Arsenal yaifunga Cardiff City

Arsenal jana ilifanikiwa kuifunga timu ya Cardiff City kwa jumla ya goli 2-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza uliofanyika katika uwanja wa Emirates.

Baada ya kufungwa na Manchester United katika kombe la FA, Arsenal ilikuwa ni muhimu kushinda jana ili kuendeleza matumaini ya kumaliza katika timu nne bora za ligi.

Goli la penati kutoka kwa Pierre Emerick Aubamayang na goli la juhudi binafsi kutoka kwa Alexandre Lacazette yalitosha kabisha kuihakikishia Arsenal point tatu muhimu.

Kabla ya goli la Auba mwamuzi wa mchezo huo Mike Dean aliikatalia Arsenal penati mbili za wazi na kuufanya uwanja mzima kumzomea.

Guendouzi alikichafua

Katika kipindi cha kwanza wachezaji wa Cardiff City walionekana wakitaka kumfanyia faulo nyingi Guendouzi kiasi cha kulalamika kwa refa na kuzawadiwa kadi ya njano, sijui nini kilitokea wakati wa mapumziko, lakini dogo alirudi na nguvu ya ajabu na kuupiga mpira mwingi sana kipindi cha pili.

Lacazette mchezaji bora wa mechi

Alexander Lacazette alipewa uchezaji bora wa mchezo wa jana, na mimi naamini alistahili kabisa tuzo hiyo kwani mwanaume jana akijituma sana, alikuwa akishuka kutafuta mipira, anapandisha timu na kutengeneza nafasi za kufunga, pia goli lake ni wachezaji wachache sana pale kwa bibi wanaweza kulifunga.

Baada ya ushindi huo Arsenal imefikisha pointi 47 ikiwa sawa na Chelsea yenye mchezo mmoja mkononi, mchezo ujao wa Arsenal utakuwa dhidi ya Machester City utakaofanyika katika uwanja wa Etihad jumapili ijayo.

#COYG

Christopher Nkunku akaribia kutua Arsenal

Kiungo wa PSG Christopher Nkunku anakaribia kutua Arsenal kwa mkopo wa miezi 6 huku Arsenal wakiwa na uwezo wa kumnunua moja kwa moja katika dirisha kubwa la usajili.

Christopher Nkunku akaribia kutua Arsenal

Taarifa za Arsenal kumtaka Christopher Nkunku zilianza juzi baada ya kuwapo kwa taarifa za kuvunjika kwa mazungumzo kati ya Arsenal na Barcelona kuhusu uhamisho wa Denis Suarez.

Jana mwandishi wa habari wa Italia DI Marzio alisema ya kwamba PSG walikuwa tayari kumuachia mchezaji huyo ila kwanza wanataka kusajili mchezaji mbadala.

Leo asubuhi niliona taarifa kutoka BBC wakisema hivyo hivyo ( BBC wanaaminika zaidi linapokuja suala la Arsenal) na leo jioni inasemekana ya kwamba PSG wanamfanyia vipimo Paredes, kama PSG watakamilisha usajili wa Paredes watakuwa tayari kumuachia Nkuku kuja Arsenal.

Nkuku mwenye umri wa miaka 22 ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati na pia kama beki mshambuliaji wa kulia.

Nkuku alifanya kazi na kocha wa Arsenal, Unai Emery wakati kocha huyo alipokuwa akiinoa timu hiyo kutoka nchini Ufaransa.

Je Arsenal itafanikisha usajili wa Nkuku? ni jambo la kusubiria na kuona.

Thierry Henry asimamishwa kazi na Monaco

Mshambuliaji mkongwe wa Arsenal, Thierry Henry amesimamishwa kazi na timu yake ya Monaco, wakati bodi ya timu hiyo ikiamua hatima yake leo usiku.

Thierry Henry asimamishwa kazi na Monaco

Hnery ambaye ni mmoja ya wachezaji waliowahi kuichezea timu ya Arsenal kwa mafanikio makubwa, aliteuliwa kuwa kocha wa Monaco miezi mitatu iliyopita na baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo 20 inaonekana ya kwamba muda wake umefikia tamati katika timu hiyo.

