Wachezaji wa Arsenal waanza mazoezi-Madogo wanne waitwa

Wachezaji wa Arsenal waanza mazoezi-Madogo wanne waitwa

Wachezaji wa Arsenal wakiwa mazoezini

Baada ya kumalizika kwa mechi za kimataifa wachezaji wa Arsenal leo jumatano walianza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Bournemouth utakaofanyika jumapili.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika katika viwanja vya London Colney wachezaji wanne wa timu ya vijana walionekana wakifanya mazoezi na timu ya wakubwa na pia kuna baadhi ya wachezaji muhimu walikosekana.

Madogo wanne waitwa

Jordi Osei-Tutu,mwenye umri wa miaka 20 anayecheza kama beki alifanya vizuri katika mechi za maandalizi ya ligi kuu lakini alipata majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda kwa sasa amepona na anafanya mazoezi na timu ya wakubwa.

Makinda wengine ambao walionekana kwenye mazoezi hayo ni Charlie Gilmour ambaye anafanya vizuri akiwa na timu ya vijana wenye umri wa miaka 23 na beki wa kati Zech Medley ambaye alikuwa kama mchezaji wa akiba katika mchezo dhidi ya Leicester.

Mchezaji wa nne aliyeonakana mazoezini leo ni beki wa kushoto Dominic Thompson.

Nacho Monreal akosekana

Nacho Monreal na Lichsteiner hawakuonekana katika mazoezi hayo, wachezaji hao walikuwa ni majeruhi na haijulikani ni lini watarudi uwanjani, labda kesho kwenye mkutano na waandishi wa habari, Unai Emery anaweza kuelezea kwa undani.

Lacazette afanya mazoezi

Habari njema ni kwamba wachezaji wa Arsenal,  Alexandre Lacazette, Pierre-Emerick Aubameyang na Laurent Koscielny wote walifanya mazoezi kama kawaida.

Kulikuwa na tetesi za kwamba Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang wangeweza kukosa mchezo huo kutokana na kupatwa na majeraha, lakini kwa sasa inaonekana ya kwamba wamepona.

Laurent Koscielny yeye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu na sasa ameanza mazoezi ingawa bado haijulikani ni lini ataanza kucheza mechi za ushindani

Sven Mislintat na Huss Fahmy wapandishwa vyeo Arsenal

Sven Mislintat na Huss Fahmy wapandishwa vyeo Arsenal

Sven Mislintat

Gazeti la Independent limeandika ya kwamba watendaji wawili wa Arsenal, Sven Mislintat na Huss Fahmy wamepandishwa vyeo na timu ya Arsenal.

Sven Mislintat, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa idara ya usajili tangu ajiunge na Arsenal akitokea Dortmund ya Ujerumani, kwa sasa atakuwa mkurugenzi wa ufundi, wakati Huss Fahmy, ambaye kazi yake ilikuwa ni kufanya mazungumzo ya mikataba, kwa sasa atachukua nafasi iliyoachwa wazi na Raul Sanllehi, kama mkuu wa mambo yote yanayohusiana na soka katika timu ya Arsenal.

Kupandishwa vyeo kwa Mislintat na Fahmy kunatokana na kazi kubwa waliyoifanya katika miezi 12 iliyopita, Mislintat ndiye aliyefanikisha usajili wa wachezaji wote wapya wa Arsenal tangu mwezi wa kwanza mwaka huu. Usajili wa wachezaji kama Pierre-Emerick Aubameyang, Henrikh Mkhitaryan, Sokratis, Lucas Torreira, Matteo Guendouzi na Bernd Leno ni kazi yake.

Fahm ndiye aliyehusika na kujadili mikataba ya wachezaji waliotajwa hapo juu,pia anahusika na kujadili mitakaba mipya ya wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Arsenal.

Uteuzi huo ni muendelezo ya mabadiliko ambayo yanaendelea kutokea ndani ya uongozi wa ngazi za juu wa Arsenal, baada ya aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Arsenal Ivan Gazidis, kuachia ngazi na kujiunga na timu ya AC Milan ya Italia.

Je unaonaje mabadiliko hayo? tupia maoni yako hapa chini.

