Kombe la Checkatrade-Vijana wa Arsenal watinga raundi ya pili

Timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 21 ya Arsenal jana ilifanikiwa kuingia raundi ya pili ya kombe la Checkatrade baada ya kuifunga timu ya daraja la pili, Forest Green.

Kombe la Checkatrade-Vijana wa Arsenal watinga raundi ya pili

Tyreece John-Jules pichani juu akishangilia baada ya kuifungia Arsenal goli

Joe Willock ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwafungia vijana hao bao la kwanza dakika ya 41 kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya mshambuliaji wa arsenal Bukaya Saka kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na  George Williams.

Dakika mbili baadaye alikuwa ni Joe Willock tena aliyefunga goli la pili baada ya kuimalizia pasi safi aliyopigiwa na Saka.

Wenyeji walifanikiwa kupata goli ya kufutia machozi katika dakika ya 60 kupitia kwa mchezaji aliyeingia kipindi cha pili  Dayle Grubb.

Mshambuliaji mwenye kipaji kikubwa kutoka katika chuo cha soka cha Arsenal, Tyreece John-Jules alifunga goli la tatu na kuihakikishia Arsenal ushindi katika mchezo huo.

Kutokana na ushindi huo timu hiyo ya vijana wa Arsenal imejihakikishia nafasi ya kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kufikisha pointi 6 katika michezo mitatu iliyocheza katika kundi G.

 

 

Arsenal vs Sporting Lisbon-Mtazamo wangu

Arsenal leo itashuka katika uwanja wa Emirates kupambana na timu ya Sporting Lisbon kutoka Ureno katika muendelezo wa michuano ya kombe la Europa League.

Arsenal vs Sporting Lisbon-Mtazamo wangu

Arsenal ambayo kwa sasa inacheza vizuri na haijafungwa katika mechi 14 ambapo imeshinda 12 na kutoka sare 2, mmoja ya michezo waliyoshinda ni ule dhidi ya timu hiyo uliofanyika wiki mbili zilizopita.

Ushindi katika mchezo wa leo sio tu kwamba utaihakikishia Arsenal nafasi ya kucheza raundi ya mtoano ya michuano hiyo pia utaihakikishia nafasi ya kwanza katika kundi hilo.

Umuhimu wa ushindi wa Leo

Ukiangalia ratiba inayoikabili Arsenal mwanzoni mwa mwezi wa 12 ni muhimu sana kushinda mchezo wa leo, kwani tarehe 29 ya mwezi huu itacheza na Vorska ugenini ambako ni mbali, siku tatu baadaye itacheza na watoto wa Pochetino, Totenham, na siku tatu baada ya hapo itacheza na Manchester United ugenini.

Ndani ya siku 6 itacheza na wapinzani wetu wakubwa kama tunataka kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao itakuwa ni muhimi sana kupumzisha wachezaji wote katika mchezo wa tarehe 29 dhidi ya Vorska na kuchezesha watoto, kitu ambacho kinaweza kufanyika iwapo tu Arsenal itakuwa imeshafuzu baada ya kushinda mchezo wa leo.

Taarifa za majeruhi

Nacho Monreal ameshaanza mazoezi na timu ya kwanza ila atakosa mchezo wa leo kwani hayupo tayari kucheza, Koscienly naye bado hayupo tayari kucheza,Elneny bado ni majeruhi na haijulikani ni lini atarudi, wachezaji wengine ukiondoa Dinos Mavporanos wote wapo safi kiafya na wanaweza kucheza katika mchezo wa leo.

Wachezaji vijana

Niliangalia mazoezi ya jana na vijana wawili walifanya mazoezi nao ni Emile Smith Rowe na Eddie Nketiah, kutokana na nilivyoona katika mitandao yao ya kijamii nina imani watakuwemo katika kikosi cha leo mmoja akianza na mwingine atakaa benchi. Willock alicheza jana katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 hivyo atakosa mchezo huu.

Kikosi

Hizi ni mechi za Mohamed Elenny lakini kutokana na kuwa majeruhi naamini Niles atachukua nafasi yake akisaidiana na Matteo Guendouzi pale kati.

Nategemea kikosi kitakachoanza kitakuwa cha nguvu akitumia wachezaje wengi wakongwe, hivi ndivyo ninavyoamini kikosi kitakavyokupangwa.

Cech; Lichtsteiner, Mustafi, Sokratis, Kolasinac; Niles, Guendouzi, Ramsey; Smith Rowe, Welbeck, Aubamayang.