Katika taarifa fupi iliyotolewa na timu ya Monaco, Henry amesimamishwa kufanya kazi yeyote kama kocha wa kikosi cha kwanza hadi hapo uamuzi wa mwisho kuhusu hatima yake utakapofikiwa, mazoezi ya leo ya Monaco yatasimamiwa na “Franck Passi”.

Thierry Henry alipata kazi hiyo mwezi wa 10 mwaka jana akichukua nafasi ya Leonardo Jardim, lakini alishindwa kuibadilisha timu hiyo kwani katika michezo 20 alifanikiwa kushinda mara 4 tu, akitoa sare mara 5 na kuambulia vipigo mara 11.

Kusimamishwa/ kufukuzwa kazi ni sehemu ya maisha, tunakutakia kila la heri mkongwe Thierry Henry.

Emi Martinez ajiunga na Reading kwa mkopo

Golikipa wa tatu wa Arsenal, Emi Martinez amejiunga na timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza, Reading kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.

Emi Martinez ajiunga na Reading kwa mkopo

Emi Martinez ambaye ni mzaliwa wa Argentina ameichezea timu ya wakubwa ya Arsenal maraa 14 katika miaka 9 ya kuitumikia timu hiyo, kwani alisajiliwa akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 17 tu.

Mchezaji huyo ambaye alikuwa chagua la tatu la kocha Unai Emery msimu huu ameichezea Arsenal katika mchezo mmoja tu katika kombe la Europa League ambapo Arsenal iliishinda timu ya Qarabag kwa goli 1-0 katika uwanja wa Emirates.

Huku Petr Cech akistaafu mwisho wa msimu na Arsenal ikiwa sokoni kutafuta kipa mwingine, sioni nafasi ya Martinez ndani ya Arsenal, kwani ana umri kama wa Bernd Leno na kipa mpya anayetafutwa ana umri mdogo zaidi, hivyo uwezekano wa kupata namba unakuwa mdogo sana.

Kipa huyo tayari amekwisha zichezea kwa mkopo timu za Oxford United, Sheffield Wednesday, Rotherham United, Wolves na Getafe katika kujaribu kupata uzoefu wa kucheza katika kikosi cha kwanza.

Kwa umri alionao anastahili kucheza mara kwa mara ili aendelee kuimalika.

kila la heri Emi Martinez.

Tetesi-Arsenal yamtaka Emil Audero

Arsenal inataka kumsajili golikipa wa Sampdoria, Emil Audero ili aje kuchukua nafasi ya Petr Cech anatetazamiwa kustaafu mwishoni wa msimu huu.

Tetesi-Arsenal yamtaka Emil Audero

Emil Audero (pichani juu) anahusishwa na kuhamia Arsenal

Mwandishi maarufu wa habari za soka Gianluca di Marzio, ameandika katika tovuti yake ya kwamba Arsenal inataka kumsajili golikipa huyo anayeichezea Sampdoria.

Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 22 ni mali ya mabingwa wa Italia Juventus na yupo Sampdoria kwa mkopo, hivyo kama Arsenal watamtaka mchezaji huyo itabidi wakubaliane na Juventus.

Taarifa hizo zimeanza kuenea kwa kasi ya ajabu na sasa mtandao wa Skysport na baadhi ya vyombo vikubwa vya habari vya kiingeleza vimeweka taarifa hizo katika mitandao yao ya kijamii.

Audero amecheza mechi 20 katika ligi kuu ya Italia msimu huu ambapo mechi nane kati ya hizo hakuruhusu mpira kugusa nyavu zake.