ARSENAL 0-0 SPORTING-ARSENAL YAFUZU HUKU WELBECK AKIUMIA

Arsenal jana ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya Sporting Lisbon na kufanikiwa kuingia katika hatua ya mtoano ya kombe la Europa League.

ARSENAL 0-0 SPORTING-ARSENAL YAFUZU HUKU WELBECK AKIUMIA

Kutokana na sare hiyo na pia  Vorskla kufungwa na Qarabag, Arsenal imefanikiwa kuingia katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo ingawa bado haijakikishia kuongoza kundi kitu ambacho kocha wa Arsenal, Unai Emery alisema ndilo lengo kuu ya Arsenal kwa sasa.

Katika mchezo huo Arsenal ilicheza vizuri kiasi lakini ilishindwa kufanya mashambulizi ya maana na hivyo kushindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga.

Dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza mchezaji wa Arsenal Danny Welbeck aliumia wakati alipojaribu kupiga mpira wa kichwa na kugongana na mlinzi wa Sporting Lisbon.

Ilikuwa ni rahisi kugundua ya kwamba mambo yalikuwa mabaya kwani alianguka huku akionesha maumivu makubwa na pia sura za wachezaji wa Arsenal zilionesha hali ya hudhuni sana.

Baada ya kutibiwa na kupewa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua Welbeck alitolewa nje ya uwanja na kukimbizwa Hospitali.

Akiongea baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Arsenak, Unai Emery alisema hali ya mchezaji huyo bado ilikuwa mbaya na bado aikuwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Wasiwasi mkubwa ulitanda kati ya mashabiki wa Arsenal huku wengi wao wakiamini ya kwamba majeraha aliyoyapata mchezaji huyo yanaweza kumfanya tusimuone uwanjani tena akiwa na jezi ya Arsenal.

Ikumbukwe ya kwamba Welbeck yupo katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na anaweza kuondoka bure katika msimu wa usajili wa majira ya joto.

Sisi kama mashabiki wa Arsenal tungependa kumuombea Danny Welbeck apone haraka ili tumuone tena akivaa jezi za Arsenal uwanjani.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Arsenal ilicheza soka la kiwango kikubwa katika mchezo ambao uliishia kwa sare ya goli 1-1 dhidi ya Liverpool.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Goli la kusawazisha kutoka kwa mshambuliaji wa Arsenal, Alexandre Lacazette lilimaanisha ya kwamba Arsenal wangeondoka na pointi moja katika mchezo huo uliokuwa mkali na na kusisimua.

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kucheza vizuri lakini Liverpool ndio waliopata nafasi nzuri zaidi za kufunga, kwani walicheza kwa kujihami na kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Kama nilivyosema asubuhi, sehemu ya kiungo ndiyo sehemu ambayo ingeamua matokeo na Lucas Torreira alimpoteza kabisa Fabinho na kutawala eneo la katikati ya uwanja.

Kipindi cha kwanza Liverpool waligongesha miamba mara mbili kupitia kwa wachezaji  Roberto Firmino na Virgil van Dijk.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Arsenal walikianza kipindi cha pili kwa nguvu lakini walikuwa ni Liverpool waliopata goli la kuongoza baada ya golikipa wa arsenal Bernd Leno kufanya makosa ambapo aliutema vibaya mpira na kumkuta James Milner ambaye aliipatia Liverpool goli la kuongoza.

Mabadiliko yaliyofanya na kocha wa Arsenal Unai Emery, ya kumtoka Henrik Mkhitryan na kumuingiza Alex Iwobi yaliisaidia sana Arsenal kwani ilianza kufanya mashambulizi ya hatari zaidi kiasi cha Liverpool kupaki basi.

Alikuwa ni mshambuliaji wa Arsenal,Alexandre Lacazette aliyeipatia Arsenal goli la kusawazisha katika dakika ya 82 baada ya kuwazunguka mabeki wa Liverpool na kupiga shuti kifundi ambalo kipa wa Liverpool,Allison hakuweza kuliona.

Hadi mwisho wa mchezo Arsenal 1-1 Liverpool.

