Kombe la FA-Arsenal kuikaribisha Machester United

Ratiba ya raundi ya nne ya kombe la FA imetoka leo ambapo Arsenal itaikaribisha timu ya Mancheter United katika uwanja wa Emirates.

Kombe la FA-Arsenal kuikaribisha Machester United

Arsenal yenye mataji 13 na Manchester United yenye mataji 12 ya kombe la FA ndizo timu zenye mafanikio makubwa katika michuano hiyo.

Timu ya Mancester United ambayo inafundishwa na Ole Gunnar Solskjaer baada ya timu hiyo kumtimua Jose Mourinho itataka kushinda mchezo huo ili kupata kombe katika msimu huu.

Pia Arsenal ina kocha mpya Master Unai Emery ambaye ana sifa kubwa ya kushinda makombe ya mtoano pia atataka kushinda kombe la FA.

Kuwafunga Manchester United kwenye kombe la FA na kuwatupa nnje ya nne bora yatakuwa mafanikio tosha kwa Unai Emery msimu huu.

Ratiba kamili ya michuano hiyo

Swansea v Gillingham
AFC Wimbledon v West Ham
Shrewsbury or Stoke v Wolves
Millwall v Everton
Brighton v West Brom
Bristol City v Bolton
Accrington v Derby or Southampton
Doncaster v Oldham
Chelsea v Sheffield Wednesday or Luton
Newcastle or Blackburn v Watford
Middlesbrough v Newport
Manchester City v Burnley
Barnet v Brentford
Portsmouth v QPR
Arsenal v Manchester United
Crystal Palace v Tottenham

Michezo hiyo itachezwa kati ya Tarehe 25 na 28 ya mwezi huu.

Blackpool 0-3 Arsenal-Joe Willock ageuka shujaa

Blackpool 0-3 Arsenal-Joe Willock ageuka shujaa

Magoli mawili yaliyofungwa na mchezaji kinda wa Arsenal, Joe Willock yalisaidia kuizamisha Blackpool kwa goli 3-0 na kuiwezesha Arsenal kutinga raundi ya nne ya kombe la FA.

Arsennal waliuanza mchezo wa jana kwa kasi ambapo ndani ya dakika 10 za mwanzo mshambuliaji kinda wa Arsenal, Eddie Nketiah alikosa nafasi mbili za wazi.

Kutawala mchezo kwa Arsenal kulizaa matunda baada ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Aaron Ramsey, kuwababatiza mabeki wa Blackpool na mpira kugonga mwamba, wakati unarudi uwanjani ukakutana na Willock ambaye aliweza kufung kwa kichwa.

Joe Willock akishangilia goli la kwanza

Goli la pili la Arsenal lilifungwa tena na Joe Willock baada ya kumalizia mpira uliopigwa kutoka upande wa kulia na Carl Jenkinson, ambaye kabla ya kupiga krosi hiyo alicheza gonga safi na Alex Iwobi.

Blackpool walijitahidi na kucheza kwa bidii katika kipindi cha pili lakini juhudi zao hazikufanikiwa kuwapatia goli, Arsenal walifanikiwa kupata goli la tatu kupitia kwa Alex Iwobi aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa wa Blackpool kufuatia shuti la Aaron Ramsey.

Pamoja na kushinda mchezo huo, Arsenal ilipata pigo kubwa baada ya nahodha wake Laurent Koscienly kuumia wakati akipata misuli kujiandaa na mchezo huo.

Katika mchezo huo kocha wa Arsenal aliamua kuwapa nafasi vijana kama Joe Willock, Eddie Nketiah na Ainsley Maitland-Niles, ambao hawakumuangusha kwani walicheza vizuri huku wakionesha ufundi na juhudi kubwa.

Pia Saka na Medley ambao waliingia kipindi cha pili walijitahidi sana ingawa hawakupata muda mrefu wa kuonesha ufundi.

Baada ya ushindi huo Arsenal imerudi London na itaendelea kujiandaa na michezo ya ligi kuu ambapo itapambana na timu za London, West Ham na baadaye Chelsea.

#COYG

Arsenal yazinduka-Yaifunga Fulham 4-1

Baada ya kumaliza mwaka vibaya kwa kufungwa 5-1 na Liverpool, jana Arsenal ilizunduka na kuwafunga wanyonge Fulham kwa jumla ya magoli 4-1.