Deloitte Football Money League-Arsenal yashika nafasi ya tisa kwa mapato

Kampuni ya Deloitte imetoa orodha ya timu tajiri na habari mbaya kwa mashabiki wa Arsenal ni kwamba Arsenal imeshuka na kushika nafasi ya tisa katika msimamo huo.
Deloitte Football Money League-Arsenal yashika nafasi ya tisa kwa mapato
Deloitte ambao kila mwaka huzipambanisha timu bora duniani na kuandaa orodha ijulikanayo kama Football Money League ambapo hupanga timu katika msimamo kutokana na mapato waliyoingiza katika mwaka huo wa soka.
Katika msimamo huo, Real Madrid wanaongoza  msimamo huo baada ya mapato yao kuongezeka kutoka £579.7m hadi £665.2m hii ni kutokana na kushinda taji la tatu la ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Timu nyingine kutoka la liga, Barcelona inashika nafasi ya pili, huku Manchester United wakishika nafasi ya tatu na nafasi ya kwanza kwa timu kutoka Uingeleza.
Kwa upande wa Arsenal imeshuka kwa nafasi tatu, ambapo mapato yamepungua kwa £20, sababu kubwa ya kupungua kwa mapato hayo kutokana na kukosa nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Timu zilizoingiza pesa nyingi katika msimu wa 2017/2018 (kwenye mabano ni kiasi walichoingiza mwaka 2016/17 ):
 
1. Real Madrid – £665.2m (£579.7m in 2016/17)
 
2. FC Barcelona – £611.6m (£557.1m in 2016/17)
 
3. Manchester United – £581.2m (£590m in 2016/17)
 
4. Bayern Munich – £557.4m (£505.1m in 2016/17)
 
5. Manchester City – £503.5m (£453.5m in 2016/17)
 
6. Paris Saint-Germain – £479.9m (£417.8m in 2016/17)
 
7. Liverpool – £455.1m (£364.5m in 2016/17)
 
8. Chelsea – £448m (£367.8m in 2016/17)
 
9. Arsenal – £389.1m (£419m in 2016/17)
 
10. Tottenham Hotspur – £379.4m (£308.9m in 2016/17)
 
11. Juventus – £349.8m (£348.6m in 2016/17)
 
12. Borussia Dortmund – £281m (£285.8m in 2016/17)
 
13. Atlético Madrid – £269.6m (£234.2m in 2016/17)
 
14. Inter Milan – £248.7m (£225.2m in 2016/17)
 
15. AS Roma – £221.5m (£147.6m in 2016/17)
 
16. Schalke – £216m (£197.8m in 2016/17)
 
17. Everton – £188.6m (£171.2m in 2016/17)
18. AC Milan – £184m (£164.7m in 2016/17)
 
19. Newcastle United – £178.5m (£85.7m in 2016/17)
 
20. West Ham United – £175.3m (£183.3m in 2016/17)
Kama msimamo wa Deloitte unavyoonesha, mapato ya Arsenal yamepungua huku matumizi yakiongezeka ndiyo maana wanakosa pesa za kununulia wachezaji wapya.

Mazungumzo kati ya Arsenal na Barcelona yavunjika

Mazungumzo kati ya timu za Arsenal na Barcelona juu ya uhamisho wa mchezaji Denis Suarez yamevunjika na kuna uwezekano mkubwa wa kwamba mpango kumsajili ukafa.

Mazungumzo kati ya Arsenal na Barcelona yavunjika

Gazeti la Mundo Deportivo limeandika ya kwamba timu hizo zilikuwa zimekubaliana ya kwamba mchezaji huyo ahamie Arsenal kwa mkopo na Arsenal walikuwa tayari kulia ada ya mkopo ya paundi milioni 2.

Kilichovunja mazungumzo hayo ni Barcelona kutaka kuweka kipengele ambacho kingeilazimisha Arsenal kumsajili Denis Suarez katika dirisha la usajili la majira ya joto, kitu ambacho Arsenal hawakukubaliana nacho.

Wakatarunya hao wakaamua kumgeukia Denis Suarez na kumtaka asaini mkataba mpya kabla ya kumruhusu kujiaunga na Arsenal kwa mkopo (mkataba kati ya Barcelona na Denis Suarez unaisha mwaka 2020, hivyo wakimuachia bila kusaini mkataba mpya ifikapo mwezi wa saba mwaka huu atakuwa amebakisha mwaka mmoja na dhamani yake kupungua).