Baada ya kuisha kwa mchezo huo nilifanikiwa kuongea na baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambapo wengi wao walionekana kuridhika na hali ya kujituma kulikooneshwa na timu yao na pia wengi wanaamini ya kwamba Arsenal ilishahili kushinda mchezo huo.

Kwangu mimi Granit Xhaka ndiye aliyekuwa mchezaji nyota katika mchezo wa leo kwani yeye na Lucas Torreira walidhibiti sehemu ya kiungo, Xhaka alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote, aliondoa mipira mingi ya hatari na pia alimsaidia sana Sead Kolasinac upande wa kushoto.

Baada ya mchezo wa leo, Arsenal itaingia dimbani tena Alhamisi ijayo kupambana na timu ya Sporting Lisbon katika michuano ya kugombea kombe la Europa League.

Pia sare ya leo inamaanisha Arsenal imecheza michezo 14 bila ya kufungwa, ikishinda 12 na kutoka sare katika michezo miwili.

Kwa wale ambao hawakuona mchezo huo hapo chini kuna video inayoonesha vipande muhimu vya mchezo huo na magoli yote mawili.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Arsenal leo itakuwa na kibarua kigumu wakati watakapowakaribisha vijana wa Jurgen Klop, Liverpool katika uwanja wa Emirates.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Pamoja na Arsenal kucheza michezo 13 bila ya kufugwa (imeshinda 12 na kutoka sare 1) bado wachambuji wengi wa soka hawaipi nafasi ya kushinda katika mchezo wa leo. Ukweli ni kwamba  kuna baadhi mashabiki wa Arsenal wanaoamini ya kwamba Arsenal itapoteza mchezo huu.

Ni kweli kwamba Liverpool chini ya Klop wameimalika sana hasa baada ya kumsajili beki kisiki kutoka Southampton Virgil Van Dijk na golikipa Allison. Wakati Arsenal ndio kwanza wana miezi mitatu tangu waanze kujipanga.

Nimekuwa nikiwaangalia Liverpool katika mechi zao nyingi msimu huu, nikiwa mkweli sio timu ya kutisha sana kama wachambuzi wengi wanavyotaka tuamini, kuna mechi dhidi ya Leicester na Huddlefield walishinda kibahati, pia safu yao ya ushambuliaji sio kali kama mwaka jana, ingawa safu yao ya ulinzi imeimarika sana.

Rekodi

Unai Emery amewahi kuifunga Liverpool ya Klop kwenye fainali ya kombe la Europa League baada ya kumzidi ujanja Klop katika kipindi cha pili, Ingawa Arsenal haijawahi kuifunga Liverpool tangu ianze kufundishwa na Klop.

Liverpool imeshinda mara mbili tu katika michezo kumi na nane iliyofanyika Emirates na Arsenal haijaifunga Liverpool katika michezo 6 ya mwisho.

Vikosi

Wao wana Allison ambaye si kipa mbaya lakini anafaungika,ikumbukwe ya kwamba ni kipa ambaye amecheza michezo 100 tu ndani ya miaka mitano iliyopita na kati ya hiyo 50 ilikuwa ni mwaka jana, pia ikumbukwe ya kwanza alikuwa anawekwa benchi na Wojciech Szczęsny.Kwenye suala la makipa naamini ngoma droo.

Linapokuja kwenye mabeki hapo ndipo vijana hao wa Klop wanapoishida Arsenal, kusajiliwa kwa Van Dijk na Allison kumewaimalisha sana, siku hizi hawafungwi magoli ya kijinga kama zamani,Arsenal ina majeruhi wengi upande wa mabeki, sina taarifa kama Kolasinac, Monreal,Sokratis na Bellerin wamepita vipimo vya afya, kama hawajapita inaweza ikawa jioni mbaya sana kwa sisi mashabiki wa Arsenal.

Kwenye kiungo naamini Torreira, Xhaka na Ôzil ni bora kuliko kiungo chote cha Liverpool kama huamini subiri baadaye uone, ila kutokana na beki kuwa mbovu itabidi viungo wa Arsenal wacheze kwa juhudi kubwa kama Arsenal inataka kushinda mchezo wa leo.

Linapokuja kwenye ushambuliaji naamini hakuna tofauti kubwa sana wao wana Manè , Bob Firminho na Moh Salah na sisi tuna Auba,Lacazette na Iwobi.

