Bournemouth 1-2 Arsenal-Arsenal yaanza kushinda tena

Baada ya kutoka sare katika michezo mitatu ya ligi kuu, Arsenal imeanza kushinda tena baada leo mchana kuifunga timu ya Bournemouth kwa jumla ya goli 2-1.

Bournemouth 1-2 Arsenal-Arsenal yaanza kushinda tena

Arsenal iliingia uwanjani na mfumo tofauti na uliozoeleka wa 4-2-3-1 na kucheza 3-4-3 huku Mesut Özil na Aaron Ramsey wakikaa benchi na Lacazette akikosa kabisa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.

Kama kawaida Arsenal walianza mchezo huo kwa kasi ndogo hali iliyowafanya Bournemouth wautawale mchezo huo katika dakika 30 za mwanzo.

Pamoja na Arsenal kutokucheza vizuri sana lakini ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli, baada ya beki wa Bournemouth,Jefferson Lerma kujifunga katika harakati za kuokoa, kwa mtazamo wangu hilo ni goli bora zaidi la kujifunga nililowahi kuliona,bonge la goli.

Baada ya goli hilo, Arsenal walianza kucheza vizuri lakini kabla refa hajapuliza kipenga cha kumaliza kipindi cha kwanza Alex Iwobi alipoteza mpira ndani ya eneo la hatari la Bournemouth na timu hiyo kufanya shambulizi la kustukiza na kuwakuta wachezaji wa Arsenal wakiwa hawajajipanga na kuifanya timu hiyo kufunga goli la kusawazisha.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana goli 1-1.

Kipindi cha pili Arsenal ilianza kwa kasi na Bournemouth walirudi nyuma hatua moja hali iliyosaidia Arsenal kupata goli la pili na la ushindi lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Gabon, Pierre Emerick Aubamayang.

Pamoja na timu zote kufanya mabadiliko matokeo ya mchezo huo hayakubadilika hivyo hadi mwisho Bournemouth 1-2 Arsenal.

Baada ya ushindi huo Arsenal imefikisha michezo 17 bila ya kupoteza na Alhamisi itaelekea nchini Ukraine kucheza na timu ya Voskla katika raundi ya tano ya kombe la Europa League.

Kwa sasa Arsenal inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kuu ya Uingeleza, ikiwa na pointi moja nyuma ya Chelsea waliopoa nafasi ya nne na pointi tatu dhidi ya Totenham waliopoa nafasi ya tatu.

Mchezo ujao wa ligi utakuwa jumapili ijayo ambapo Arsenal itawakaribisha wapinzani wao wa jadi Totenham katika uwanja wa Emirates.

Hapo chini nimekuwekea video yenye magoli yote na matukio muhimu ya mchezo huo, uwe na jumapili njema mdau.

Speak Your Mind

*