Mchezaji huyo akagoma kusaini mkataba mpya na kuamua kubaki Hispania ambapo wakati wa dirisha la usajili la majira ya joto atafikia uamuzi wa timu ya kuichezea.

Habari mbaya-Hector Bellerin aumia kuwa nje miezi sita hadi tisa

Majeruhi yameendelea kuiandama timu ya Arsenal baada ya jana kutangaza ya kwamba beki wake wa kulia Hector Bellerin atakuwa nje kwa kipindi cha kati ya miezi sita na tisa.

Habari mbaya-Hector Bellerin aumia kuwa nje miezi sita hadi tisa

Hector Bellerin anakuwa mchezaji wa tatu wa Arsenal kuumia na kukosa mechi zote zilizobaki katika msimu huu, anaungana na Danny Welbeck na Rob Holding ambao waliumia mwishoni mwa mwaka jana.

Bellerin aliumia juzi wakati wa mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza dhidi ya Chelsea ambapo Arsenal ilishinda kwa jumla ya goli 2-0.

Vipimo vya awali vinaenesha ya kwamba atakosa michezo yote iliyobakia msimu huu na kuna uwezekano mkubwa akakosa miezi miwili ya msimu ujao.

Atafanyika vipimo vingine ndani ya siku chache zijazo ili kujua zaidi juu ya majeraha hayo.

Kuumia kwa Bellerin ni pigo kubwa sana kwa Arsenal kwani kwa miaka ya karibuni amekuwa tegemezi sana upande wa kulia na itakuwa kazi ngumu sana kupata mchezaji wa kuchukua nafasi yake.

Ukichuk

Rasmi Sven Mislintat kuondoka Arsenal

Timu ya Arsenal imetangaza ya kwamba mjerumani Sven Mislintat ataondoka tarehe nane ya mwezi ujao baada ya kuitumikia Arsenal kwa miezi 14 tu.

Rasmi Sven Mislintat kuondoka Arsenal

Katika taarifa rasmi katika tofuti ya Arsenal, hawakuweka wazi sababu za Sven Mislintat kuondoka licha ya kuandika ujumbe mfupi wa kumshukuru kwa kazi yake kubwa na kumtakia mafanikio huko aendako.

Mislintat ambaye anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kutafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa na kuweza kuwasajili kwa bei rahisi kiasi cha kupewa jina la utani la jicho la dhahabu.

Akiwa Arsenal aliweza kusaidia kupatikana kwa wachezaji ambao walikuwa hawajulikani kama Matteo Guendouzi na Mavporanos, pia inasemekana yeye ndiye aliyefanikiwa mpango wa kuwasajili wachezaji Pierre Emerick Aubamayang, Henrik Mkhitryan na Papa Sokratis.

Wakati akiajiliwa na Arsenal mnano tarehe moja ya mwezi wa 12 mwaka 2017 alionekana ya kwamba alikuwa mtu sahihi ambaye angeweza kuisaidia Arsenal kuvumbua vipaji hasa katika kipindi hiki ambacho timu haina pesa.

Pamoja na timu kutokuweka wazi sababu za kuondoka kwa Sven, mitandaoni kila mtu anajaribu kuweka sababu ambazo anaamini ndizo zilizosababisha kuondoka kwa Sven Mislintat.

Kutokupewa chezo cha mkurugenzi wa soka

Arsenal ipo mbioni kumteua mkurugenzi wa soka na taarifa tulizonazo ni kwamba bodi ya Arsenal inataka kumteua mtu ambaye ana uhusiano na Arsenal (mchezaji wa zamani) au mtu ambaye ana uhusiano mzuri na kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery.