Utabiri

Ni mchezo mgumu sana kutabiri, lakini naamini katika uwezo wa kikosi cha Arsenal na pia nina imani na kocha Unai, kama nilivyosema tuna kiungo bora kuliko Liverpool na hapo ndipo tunapoweza kuwafungia, ingawa sina imani na safu ya ulinzi kama inaweza kuwazuia Moh Salah na wenzie.

Naani mchezo wa leo utakuwa na magoli mengi na Arsenal itashinda na kuwafunga midomo wapinzani wote waliokuwa wanadai tunazifunga timu dhaifu, naamini Arsenal atashinda kwa goli 3-2.

Je wewe una maoni gani? tupia maoni yako na utabiri hapo chini.

 

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Mchezaji na nahodha wa zamani wa Arsenal,  Per Mertesacker amepandishwa cheo na sasa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Arsenal.

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Katika mahojiano na gazeti la Telegraph,Mkuu wa kitengo cha soka katika timu ya Arsenal,Raul Sanllehi alisema ya kwamba Per Mertesacker amejiunga na timu ya wakurugenzi wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa  Raul Sanllehi uteuzi wa Matersacker ni sehemu ya jitihada za uongozi wa Arsenal kuongeza watu wa soka katika ngazi za juu za uongozi wa Arsenal.

Mertesacker anakuwa mtu wa nne ambaye anajua soka kujiunga na timu ya wakurugenzi 15 ambao kwa sasa ndio wanaofanya maamuzi yote yanayoihusu Arsenal kwa sasa.

Kiongozi mwandamini wa Arsenal,Vinai Venkatesham anasema ya kwamba Per anajiunga na Huss Fahmy, Sven Mislintat,na Raul Sanllehi kama vichwa vya soka katika uongozi huo.

Sanllehi hakuweza wazi kama Mertesacker ataendelea na majukumu yake kama mkuu wa kituo cha soka cha Arsenal cha Hale End, lakini tunaamini ya kwamba ataendelea na majukumu yake kama kawaida kwani wakurugenzi wote wa Arsenal wana majukumu tofauti ndani ya Arsenal na sioni sababu kwa nini iwe tofauti kwa Mertesacker.

Kuongezwa kwa Per mwenye uzoefu mkubwa kama mchezaji kwani ameichezea Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani michezo mingi na pia amewahi kushinda kombe la dunia ni jambo zuri kwa timu kwani miaka miaka ya karibuni timu imekuwa ikufanya maamuzi ya ajabu hasa linapokuja suala la mikataba ya wachezaji.

Je unasemaje kuhusu uteuzi huo? tupia maoni yako hapa chini.

Kombe la Carabao: Arsenal kucheza na Totenham robo fainali

Baada ya kutinga robo fainali ya kombe la Carabao, Arsenal imepangiwa kucheza na mahasimu wao wakubwa Totenham Hotspurs.

Kombe la Carabao: Arsenal kucheza na Totenham robo fainali

Katika mchezo huo uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Emirates mwishoni mwa mwezi utakuwa ni kipimo tosha kwa vijana wa Unai Emery kwani kwa miaka mitatu sasa Totenham wamekuwa wakicheza vizuri.

Ikumbukwe ya kwamba Arsenal ilitinga fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na kufungwa na timu ya Manchester City.

Ratiba kamili ya michuano hiyo

Arsenal v Tottenham

Leicester/Southampton v Manchester City

Middlesbrough v Burton

Chelsea v Bournemouth

Mchezo kati ya Leicester na Southampton uliahirishwa baada ya kutokea ajali ya Helikopta katika uwanja wa King Power na kuua watu watano akiwemo mmiliki wa timu hiyo.

Arsenal yatinga robo fainali ya kombe la Carabao

Timu ya Arsenal imefanikiwa kuifunga timu ya Blackpool kwa jumla ya magoli 2-1 na kufanikiwa kuingia robo fainali ya kombe la Carabao.

Arsenal yatinga robo fainali ya kombe la Carabao

Baada ya kulazimishwa sare na Crystal Palace,Arsenal wamezinduka na kufanikiwa kuifunga timu ya ligi daraja la kwanza ya Blackpool kwa goli 2-1 katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Emirates.