Utabiri

Utakuwa ni mchezo mgumu kwani Sporting Lisbon watataka kushinda ili wajiongezee matumaini ya kupita ila naamini Arsenal itashinda kwa goli 3-1.

Hizo ndizo taarifa muhimu na mtazamo wangu kuhusu mchezo wa leo dhidi ya Sporting Lisbon, je wewe unatabiri nini? tupia maoni yako hapa chini.

Tumuongelee Rob Holding

Leo nataka nichukue nafasi hii nimuongelee kwa ufupi Rob Holding na kiwango chake alichokionesha msimuu huu. Pamoja na kwamba amekuwa haongelewi sana na vyombo vya habari, mchezaji huyo wa kiingeleza amefanya mambo mengi makubwa msimu huu.

Tumuongelee Rob Holding

Amekuwa akicheza kwa kiwango kizuri katika mechi nyingi sasa na tangu aanze kucheza katika timu ya kwanza upande wa ulinzi umeonekana kuimalika kwa kiwango cha kuridhisha.

Baada ya mchezo wa Liverpool kila mtu alikuwa anaongelea jinsi Xhaka na Torreira walivyowakimbiza viungo vya Liverpool, goli la Lacazette, jinsi Alex Iwobi alivyomfundisha Trent Anord soka na vitu kama hivyo, lakini ni wachache sana wanaoongelea jinsi Rob Holding alivyomuweka mfukoni mfungaji bora wa mwaka jana Moh Salah.

Angalia alichofanya dhidi ya Liverpool.

Katika tackle 6 alizojaribu 4 alifanikiwa.

Aliwanyang’anya mpira maadui mara 6.

Katika mipira 7 aliyojaribu kuokoa alifanikiwa mara 7.

Katika mipira 3 ya vichwa aliyojaribu alifanikiwa mara 3.

Alizuia pasi isimfikie mlengwa mara 2.

Hakucheza rafu hata moja, 0.

Alipiga pasi 81 na kati ya hizo 74 zilimfikia mlengwa maana yake ni kwamba asilimia 91.4 ya pasi zilifika alipotata zifike.

Ukumbuke ya kwamba alifanya yote hayo akipambana na safu ya ushambuliaji inayosikiwa ya kwamba ndiyo moto zaidi katika ligi kuu ya Uingeleza.

Pia inaonekana ya kwamba kwa sasa ndiye beki wa kati anayetegemewa sana katika timu ya Arsenal, kwani ukiangalia katika mechi dhidi ya Blackpool hakucheza, hii inaonesha imani kubwa aliyonayo kocha Unai Emery kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 tu.

Kuna kitu kingine ambacho nilikiona katika mchezo huo, wakati Rob Holding akipiga pasi kwa mchezaji mwingine anafanya hivyo kwa kasi tofauti na Mustafi ambaye pia alicheza katika mchezo huo.

Sio kwamba nasema ya kwamba Mustafi alicheza vibaya, binafsi naamini ule ulikuwa ni moja ya micheza ambaye Mustafi amecheza kwa kiwango cha hali ya juu, ila nilikuwa najaribu kuonesha tofauti kati ya mabeki hao wawili.

Hata walipokuwa wakipigiana pasi kati yao utaona mpira ukienda kwa kasi kwa kutoka kwa Holding kwenda kwa Mustafi kuliko unavyotoka kwa Mustafi kwenda kwa Holding.

Kwa wale watu waliocheza mpira wanajua ya kwamba mpira ukija kwa nguvu ni rahisi zaidi kupiga pasi upande wowote ule bila ya kuutuliza, kitu ambacho ni muhimu katika kuanzisha mashambulizi ya kustukiza ama kucheza emeryball.

Pia lilikuwa ni jambo la kufurahisha kuona ya kwamba wachezaji waliokulia katika timu ya Arsenal, Hector Bellerin na Alex Iwobi wakifanya vizuri sana msimu huu chini ya mwalimu Unai Emery.

Hayo ndiyo niliyoyaona kuhusu Rob Holding jumamosi iliyopita na nikaamua leo wacha niyaongelee kidogo, kesho tunacheza na Sporting Lisbon ambapo ushindi utamaanisha ya kwamba Arsenal itafuzu hatua ijayo ya Europa ligi kama kiongozi wa kundi.