Arsenal yazinduka-Yaifunga Fulham 4-1

Arsenal waliuanza mchezo huo taratibu na kama washambuliaji wa Fulham wangekuwa makini wangeweza kufunga magoli mawili au matatu kabla ya dakika ya 20.

Arsenal ndiyo waliokuwa kupata goli baada ya kiungo Granit Xhaka kufunga goli katika dakika ya 25 kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Alex Iwobi.

Beki ya Arsenal iliendelea kukatika lakini hadi mapumziko Arsenal walifanikiwa kulinda goli lao na kuendelea kuongoza kwa goli hilo moja.

Kipindi ch pili kilianza kwa Arsenal kufanya mabadiliko ambapo Mustafi alitoka na kuingia Lucas Torreira, pia walifanya mabadiliko ya kimfumo kutoka kutumia 3-4-1-2 na kuanza kucheza 4-4-2 diamond.

Mabadiliko hayo yaliwasaidia Arsenal kwani katika dakika ya 55 walifanikiwa kufunga goli la pili kupitia kwa Alexandre Lacazette.

Wakati nikiamini ya kwamba Arsenal wameanza kucheza vizuri, Laurent Koscienly aliokoa vibaya mpira uliomkuta Torreira hajakaa sawa na kupokonywa mpira (alifanyiwa faulo na refa akapeta) na kusababisha Fulham kupata goli la kufutia machozi kupitia kwa Kamara, hii ilikuwa dakika ya 69.

Aaron Ramsey aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Lacazette, alifanikiwa kuipatia Arsenal goli la tatu katika dakika ya 79.

Pierre Emerick Aubamayang alifunga goli la nne na la mwisho kwa Arsenal katika dakika ya 83 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Sokratis.

auba akishangilia goli lake

Auba akishangilia goli lake

Kwa ushindi huo Arsenal inaendelea kubakia katika nafasi ya tano ikiwa imezidiwa pointi mbili na timu ya Chelsea iliyopo nafasi ya nne (Chelsea ina mchezo mmoja mkononi ambao itacheza leo).

Arsenal itacheza mchezo ujao dhidi ya Blackpool katika kombe la FA mchezo ambao utafanyika jumamosi ijayo.

#COYG

Arsenal yafungwa 5-1 na Liverpool

Timu ya Arsenal leo imepokea kipigo kikali cha goli 5-1 kutoka kwa Liverpool na kujiweka katika mazingira magumu ya kumaliza ndani ya timu nne bora.

Arsenal yafungwa 5-1 na Liverpool

Kipigo hicho ni kikubwa zaidi kupokea tangu kocha mkuu wa Arsenal achukue nafasi ya kuinoa timi hiyo mwezi wa sita mwaka huu.

Liverpool waliuanza mchezo huo kwa kasi kubwa lakini Arsenal ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli baada ya Ainsley Niles kufunga goli kufuatia krosi safi iliyopigwa na Alex Iwobi.

Dakika chache baadaye Liverpool walisawazisha kupitia kwa Roberto Firmino kufuatia mabeki wa Arsenal kujichanganya katika harakati za kuokoa mpira na kumpa Firmino nafasi ya kufunga.

Uzembe wa mabeki wa Arsenal ulisababisha Firmino aifungie Liverpool goli la pili sekunde 90 baada ya goli la kwanza.

Mané alifunga goli la tatu kwa Liverpool kufuatia krosi safi ya Mo Salah kabla ya Salah kufunga la nne kwa mkwaju wa penati baada ya Sokratis kumuangusha Salah ndani ya eneo la hatari.

Hadi mpira unaenda mapumziko timu hizo matokeo yalikuwa Liverpool 4-1 Arsenal.

Roberto Firmino alifanikiwa kufunga goli la tatu kwa mkwaju wa penati baada ya Kolasinac kumsukuma mchezaji wa Liverpool ndani ya eneo la hatari la Arsenal.

Emery alifanya mabadiliko katika kipindi cha pili lakini hayakuwa na tija kwani licha ya Arsenal kucheza vizuri kipindi cha pili walishindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga.

Kuna wakati unatakiwa ukubali ya kwamba wapinzani ni bora kuliko wewe, hicho ndicho kilichotokea leo, Liverpool walikuwa bora na wamestahili kushinda, haina haja ya kugombana ama kutupiana lawama, cha msingi wajipange kwani timu nyingine sio nzuri kama Liverpool na wanaweza kupata matokeo.