Arsenal ilianza mchezo huo taratibu lakini ilifanikiwa kujipatia goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza baada ya kiungo Matteo Guendouzi kupiga bonge la pasi lililomaliziwa na beki wa kulia  Stephan Lichtsteiner.

Hadi mapumziko Arsenal ilikuwa bado inaongoza kwa goli hilo moja.

Kipindi cha pili Arsenal ilicheza kwa kujiamini zaidi na alikuwa ni kinda Emile Smith Rowe aliyeipatia Arsenal goli la pili baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Cark Jenkinson, ukagonga  mwamba na kurudi uwanjani.

Wakati Arsenal wakiendelea kutawala mchezo huo, kiungo Matteo Guendouzi alipewa kandi nyekundu yenye utata baada ya kupewa kadi mbili za njano kwenye mazingira ya kutatanisha.

Dakika 10 baada ya Guendouzi kutoka, Blackpool walipata goli lao la kwanza baada ya mchezaji O’Connor kuifungia timu hiyo baada ya kumalizia kwa kichwa kona iliyopigwa na Jordan Thompson.

Baadaye kidogo Blackpool walikaribia kupata goli la pili baada ya golikipa wa Arsenal, Petr Cech kujaribu kumpiga chenga Jay Spearing, lakini mchezaji huyo alifanikiwa kumpoka Cech mpira huo na kumpasia Nathan Delfouneso ambaye alifunga lakini goli hilo lilikataliwa na mwamuzi kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ameotea.

Matumaini ya Blackpool ya kusawazisha katika mchezo huo yalipotea baada ya mchezaji   O’Connor kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Arsenal,Pierre-Emerick Aubameyang.

Baada ya ushindi huo Arsenal itacheza na Totenham katika robo fainali ya michuano hiyo.

Mechi ijayo ni dhidi ya Liverpool jumamosi ijayo.

#COYG.

Kama unataka kuangalia tena magoli au hukuyaona cheki hapo chini.

 

Arsenal vs. Blackpool: Watoto wapewe nafasi

Arsenal leo wanacheza na timu ya Blackpool katika raundi ya nne ya kombe la Carabao na ufuatao ni mtazamo wangu kuelekea mchezo huo.

Arsenal vs. Blackpool: Watoto wapewe nafasi

Arsenal inacheza na Liverpool katika mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza jumamosi hii, lakini kabla ya mchezo huo leo itacheza na timu ya Daraja la kwanza Blackpool katika kugombea kombe la Carabao.

Bila kuwadharau Blackpool, mchezo dhidi ya Liverpool ni wa muhimu zaidi kama Arsenal inataka icheze katika ligi ya mabingwa msimu ujao. Pia kufungwa na Liverpool kutapunguza sana hali ya kujiamini kwa wachezaji na mashabiki pia wanaoichukia Arsenal watapata la kuongea na kusema si mnaona tulisema wanazifunga timu ndogo tu.

Hivyo ni muhimu mno kwa kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery akawapa nafasi makinda kutoka timu ya vijana na kupumzisha wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.

Nikiwa mkweli ni kwamba Arsenal imekuwa ikichezesha kikosi cha kwanza katika mechi zote msimu huu na timu ikiwa imecheza mechi tatu za Europa League na moja ya kombe la karabao kuna wachezaji kama Eddie Nketiah na Willock hawajacheza hata dakika moja na timu ya wakubwa.

Katika mazoezi ya jana niliwaona wachezaji vijana wanne tu ambao ni Emile Smith Rowe, Joe Willock, Julio Pleguezuelo na Eddie Nketiah.Lingekuwa ni jambo jema kama wote wanne wangeanza huku nafasi zilizobaki zikijazwa na wachezaji wenye uzoefu.

Kikosi ambapo ningependa kianze leo ni kama ifuatavyo:

Cech, Maitland-Niles, Holding, Julio Pleguezuelo, Jenkinson, Ramsey, Guendouzi, Welbeck, Nketiah, Willock, Smith Rowe.