Rob Holding you know, he is better than Cannavaro

#COYG

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Arsenal ilicheza soka la kiwango kikubwa katika mchezo ambao uliishia kwa sare ya goli 1-1 dhidi ya Liverpool.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Goli la kusawazisha kutoka kwa mshambuliaji wa Arsenal, Alexandre Lacazette lilimaanisha ya kwamba Arsenal wangeondoka na pointi moja katika mchezo huo uliokuwa mkali na na kusisimua.

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kucheza vizuri lakini Liverpool ndio waliopata nafasi nzuri zaidi za kufunga, kwani walicheza kwa kujihami na kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Kama nilivyosema asubuhi, sehemu ya kiungo ndiyo sehemu ambayo ingeamua matokeo na Lucas Torreira alimpoteza kabisa Fabinho na kutawala eneo la katikati ya uwanja.

Kipindi cha kwanza Liverpool waligongesha miamba mara mbili kupitia kwa wachezaji  Roberto Firmino na Virgil van Dijk.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Arsenal walikianza kipindi cha pili kwa nguvu lakini walikuwa ni Liverpool waliopata goli la kuongoza baada ya golikipa wa arsenal Bernd Leno kufanya makosa ambapo aliutema vibaya mpira na kumkuta James Milner ambaye aliipatia Liverpool goli la kuongoza.

Mabadiliko yaliyofanya na kocha wa Arsenal Unai Emery, ya kumtoka Henrik Mkhitryan na kumuingiza Alex Iwobi yaliisaidia sana Arsenal kwani ilianza kufanya mashambulizi ya hatari zaidi kiasi cha Liverpool kupaki basi.

Alikuwa ni mshambuliaji wa Arsenal,Alexandre Lacazette aliyeipatia Arsenal goli la kusawazisha katika dakika ya 82 baada ya kuwazunguka mabeki wa Liverpool na kupiga shuti kifundi ambalo kipa wa Liverpool,Allison hakuweza kuliona.

Hadi mwisho wa mchezo Arsenal 1-1 Liverpool.

Baada ya kuisha kwa mchezo huo nilifanikiwa kuongea na baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambapo wengi wao walionekana kuridhika na hali ya kujituma kulikooneshwa na timu yao na pia wengi wanaamini ya kwamba Arsenal ilishahili kushinda mchezo huo.

Kwangu mimi Granit Xhaka ndiye aliyekuwa mchezaji nyota katika mchezo wa leo kwani yeye na Lucas Torreira walidhibiti sehemu ya kiungo, Xhaka alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote, aliondoa mipira mingi ya hatari na pia alimsaidia sana Sead Kolasinac upande wa kushoto.

Baada ya mchezo wa leo, Arsenal itaingia dimbani tena Alhamisi ijayo kupambana na timu ya Sporting Lisbon katika michuano ya kugombea kombe la Europa League.

Pia sare ya leo inamaanisha Arsenal imecheza michezo 14 bila ya kufungwa, ikishinda 12 na kutoka sare katika michezo miwili.

Kwa wale ambao hawakuona mchezo huo hapo chini kuna video inayoonesha vipande muhimu vya mchezo huo na magoli yote mawili.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Arsenal leo itakuwa na kibarua kigumu wakati watakapowakaribisha vijana wa Jurgen Klop, Liverpool katika uwanja wa Emirates.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Pamoja na Arsenal kucheza michezo 13 bila ya kufugwa (imeshinda 12 na kutoka sare 1) bado wachambuji wengi wa soka hawaipi nafasi ya kushinda katika mchezo wa leo. Ukweli ni kwamba  kuna baadhi mashabiki wa Arsenal wanaoamini ya kwamba Arsenal itapoteza mchezo huu.

Ni kweli kwamba Liverpool chini ya Klop wameimalika sana hasa baada ya kumsajili beki kisiki kutoka Southampton Virgil Van Dijk na golikipa Allison. Wakati Arsenal ndio kwanza wana miezi mitatu tangu waanze kujipanga.

Nimekuwa nikiwaangalia Liverpool katika mechi zao nyingi msimu huu, nikiwa mkweli sio timu ya kutisha sana kama wachambuzi wengi wanavyotaka tuamini, kuna mechi dhidi ya Leicester na Huddlefield walishinda kibahati, pia safu yao ya ushambuliaji sio kali kama mwaka jana, ingawa safu yao ya ulinzi imeimarika sana.

Rekodi

Unai Emery amewahi kuifunga Liverpool ya Klop kwenye fainali ya kombe la Europa League baada ya kumzidi ujanja Klop katika kipindi cha pili, Ingawa Arsenal haijawahi kuifunga Liverpool tangu ianze kufundishwa na Klop.