#COYG

Liverpool Vs Arsenal-Mesut Özil kukosekana kesho

Baada ya Arsenal kukwama na kutoa sare na timu ya Brigthon, kesho itakuwa na kibarua kigumu pale ambapo itacheza na viongozi ya ligi kuu ya Uingeleza, Liverpool katika uwanja wa Anfield.

Liverpool Vs Arsenal-Mesut Özil kukosekana kesho

Arsenal ambayo imekuwa na mwenendo wa kusuasua katika michezo ya hivi karibuni itakumbana na Liverpool ambayo inacheza kwa kiwango kikubwa na kufanikiwa kukaa kileleni mwa ligi kuu ya Uingeleza.

Kama hili halitoshi, usiku huu kuliibuka tetesi za kwamba kiungo mchezeshaji wa Arsenal, Mesut Özil angeanza kama mchezaji wa akiba na nusu saa baadaye BBC walitangaza ya kwamba mchezaji huyo alilalamika ya kwamba ana maumivu ya goti mara baada ya mazoezi ya mwisho leo na madaktari wa Arsenal walipomfanyia vipimo walidhibitisha ya kwamba ana maumivu na ameondolewa kwenye kikosi hicho.

Liverpool vs Arsenal

Tukirudi katika mchezo ni kwamba Liverpool wapo vizuri zaidi kuliko Arsenal, huo ni ukweli, Liverpool wana beki bora katika ligi kuu ya Uingeleza na pia wana moja ya safu bora za ushambuliaji (ingawa bado naamini Arsenal ina washambuliaji bora kuliko Liverpool).

Arsenal inaingia katika mchezo huu ikiwa imegubikwa na wimbi la majeruhi hasa upande wa safu ya ulinzi na pia kukosekana kwa Özil na Mkhitaryan kunapunguza uwezo wa Arsenal kutengeneza magoli.

Kikosi

Nategemea Bernd Leno kuanza golini,pia kukosekana kwa Özil na Mkhi kunaweza kumlazimisha Unai Emery kuchezesha mabeki watatu wa kati(Sokratis, Koscienly na Nacho Monreal) ili kumtumia Kolasinac kutengeneza nafasi kutokea winga wa kushoto.

Kwa upande wa viungo nadhani Xhaka, Torreira na Guendouzi kucheza huku Aaron Ramsey akianza kama mchezaji wa akiba, Pierre Emerick Aubamayang na Alexandre Lacazette kuanza kama washambuliaji wa kati.

Utabiri

Najua mashabiki wengi wa Arsenal wana wasiwasi na mchezo huu na wana sababu ya kuwa hivyo kwani kila mchambuzi wa soka anaamini ya kwamba Liverpool watashinda, ila mimi naamini ya kwamba Jurgen Klop bado hajapata mbinu za kumfunga Unai Emery hivyo kesho naamini Arsenal watamaliza ubabe wa jinana wa Klopp na kuwafunga pale pale kwao Anfield.

Utabiri wangu Liverpool 1- 2 Arsenal

Je wewe unatabiri vipi? tupia maoni yako hapa chini.

#COYG

Arsenal waingia mkataba na SKOL Rwanda

Arsenal imeingia mkataba na kampuni ya kutengeneza bia iitwayo,  SKOL Brewery Limited Rwanda katika mkataba utakaodumu kwa miaka miwili na nusu.Arsenal waingika mkataba na SKOL Rwanda

Katika taarifa iliyotolewa na timu, Arsenal imeingia mkataba na SKOL Rwanda, ikiwa ni jitihada zake za kuongeza nguvu zake katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Mkataba huo unafuatia na ule kati ya Arsenal na bodi ya utalii ya Rwanda, ambapo Arsenal imekuwa ikivaa nembo za Visit Rwanda tangu kuanza kwa msimu huu.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, afisa masoko wa Arsenal, Peter Silverstone, alisema ya kwamba Arsenal ina mashabiki zaidi ya milioni 90 katika nchi zilizo kusini mwa jangwa na Sahara na mkataba huo utasaidia taasisi zote mbili kuendelea kujitangaza katika ukanda huo.

