Bournemouth vs Arsenal-Henrikh Mhkitaryan aliibeba Arsenal

Mara baada ya mchezo wa juzi kumalizika mashabiki wengi wa Arsenal walianza kumponda kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Henrikh Mhkitaryan.

Iwe kwenye twitter, facebook au WhatsApp asilimia kubwa ya mashabiki hao walionekana kutoridhishwa na kiwango cha mchezaji huyo hadi wengine wakisema biashara kati ya Arsenal na Manchester United ya kubadilishana Sanchez na Mhkitaryan ilikua ndiyo biashara mbovu kabisa kuwahi kutokea duniani.

Je madai hayo yana ukweli ? niliamua kuingia msituni na kufanya uchunguzi wa kina na haya ndiyo majibu niliyoyapata, wengi wao walikosea kwani Mhkitaryan alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliofanya kazi kubwa sana katika mchezo huo.

Sintokaa hapa nikuandikie maneno tu, nitakuwekea pia na ushahidi katika mambo matano ambayo aliyafanya vizuri na kuchangia kwa asilimia kubwa katika ushindi huo, twende kazi.

Alianzisha mnyororo wa goli la ushindi

Ukirudi nyuma na kuangalia goli la pili na la ushindi la Arsenal lilivyopatikana utaona ya kwamba mpira ulianzia kwa Henrikh Mhkitaryan (ulikuwa ni mpira uliokufa baada ya Lerma kufanya faulo) yeye alimpasia Xhaka, ambaye alimpatia Iwobi aliyepiga pinpoint pasi iliyomkuta Kolasinac ambaye aliujaza ndani ya 18 na Auba akauzamisha wavumi. angalia picha ya hapo chini utaelewa zaidi.

goli la pili la Arsenal

goli la pili la Arsenal

Alikuwa kila sehemu

Kama ulikuwa hujui ni kwamba mchezo wa juzi dhidi ya Bournemouth ndiyo mcheza ambao Arsenal wamekimbia zaidi msimu huu, katika mchezo huo wachezaji wa Arsenal walikimbia kilometa 121.6, katika mchezo huo wachezaji watatu tu ndiyo waliokimbia daidi ya kilometa 12 ( ni mara chache sana wachezaji kuvusha kilometa 12 ndani ya dakika 90).

Katika mchezo huyo Henrikh Mhkitaryan alikumbia kilometa 12.3 na kushika nafasi ya 2 nyuma ya Hector Bellerin (angalia picha hapo chini), na sio kwamba alikimbia tu pia alikimbia maeneo muhimu (soma pointi inayofuatia)

wachezaji waliokimbia zaidi

Aliunganisha vizuri kati ya mabeki wa washambuliaji

Kama nilivyosema awali sio kwamba Henrikh Mhkitaryan alikuwa kila sehemu, pia alifanya kazi kubwa sana katika kiungo.

Kazi ya kuunganisha washambuliaji na mabeki mara nyingi huifanya Granit Xhaka lakini juzi mchezaji aliyeifanya kazi hiyo alikuwa ni Mhki, Hii ilitokana na kocha Emery kuamua kumchezesha chini zaidi kuliko kawaida.

Ukiangalia katika karatasi la timu, yeye anaanza kama kiungo mshambuliaji, lakini ukiangalia jinsi sehemu alizopokelea pasi utaona kabisa ya kwamba anapokea pasi kutoka nyuma zaidi.

pasi alizopokea mhkitaryan

Ukiangalia kwa karibu picha ya hapo juu utaona ya kwamba Mhki alipokea pasi 11 kutoka kwa Mustafi (ambaye alicheza kama beki wa kati) na pia alipokea pasi 10 kutoka kwa Torreira (kiungo mkabaji). Tofauti na kiungo mshambukiaji mwingine katika mchezo huo (Alex Iwobi) ambaye alipokea pasi tatu tu kutoka kwa Rob Holding na nne tu kutoka kwa Torreira (angalia picha ya hapo chini).

iwobi passes to

Pia katika mchezo wa juzi Arsenal walipiga pasi nyingi zaidi ndani ya eneo la hatari la adui (asilimia 33) huku Iwobi na Mhkitaryan wakiongoza katika eneo hilo.

Alicheza vizuri mfumo wa 3-4-3

Antonio Conte na timu yake ya Chelsea ndiyo waliupa umaarufu huu mfumo katika ligi kuu ya Uingeleza mwaka juzi, kama uliwaangalia Chelsea vizuri mwaka ule utagundua ya kwamba alikuwa akiwachezesha Hazad na Wilian au Hazad na Pedro kama viungo washambuliaji, wachezaji wote watatu wana sifa kubwa moja, wanaweza kucheza kama viungo washambuliaji wa kati na pia wana uwezo wa kucheza kama mawinga.

Henrikh Mhkitaryan aliitendea vyema nafasi hiyo kwani hicho ndicho alichokifanya (angalia tena picha ya pasi alizopokea hapo juu), katika Arsenal hii ni wachezaji wawili tu wenye uwezo huo nao ni Alex Iwobi na Mhki na ndiyo maana wote wawili walianza hiyo juzi.

Anaweza soka la kibabe

Katika mchezo wa wiki mbili zilizopita dhidi ya Wolves, mwalimu Emery aliamua kumtoa Mesut Ôzil na kumuingiza Mhki na watu wengi hawakuelewa kwa nini alifanya hivyo.

Sababu kubwa ilikuwa ni kwamba Wolves waliamua kurudi nyuma na kuzuia, walikuwa wakitumia nguvu nyingi na pia walikuwa wakiacha nafasi finyu kati yao.

Ukitaka Ôzil aache kucheza mpira anza kumchezea rafu au kutumia nguvu, Ôzil yeye hutumia akili zaidi ila kuna sehemu na wakati nguvu zinahitajika na Mkhi analiweza hilo.

Juzi pia kocha huyo aliamua kumuacha katika benchi Ôzil na kumuanzisha Mhki na baada ya mchezo aliulizwa sababu kwa nini alimuacha Ôzil benchi, jibu lake lilikuwa nilijua ya kwamba Bournemouth wanatumia nguvu sana wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani hivyo nikaamua kutumia wachezaji wengine.

Pamoja na Bournemouth kutumia nguvu lakini bado Mhkitaryan aliweza kucheza vizuri na kuwakimbiza.

Neno la mwisho

Huu ni mtazamo wangu nimejaribu kuweka baadhi ya data ili kudhibisha maoni yangu ya kwamba Henrikh Mhkitaryan alicheza vizuri katika mchezo dhidi ya Bournemouth na alikuwa ni mmoja ya wachezaji waliosaidia sana kupatikana kwa ushindi huo.

Kama wewe unaona tofauti ni sawa, unaweza kutumia nafasi hii kuonesha ya kwamba nimekosea, ukumbi ni wako tupia maoni yako hapo chini.

Speak Your Mind

*