Lakini naami ya kwamba Unai Emery atapanga kama ifuatavyo:

Cech, Maitland-Niles, Holding, Mustafi, Jenkinson, Ramsey, Guendouzi, Aubameyang, Mkhitaryan, Welbeck, Smith Rowe.

Bila kujali nani anaanza naamini Arsenal itapata ushindi kesho na kufuzu katika hatua ya raundi ya tano ya kombe hili.

#COYG

Kombe La Carabao-Petr Cech kuanza

Arsenal leo itacheza na timu ya Blackpool katika raundi ya nne ya kuwania kombe la Carabo, na katika kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery amedhibitisha ya kwamba golikipa Petr Cech ataanza katika mchezo huo.

Kombe La Carabao-Petr Cech kuanza

Cech ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa mwezi muda baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Watford mwezi uliopita ambapo nafasi yake ilichukuliwa na kipa Bernd Leno ambaye alifanya vizuri katika michezo yote aliyocheza.

Lakini Unai Emery ameamua kumpumzisha Leno wakati Arsenal itakapoikaribisha timu hiyo ya ligi daraja la kwanza la Uingeleza.

Akiongea na kituo cha luninga cha Sky Sports Emery alisema.

“katika kila mchezo tutawapa nafasi makipa wetu nafasi ya kutusaidia ili kupata ushindi, tunaangali hali ya kujiamini kutoka katika kila golikipa tuliyenaye.”

“Lakini kwa sasa,Petr Cech ataanza katika mchezo dhidi ya Blackpool, baada ya kupona majeraha aliyokuwa nayo”
Alimalizia kocha huyo wa Arsenal.

 

Crystal Palace yaisimamisha Arsenal

Wimbi la ushindi la Arsenal jana lilifika ukingoni baada ya kulazimishwa sare ya magoli 2-2 na timu ya Crystal Palace katika mechi ya ligi kuu ya Uingeleza.

Crystal Palace yaisimamisha  Arsenal

Palace ndiyo waliokuwa wa kwanza kujipatia goli kupitia kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya beki wa Arsenal Skondrani Mustafi kumuangusha mchezaji wa Palace na muamuzi kuamua kuwa ni penati, na nahodha ya Palace, Luka Milivojevic alimpoteza Bernd Leno na kufunga.

Hadi mapumziko Crystal Palace 1-0 Arsenal.

Arsenal ilianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ambapo,Stephan Lichtsteiner aliingia kuchukua nafasi ya Hector Bellerin aliyeumia.

Arsenal walifanikiwa kupata goli la kusawazisha  baada ya Granit Xhaka kufunga kwa mpira wa adhabu ndogo nje kidogo la  eneo la 18.

Dakika mbili baadaye Pierre Emerick Aubamayang aliifungia Arsenal goli la pili na la kuongoza baada ya kumlizia mpira wa krosi kutoka upande wa kushoto na kuibua furaha kubwa kutoka mashabiki wa Arsenal.

Baada ya kuingia kwa goli hilo, Crystal Palace waliamka na kuanza kushambulia kwa nguvu na katika jitihada ya kocha Unai Emery za kulinda ushindi huo aliwatoa Aubamayang na Ôzil na nafasi zao kuchukuliwa na Danny Welbeck na Aaron Ramsey.

Mabadiliko hayo hayakuisaidia Arsenal kwani iliendelea kushambuliwa mara kwa mara,na wakatimchezo huo ukielekea dakika za mwishoni,Alexandre Lacazette alijaribu pasi ya mbali na kumkosa Lucas Torreira hali iliyofanya Crystal Palace waanzishe shambulizi la haraka hali iliyomfanya Granit Xhaka ajikute akiwa ana kwa ana na Wilfred Zaha ndani ya enero la penati la Arsenal na katika jaribuo la kumkaba mchezaji huo akatumia mwanya huo na kuanguka na mwamuzi akaamua iwe penati.

Luka Milivojevic alifanikiwa kufunga penati hiyo licha ya jitihada za Leno kuufuata mpira huo.

Hadi mwisho wa mchezo huo Crystal Palace 2-2 Arsenal.

Arsenal itacheza na Blackpool jumatano ijayo katika mchezo wa kugombea kombe la Carabao na mwisho wa wiki itacheza na Liverpool katika ligi kuu ya Uingeleza.