SKOL Brewery Limited Rwanda wamekuwa wakihusika na kuendeleza soka katika nchi ya Rwanda kwani ndiyo wadhamini wakuu wa timu ya Rayon Sports.

Pia katika mkataba huo kuna kipengele ambacho kitaifanya Arsenal iwe inatoa ushauri wa kiufundi wa timu zote zinadhaminiwa na kampuni hiyo ya bia.

#COYG

Arsenal Vs Southampton-Nani kucheza kama beki wa kati?

Arsenal Vs Southampton-Nani kucheza kama beki wa kati?

Laurent Koscielny anaweza kuanza leo dhidi ya Southampton

Arsenal leo inaingia katika uwanja wa St Mary’s kupambana na Southampot katika mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza ikikubwa na tatizo la kukosa mabeki wa kati kutokana na majeruhi au kadi.

Kuingia katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, Arsenal itacheza na Southampton (ya 19), Burnley (ya 17) na Brighton (ya 13), kwa kawaida hizi ndizo mechi ambazo ungependa kocha awapumzisha baadhi ya wachezaji ili wale ambao hawachezi mara kwa mara wapate nafasi.

Tatizo kubwa lipo kwa upande wa mabeki wa kati, Rob Holding ameumia na atakosa mechi zote zilizobaki za msimu huu,Dinos Mavropanos bado hajapona na Skrodran Mustafi naye ameumia kifundo cha mguu, hat kama angekuwa mzima angekosa mchezo wa leo kutokana na kuwa na kadi tano za njano.

Sokratis pia anakosa mchezo wa leo kutokana na kuwa na kadi tano za njano, hivyo leo kocha Unai anamaamuzi magumu ya kufanya, amchezeshe Laurent Koscienly ambaye juzi alicheza dhidi ya Qarabaq au amchezeshe Medley ambaye kwa taarifa nilizonazo ni kwamba amesafiri na timu kuelekea Southampton.

Wachezaji wengine wanaoweza kucheza kama mabeki wa kati ni Nacho Monreal, Stephan Lichtsteiner, Mohamed Elneny,Carl Jekinson na Granit Xhaka. Ingawa naamini wawili wa mwanzo ndiyo wenye nafasi kubwa.

Upande wa kiungo hakuna tatizo kubwa kwani maestro Mesut Özil ameshapona na leo anaweza kucheza, Aaron Ramsey amepona, Xhaka na Torreira hawakucheza alhamisi hivyo wanaweza kucheza leo.

Kwa upande wa ushambuliaji, ukiondoa Danny Welbeck ambaye ni majeruhi wachezaji wengine wote wapo fiti, nimeambiwa ya kwamba makinda Eddie Nketiah na Bukayo Saka pia wamesafiri na timu na wanaweza kuwa sehemu ya wachezaji watakaoanzia katika benchi la wachezaji wa akiba.

Utabiri wa matokeo

Southampton wamekuwa wakicheza vibaya na wameshinda mechi moja tu, wanashika nafasi ya 19, wiki iliyopita walimtumua kocha wao Mark Hughes baada ya kutoa sare ya goli 2-2 na Machester United,sasa wana kocha mpya, Ralph Hasenhüttl ambaye ni raia wa Austraria.

Ralph Hasenhüttl ni mmoja ya makocha bora wanaochipukia katika ulimwengu wa soka. Hivyo ukichukulia mori mpya watakayokuwa nayo wachezaji, na pia ukweli wa kwamba Southampton huwa wanaisumbua sana Arsenal wakicheza kwao, huu utakuwa ni mchezo mgumu sana kwa Arsenal.

Pamoja na hayo yote naamini timu ya Arsenal ina kikosi bora na wana uwezo wa kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo, utabiri wangu ni Southampton 1- 3 Arsenal. Lacazette na Aubamayang kutupia.

Je wewe unatabiri nini? tupia maoni yako hapo chini.

Gurban Gurbanov-Arsenal sio timu ya kucheza Europa League

Kocha wa Qarabag, Gurban Gurbanov, amesema ya kwamba timu ya Arsenal haipaswi kucheza katika michuano ya kombe la Europa League.

Gurban Gurbanov-Arsenal sio timu ya kucheza Europa League

Gurban Gurbanov (Pichani juu)

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya timu yake na Arsenal, kocha huyo alisema ya kwamba kiwango cha wachezaji wa Arsenal ni kikubwa mno na hawastahili kucheza katika michuano hiyo.