Liverpool imeshinda mara mbili tu katika michezo kumi na nane iliyofanyika Emirates na Arsenal haijaifunga Liverpool katika michezo 6 ya mwisho.

Vikosi

Wao wana Allison ambaye si kipa mbaya lakini anafaungika,ikumbukwe ya kwamba ni kipa ambaye amecheza michezo 100 tu ndani ya miaka mitano iliyopita na kati ya hiyo 50 ilikuwa ni mwaka jana, pia ikumbukwe ya kwanza alikuwa anawekwa benchi na Wojciech Szczęsny.Kwenye suala la makipa naamini ngoma droo.

Linapokuja kwenye mabeki hapo ndipo vijana hao wa Klop wanapoishida Arsenal, kusajiliwa kwa Van Dijk na Allison kumewaimalisha sana, siku hizi hawafungwi magoli ya kijinga kama zamani,Arsenal ina majeruhi wengi upande wa mabeki, sina taarifa kama Kolasinac, Monreal,Sokratis na Bellerin wamepita vipimo vya afya, kama hawajapita inaweza ikawa jioni mbaya sana kwa sisi mashabiki wa Arsenal.

Kwenye kiungo naamini Torreira, Xhaka na Ôzil ni bora kuliko kiungo chote cha Liverpool kama huamini subiri baadaye uone, ila kutokana na beki kuwa mbovu itabidi viungo wa Arsenal wacheze kwa juhudi kubwa kama Arsenal inataka kushinda mchezo wa leo.

Linapokuja kwenye ushambuliaji naamini hakuna tofauti kubwa sana wao wana Manè , Bob Firminho na Moh Salah na sisi tuna Auba,Lacazette na Iwobi.

Utabiri

Ni mchezo mgumu sana kutabiri, lakini naamini katika uwezo wa kikosi cha Arsenal na pia nina imani na kocha Unai, kama nilivyosema tuna kiungo bora kuliko Liverpool na hapo ndipo tunapoweza kuwafungia, ingawa sina imani na safu ya ulinzi kama inaweza kuwazuia Moh Salah na wenzie.

Naani mchezo wa leo utakuwa na magoli mengi na Arsenal itashinda na kuwafunga midomo wapinzani wote waliokuwa wanadai tunazifunga timu dhaifu, naamini Arsenal atashinda kwa goli 3-2.

Je wewe una maoni gani? tupia maoni yako na utabiri hapo chini.

 

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Mchezaji na nahodha wa zamani wa Arsenal,  Per Mertesacker amepandishwa cheo na sasa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Arsenal.

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Katika mahojiano na gazeti la Telegraph,Mkuu wa kitengo cha soka katika timu ya Arsenal,Raul Sanllehi alisema ya kwamba Per Mertesacker amejiunga na timu ya wakurugenzi wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa  Raul Sanllehi uteuzi wa Matersacker ni sehemu ya jitihada za uongozi wa Arsenal kuongeza watu wa soka katika ngazi za juu za uongozi wa Arsenal.

Mertesacker anakuwa mtu wa nne ambaye anajua soka kujiunga na timu ya wakurugenzi 15 ambao kwa sasa ndio wanaofanya maamuzi yote yanayoihusu Arsenal kwa sasa.

Kiongozi mwandamini wa Arsenal,Vinai Venkatesham anasema ya kwamba Per anajiunga na Huss Fahmy, Sven Mislintat,na Raul Sanllehi kama vichwa vya soka katika uongozi huo.

Sanllehi hakuweza wazi kama Mertesacker ataendelea na majukumu yake kama mkuu wa kituo cha soka cha Arsenal cha Hale End, lakini tunaamini ya kwamba ataendelea na majukumu yake kama kawaida kwani wakurugenzi wote wa Arsenal wana majukumu tofauti ndani ya Arsenal na sioni sababu kwa nini iwe tofauti kwa Mertesacker.

Kuongezwa kwa Per mwenye uzoefu mkubwa kama mchezaji kwani ameichezea Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani michezo mingi na pia amewahi kushinda kombe la dunia ni jambo zuri kwa timu kwani miaka miaka ya karibuni timu imekuwa ikufanya maamuzi ya ajabu hasa linapokuja suala la mikataba ya wachezaji.

Je unasemaje kuhusu uteuzi huo? tupia maoni yako hapa chini.