Taarifa kutoka Brazil zinadai ya kwamba tayari Arsenal imeshawasiliana na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Mbrazil Edu ili achukue nafasi hiyo, ikumbukwe ya kwamba Edu ndiye mkurugenzi wa soka wa shirikisho la soka la Brazil, pia kuna taarifa za kwamba iwapo Edu atakataa nafasi hiyo atapewa winga wa zamani wa Arsenal, Marc Overmars ambaye ana cheo kama hicho katika timu ya Ajax Armsterdam.

Taarifa hizo zinaendelea kudai ya kwamba Sven alitegemea ya kwamba yeye ndiye ambaye angepewa cheo hicho na uamuzi wa bodi wa kutafuta mtu mwingine umemuuzi na ameamua kuachana na Arsenal kwani wanaonesha ya kwamba hawaudhamini mchango wake.

Kukosana na Emery na Raul

Baada ya kuondoka Wenger, Ivan Gazidis ndiye aliyekuwa mwamuzi wa mwisho kuhusu usajili wa Arsenal, na baadaye Gazidis naye akaondoka na rungu hilo likaangukia mikononi mwa mhispania Raul Sahleli.

Taarifa zilizopo ni kwamba wawili hao wanapishana aina ya wachezaji wanaotaka kuwasajili Arsenal, wakati Sven yeye anaamini sana katika namba za wachezaji ( magoli wanayofunga, asisti, dakika wanazokimbia nk) , Raul yeye anaamini sana katika mtandao alionao ndani na nje ya ulaya unaomuwezesha kupata wachezaji wengi.

Kuna taarifa za kwamba Sven alipinga usajili wa Denis Suarez, wakati Raul na Unai wanamtaka mchezaji huyo, ameona ya kwamba wachezaji anaowataka hawasajiliwi na Arsenal hivyo ameona ya kwamba bora aondoke.

 

Arsena kukosa pesa za usajili

Hili nililiona katika mtandao wa Reddit ambapo kuna jamaa anadai ya kwamba baada ya kukaa na Arsenal mwaka mmoja Sven hajarizishwa na uendeshwaji wa Arsenal na haoni kama ni timu yenye uelekeo mzuri na suala la timu kukosa pesa la usajili limemlazimisha kuondoka kwani anaamini hata akitafuta wachezaji wazuri Arsenal haiwezi kuwasajili.

Binafsi sijui sababu ipi kati ya hizo tatu ni ya kweli, ila nauheshimu uamuzi wake na kumtakia kila la heri aendako.

 

Tetesi-Arsenal yatuma maombi ya kumsajili Gelson Martins

Wakati zikiwa zimebaki siku 10 kufikia tamati kwa dirisha hili la usajili, timu ya Arsenal imehusishwa na usajili wa winga wa Atletico Madrid Gelson Martins.

Tetesi-Arsenal yatuma maombi ya kumsajili Gelson Martins

Kocha wa Arsenal Unai Emery yupo sokoni kutafuta wachezaji wa kukiimalisha kikosi chake hasa kwa upande wa mawinga na mabeki wa kati lakini kutokana na Arsenal kutokuwa na pesa za kufanya usajili kazi hiyo imekuwa ngumu maradufu kwani kwa sasa Arsenal inaweza kusajili kwa mkopo tu.

Gazeti maarufu la soka la Ureno O Jogo limeandika ya kwamba Arsenal imetuma rasmi maombi ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23.

Gelson Martins aliwasili katika timu ya Atletico Madrid msimu uliopita, lakini ameshindwa kuwika katika kikosi cha Diego Simeone kiasi cha kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

Inasemekana ya kwamba Atletico Madrid wapo tayari kumuachia mchezaji huyo kwa mkopo ili kumpisha Alvaro Morata ambaye wapo mbioni kumsajili kutoka Chelsea.

Iwapo mpango huo utafanikiwa Arsenal itamsajili mchezaji huyo kwa mkopo wa miezi 6 na kama atafanya vizuri wana mpango wa kumsajili moja kwa moja.

Wakati tetesi hizo za Martins zikipamba moto taarifa nyingine ni kwamba Arsenal imeshaafikiana na Barcelona kuhusu usajili wa Denis Suarez na bado mambo madogo madogo yanayokwamisha kutangazwa kwa usajili huo.

