mchezaji ambaye tunamfahamu vizuri kwani tulifanya naye kazi vizuri katika timu ya Sevilla” alisema kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery alipofanya mahojiano na mtandao wa Arsenal.com

Katika mahojiano ya kwanza ya Suarez kama mchezaji wa Arsenal, alionekana kufurahia kujiunga na timu hii ambapo alidai ya kwamba amekuwa akiifuatilia kwa muda mrefu.

Pia mchezaji huyo hakuchelea kutumia ukurasa wake wa twitter kuwashukuru wachezaji na mashabiki wa Barcelona huku akiwatakia kila la heri katika mechi zilizobaki msimu huu.

Mchezaji huyo alifanya mazoezi ya kwanza katika viwanja vya London Colney akiwa amevalia jezi namba 22 na anaweza kuanza kuichezea Arsenal katika mchezo dhidi ya Manchester City jumapili ijayo.

Arsenal wana uwezo wa kumsajili mchezaji huyo moja kwa moja kwa dau la paundi milioni 20.

Karibu Denis Suarez, Bienenido Denis Suarez #HolaDenis