Kombe la Carabao: Arsenal kucheza na Totenham robo fainali

Baada ya kutinga robo fainali ya kombe la Carabao, Arsenal imepangiwa kucheza na mahasimu wao wakubwa Totenham Hotspurs.

Kombe la Carabao: Arsenal kucheza na Totenham robo fainali

Katika mchezo huo uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Emirates mwishoni mwa mwezi utakuwa ni kipimo tosha kwa vijana wa Unai Emery kwani kwa miaka mitatu sasa Totenham wamekuwa wakicheza vizuri.

Ikumbukwe ya kwamba Arsenal ilitinga fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na kufungwa na timu ya Manchester City.

Ratiba kamili ya michuano hiyo

Arsenal v Tottenham

Leicester/Southampton v Manchester City

Middlesbrough v Burton

Chelsea v Bournemouth

Mchezo kati ya Leicester na Southampton uliahirishwa baada ya kutokea ajali ya Helikopta katika uwanja wa King Power na kuua watu watano akiwemo mmiliki wa timu hiyo.

Arsenal yatinga robo fainali ya kombe la Carabao

Timu ya Arsenal imefanikiwa kuifunga timu ya Blackpool kwa jumla ya magoli 2-1 na kufanikiwa kuingia robo fainali ya kombe la Carabao.

Arsenal yatinga robo fainali ya kombe la Carabao

Baada ya kulazimishwa sare na Crystal Palace,Arsenal wamezinduka na kufanikiwa kuifunga timu ya ligi daraja la kwanza ya Blackpool kwa goli 2-1 katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Emirates.

Arsenal ilianza mchezo huo taratibu lakini ilifanikiwa kujipatia goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza baada ya kiungo Matteo Guendouzi kupiga bonge la pasi lililomaliziwa na beki wa kulia  Stephan Lichtsteiner.

Hadi mapumziko Arsenal ilikuwa bado inaongoza kwa goli hilo moja.

Kipindi cha pili Arsenal ilicheza kwa kujiamini zaidi na alikuwa ni kinda Emile Smith Rowe aliyeipatia Arsenal goli la pili baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Cark Jenkinson, ukagonga  mwamba na kurudi uwanjani.

Wakati Arsenal wakiendelea kutawala mchezo huo, kiungo Matteo Guendouzi alipewa kandi nyekundu yenye utata baada ya kupewa kadi mbili za njano kwenye mazingira ya kutatanisha.

Dakika 10 baada ya Guendouzi kutoka, Blackpool walipata goli lao la kwanza baada ya mchezaji O’Connor kuifungia timu hiyo baada ya kumalizia kwa kichwa kona iliyopigwa na Jordan Thompson.

Baadaye kidogo Blackpool walikaribia kupata goli la pili baada ya golikipa wa Arsenal, Petr Cech kujaribu kumpiga chenga Jay Spearing, lakini mchezaji huyo alifanikiwa kumpoka Cech mpira huo na kumpasia Nathan Delfouneso ambaye alifunga lakini goli hilo lilikataliwa na mwamuzi kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ameotea.

Matumaini ya Blackpool ya kusawazisha katika mchezo huo yalipotea baada ya mchezaji   O’Connor kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Arsenal,Pierre-Emerick Aubameyang.

Baada ya ushindi huo Arsenal itacheza na Totenham katika robo fainali ya michuano hiyo.

Mechi ijayo ni dhidi ya Liverpool jumamosi ijayo.

#COYG.

Kama unataka kuangalia tena magoli au hukuyaona cheki hapo chini.

 

Arsenal vs. Blackpool: Watoto wapewe nafasi

Arsenal leo wanacheza na timu ya Blackpool katika raundi ya nne ya kombe la Carabao na ufuatao ni mtazamo wangu kuelekea mchezo huo.

Arsenal vs. Blackpool: Watoto wapewe nafasi

Arsenal inacheza na Liverpool katika mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza jumamosi hii, lakini kabla ya mchezo huo leo itacheza na timu ya Daraja la kwanza Blackpool katika kugombea kombe la Carabao.

Bila kuwadharau Blackpool, mchezo dhidi ya Liverpool ni wa muhimu zaidi kama Arsenal inataka icheze katika ligi ya mabingwa msimu ujao. Pia kufungwa na Liverpool kutapunguza sana hali ya kujiamini kwa wachezaji na mashabiki pia wanaoichukia Arsenal watapata la kuongea na kusema si mnaona tulisema wanazifunga timu ndogo tu.