 

Mambo Matano niliyoyaona katika mchezo dhidi ya Chelsea

Arsenal ilirudi katika hali ya ushindi mwishoni mwa wiki baada ya kuifunga timu ya Chelsea kwa jumla ya magoli 2-0. Katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Emirates kuna mengi yalitokea lakini haya ni mambo matano niliyoyaona kwa upande wa Arsenal.

Master Unai Emery alionesha ustadi wake

Ninachompendea Unai Emery ni uwezo wake wa kubadilisha timu kulingana na aina ya mchezo unaocheza timu pinzani. Emery aliwasoma vilivyo Chelsea na akaja na mfumo ambao uliwafanya wachezaji muhimu wa Chelsea wapoteane.

Chelsea huwa wanacheza pasi nyingi kupitia kwa Jorginho, Emery alichofanya ni kumcheza Ramsey nafasi ya kiungo mshambuliaji na Ramsey aliitumia vizuri nafasi hiyo kwani kila alipokuwepo Jorginho, Ramsey alikuwepo, kuna kipindi nilimuona Jorginho akirusha mikono hewani kuonesha kukelwa na ukabaji wa Ramsey, kwa hilo nampa tano Master Unai Emery.

Wachezaji walionesha kupania kushinda mchezo huo

Tangu mwamuzi apulize kipenga cha kuanza kwa mchezo huo, wachezaji wa Arsenal walionesha nia ya kushinda mchezo huo, walikuwa wanakaba kwa nguvu na kwa pamoja na pia walicheza kwa umakini mkubwa, wangefanya hivyo dhidi ya West Ham sasa tungekuwa tunaongea hadithi tofauti.

Koscienly bado wamo

Mambo Matano niliyoyaona katika mchezo dhidi ya Chelsea

Baada ya kuumia na kukaa nje kwa muda mrefu, Koscienly alirudi uwanjani, kuna baadhi ya mechi hakucheza vizuri hadi kufikia hatua ya kwamba baadhi ya mashabiki wa Arsenal walikuwa wanataka asipangwe, lakini juzi aliwajibu kwani alicheza mchezo huo kwa kiwango kikubwa, alifanikiwa kumficha Eden Hazard na kupewa zawadi ya mchezaji bora wa mchezo.

Kuumia kwa Hector Bellerin kulipunguza radha ya ushindi

Pamoja ya mambo mazuri yote yaliyojitokeza katika mchezo huo, kuumia kwa beki wa kulia wa Arsenal, Hector Bellerin ni pigo kubwa sana kwa kikosi hicho, mchezaji huyo ambaye alikuwa ndiyo kwanza amerudi baada ya kukosa michezo kadhaa, ameumia tena na anaweza asicheza kabisa katika mechi zilizobaki msimu huu.

Mashabiki wa Arsenal waliimba jina la Olivier Giroud

Mwaka mmoja uliopita mchezaji wa kifaransa Olivier Giroud alijiunga na Chelsea akitokea Arsenal,na juzi alikuwa anarudi Emirates kwa mara ya kwanza akiwa na jezi ya Chelsea.

Wakati akijiandaa kuingia uwanjani uwanja mzima ulilipuka na kuanza kuimba na na na Giroud, mimi nikiwa mmoja ya mashabiki waliokuwa wakimtetea sana Giroud wakati akiwa Arsenal, nilifarijika kuona ya kwamba mashabiki wengi wanaudhamini mchango wa Giroud kwa Arsenal ingawa sikukubaliana na kuimba jina lake wakati mchezo unaendelea, wangefanyaje iwapo Giroud angeisaidia Chelsea kurudisha magoli na kushinda? kuimba sio mbaya ila wangeimba wakati mchezo umeisha wakati anaingia kumpigia makofi kungetosha.

Hayo ndiyo mambo matano niliyoyaona katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Chelsea, je wewe uliona mambo gani? tupia maoni yako hapa chini.