Wanastahili kucheza katika ligi ya mabingwa wa ulaya, kocha huyo alisema.

“Nina imani ya kwamba Arsenal watafika fainali ya michuano hii,Ningependa kuwaona Arsenal wakicheza Baku katika fainali. ” kocha huyo aliwaambia waandishi wa habari.

Huu ni msimu wa pili wa Arsenal kushiriki katika michuano hii, msimu uliopita Arsenal ilifika nusu fainali na kutolewa na Atletico Madrid.

Mwaka huu ikiwa na mtaalamu wa Europa League, Unai Emery ni matarajio ya mashabiki wengi wa Arsenal ya kwamba timu hiyo itafika mbali zaidi na kulitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.

#COYG

 

Arsenal yaifunga Qarabag, yafikisha michezo 22 bila ya kufungwa

Timu ya Arsenal jana ilimaliza mechi za makundi za michuano ya Europa League kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya timu ya Qarabag.

Arsenal yaifunga Qarabag, yafikisha michezo 22 bila ya kufungwa

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery alikifanyia mabadiliko makubwa kikosi kilichoanza jana baada ya kuwaanzisha kwa mara ya kwanza Emi Martinez golini na  Laurent Koscienly kama beki wa kati.

Pia Unai aliwaanzisha wachezaji wengi vijana kama Bukayo Saka, Eddie Nketiah,na Joe Willock na kuwachanganya na wachezji wakongwe kama Mesut Özil na Alexandre Lacazette.

Mchanganyiko huo wa wachezaji vijana na wakongwe ulitosha kuifanya Arsenal iifunge Qarabag kwa goli moja lililofungwa na Alexandre Lacazette.

Arsenal ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo lakini makosa madogo madogo yaliifanya timu ishindwe kuibuka na ushindi mnono zaidi.

Lakini cha muhimi zaidi ni kwamba mashabiki 21,500 waliokuwepo uwanjani na mamilioni ya waliokuwa wanaangalia kwenye luninga walionekana kufurahishwa sana na vijana hao wa Arsenal waliokuwa wanacheza kwa juhudi kubwa.

Pia mchezo huo ulikuwa ni wa kwanza kwa nahodha wa Arsenal, Laurent Koscielny, ambaye alikuwa majeruhi tangu mwezi wa tano mwaka huu, baada ya kupumzishwa katika kipindi cha pili uwanja mzima ulisimama na kumpigia makofi huyu akionekana kutabasamu.

Baada ya mchezo huo Kocienly aliwashukuru mashabiki wa Arsenal kwa mapokezi waliyompa.

Arsenal inamaliza hatua ya makundi ikiongoza kundi lake kwa kufikisha pointi 16, ikishinda michezo mitano na kutoa sare mchezo mmoja.

Jumatatu ijayo ndiyo siku ambayo itapangwa ratiba ya hatua ya 32 bora na Arsenal inaweza ikacheza na moja ya timu zifuatazo.

• BATE.
• Celtic.
• Brugge.
• Fenerbahçe.
• Galatasaray.
• FC Krasnodar.
• Lazio.
• Malmo.
• Olympiakos.
• Rapid Vienna.
• Rennes.
• Shakhtar.
• Slavia Prague.
• Plzeň.
• Villarreal.
• Zurich.

Je ni timu gani ambayo ungependa tukutane nayo? toa maoni yako hapa chini.

 

Arsenal vs Qarabag-Nafasi nyingine ya vijana kuonesha uwezo

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery anatazamiwa kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha Arsenal kitakachocheza na timu ya Qarabaq kesho katika michuano ya kombe la Europa League.

Arsenal vs Qarabag-Nafasi nyingine ya vijana kuonesha uwezo

Arsenal tayari imeshajihakikishia uongozi wa kundi lake na kufuzu kwa 32 ya michuano ya kombe la Europa League na ukweli ni kwamba mchezo wa kesho hauna umuhimu wowote zaidi ya kuendeleza wimbi la ushindi na kuwapa nafasi wachezaji vijana na wale ambao walikuwa majeruhi nafasi ya kucheza.