Hivyo ni muhimu mno kwa kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery akawapa nafasi makinda kutoka timu ya vijana na kupumzisha wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.

Nikiwa mkweli ni kwamba Arsenal imekuwa ikichezesha kikosi cha kwanza katika mechi zote msimu huu na timu ikiwa imecheza mechi tatu za Europa League na moja ya kombe la karabao kuna wachezaji kama Eddie Nketiah na Willock hawajacheza hata dakika moja na timu ya wakubwa.

Katika mazoezi ya jana niliwaona wachezaji vijana wanne tu ambao ni Emile Smith Rowe, Joe Willock, Julio Pleguezuelo na Eddie Nketiah.Lingekuwa ni jambo jema kama wote wanne wangeanza huku nafasi zilizobaki zikijazwa na wachezaji wenye uzoefu.

Kikosi ambapo ningependa kianze leo ni kama ifuatavyo:

Cech, Maitland-Niles, Holding, Julio Pleguezuelo, Jenkinson, Ramsey, Guendouzi, Welbeck, Nketiah, Willock, Smith Rowe.

Lakini naami ya kwamba Unai Emery atapanga kama ifuatavyo:

Cech, Maitland-Niles, Holding, Mustafi, Jenkinson, Ramsey, Guendouzi, Aubameyang, Mkhitaryan, Welbeck, Smith Rowe.

Bila kujali nani anaanza naamini Arsenal itapata ushindi kesho na kufuzu katika hatua ya raundi ya tano ya kombe hili.

#COYG

Kombe La Carabao-Petr Cech kuanza

Arsenal leo itacheza na timu ya Blackpool katika raundi ya nne ya kuwania kombe la Carabo, na katika kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery amedhibitisha ya kwamba golikipa Petr Cech ataanza katika mchezo huo.

Kombe La Carabao-Petr Cech kuanza

Cech ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa mwezi muda baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Watford mwezi uliopita ambapo nafasi yake ilichukuliwa na kipa Bernd Leno ambaye alifanya vizuri katika michezo yote aliyocheza.

Lakini Unai Emery ameamua kumpumzisha Leno wakati Arsenal itakapoikaribisha timu hiyo ya ligi daraja la kwanza la Uingeleza.

Akiongea na kituo cha luninga cha Sky Sports Emery alisema.

“katika kila mchezo tutawapa nafasi makipa wetu nafasi ya kutusaidia ili kupata ushindi, tunaangali hali ya kujiamini kutoka katika kila golikipa tuliyenaye.”

“Lakini kwa sasa,Petr Cech ataanza katika mchezo dhidi ya Blackpool, baada ya kupona majeraha aliyokuwa nayo”
Alimalizia kocha huyo wa Arsenal.

 

Taarifa za wachezaji majeruhi Arsenal

Timu ya madaktari wa Arsenal leo kupitia tovuti ya timu walitoa taarifa kuhusu wachezaji majeruhi wa Arsenal, taarifa hizo ni kama ifuatavyo.

Taarifa za wachezaji majeruhi Arsenal

Nacho Monreal

Nacho ana matatizo ya msuli na leo anafanyiwa vipimo ili kuangalia uwezekano kama anaweza kucheza kesho ama la.

Sead Kolasinac
Kolasinac naye ana tatizo kama la Monreal naye atafanyiwa vipimo leo, pia kuna taarifa ya kwamba leo alifanya mazoezi kama kawaida na kikosi cha kwanza.

Hector Bellerin
Aliumia katika mchezo dhidi ya Palace, atakosa mchezo wa kesho, ila atafanyiwa vipimo kuangalia uwezekano wa kucheza katika mchezo dhidi ya Liverpool.

Mo Elneny
Ni majeruhi na anategemewa kurudi uwanjani ndani ya wiki mbili, hivyo kukosa michezo kama minne hivi.

Laurent Koscielny
Ameanza mazoezi na timu ya kwanza baada ya kuumia kifundop cha mguu, haijulikani lini atacheza mechi ya ushindani.

Dinos Mavropanos

Yupo katika hatua za mwisho za kupona anategemea kuanza mazoezi kamili mwezi ujao.

Katika michezo miwili sasa Arsenal ilicheza bila beki wa kushoto na kumlazimisha Granit Xhaka kucheza nafasi hiyo, ingawa hakufanya vibaya litakuwa jambo jema kama mabeki wa kushoto watarudi katika mchezo wa kesho.

Tukutane kesho Arsenal Vs Blackpool.