Kocha Emery tayari ameshadhibitisha ya kwamba Laurent Koscienly ataanza katika mchezo huo, pia alisema ya kwamba Mesut Özil ambaye alikosa michezo mitano kwa maumivu ya mgongo naye yumo katika kikosi cha wachezaji 18 walioitwa kushiriki katika mchezo huo. Pia alisema ya kwamba atatumia baadhi ya wachezaji wanaocheza katika kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 23.

Taarifa ya wachezaji majeruhi.

Mesut Ozil anaweza kucheza mchezo wa kesho kutokana na kupona, Aaron Ramsey aliyekuwa na maumivu ya kifundo cha mguu pia amepona – ingawa Konstantinos Mavropanos , Rob Holding , Danny Welbeck  na Shkodran Mustafi watakosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.

Mesut Ozil  anaweza kucheza kesho dhidi ya Qarabag

Mesut Ozil anaweza kucheza kesho dhidi ya Qarabag

Kikosi

Kutokana na Arsenal kucheza michezo mitatu katika siku 10, ninategemea Unai Emery kubadilisha kikosi na kuwatumia wachezaji wengi wa akiba au vijana.

Mchanganyiko wa wachezaji wakongwe kama Petr Cech, Laurent Koscienly ,Mesut Özil na wachezaji vijana kama Emile Smith Rowe,Eddie Nketiah,Joe Willock Ainsely Niles na wengineo utakuwa ni muhimu katika kuiletea Arsenal ushindi hapo kesho.

Utabiri wa Matokeo

Pamoja na Arsenal kuchezesha kikosi cha pili, nategemea ya kwamba Arsenal itakuwa na kikosi ambacho kitaweza kuwashinda Qarabag, utabiri wangu ni kwamba Arsenal itashinda kwa goli 2-0, Eddie Nketiah akifunga moja ya magoli hayo.

#COYG

Arsenal 1-0 Huddersfield-Lucas Torreira aiokoa Arsenal

Mchezaji kiungo wa Arsenal Lucas Torreira, jana alifunga bao pekee na kuisezesha timu ya Arsenal kuibuka na ushinda wa goli 1-0 dhidi ya timu ya Huddersfield.

Arsenal 1-0 Huddersfield-Lucas Torreira aiokoa Arsenal

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kuchezesha viungo wakabaji watatu, mabeki watano wa washambuliaji wawili, hali iliyosababisha timu kucheza tofauti sana na mechi nyingine.

Kuchezesha kwa viungo wengi wakabaji kulifanya timu kutotengeneza nafasi za kupata magoli kwani hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza Arsenal ilifanikiwa kupiga shuti moja tu kulenga goli.

Pamoja na hali hiyo Arsenal wangeweza kupata magoli katika kipindi hicho, baada ya washambuliaji wake Pierre Emerick Aubamayang na Alexandre Lacazette kupoteza nafasi za wazi, pia Lacazette alifunga goli lililokataliwa na mwamuzi kwa madai ya kwamba alikuwa ameotea lakini marudio kwenye luninga yalionesha ya kwamba lilikuwa ni goli kwani beki wa Huddersfield aliugusa mpira na kuvunja mtego wa kuotea.

Wakiiga mbinu chafu za Mourinho, Huddersfield walianza mchezo huo kwa kucheza rafu za makusudi dhidi ya wachezaji wa Arsenal huku mwamuzi wa jana akishindwa kuwapa kadi au kuwaonya.

Kipindi cha pili mwalimu Unai Emery aliamuakuwaingiza Alex Iwobi na Henrikh Mkhitaryan, ingawa kwa mtazamo wangu wachezaji hao hawakubadilisha sana hali ya mchezo.

Zikiwa zimebaki dakika 7 mpira kumalizika na nikianza kuamini ya kwamba mpira huo ungemalizika kwa sare alikuwa ni kiungo mfupi kutoka Uruguay, Lucas Torreira aliyefunga moja ya magoli bora kabisa akimalizia pasi aliyopewa na Aubamayang ndani ya eneo la hatari la Huddersfield.

hadi mwisho wa mchezo Arsenal 1-0 Huddersfield.

pamoja na ushindi huo Arsenal inaendelea kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na alama 34 nyuma ya Chelsea yenye alama 34 lakini ikiwa na wastani mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa.

Arsenal itaingia tena uwanjani Alhamisi ya wiki hii kucheza na timu ya Qarabag katika mchezo wa kukamilisha ratiba wa kombe la Europa League.