Mike Dean ateuliwa kuamua mchezo kati ya Arsenal na Spurs

Mwamuzi mtata, Mike Dean amteuliwa kuamua mchezo wa ligi kuu ya Uingeleza kati ya Arsenal na Totenham Hotspurs jumapili ijayo.

Uteuzi huo uliotangazwa leo na chama cha soka cha Uingelea FA umepokelewa vibaya na mashabiki wengi wa Arsenal, sababu kubwa ya mashabiki wa Arsenal kutomtaka Mike Dean ni kwamba mwamuzi huyo ni shabiki wa kutupwa wa Totenham.

Kuna video nyingi zinazoonesha kwa nyakati tofauti mwamuzi huyo akishangilia magoli ya Totenham kama anavyoonekana hapo chini kwenye video akishangilia goli la timu hiyo dhidi ya Aston Villa.

Hii sio mara ya kwanza kwa mashabiki kumkataa mwamuzi huyo ambaye alizaliwa na kukulia katika jiji la Manchester na kwani pia rekodi zake zinaonesha ya kwamba huwa anazipendelea sana timu kutoka katika jiji hilo hasa linapokuja suala la kutoa penati.

Hizi ni penati anazotoa Mike Dean kwa timu kubwa.
Man Utd – 16 katika michezo 61.
Chelsea – 12 katika michezo 65 .
Man City – 11 katika michezo 63.
Spurs – 10 katika michezo 58.
Arsenal – 3 katika michezo 64 .

Sio kwamba tunatafuta sababu ya kufungwa kabla ya mchezo, ukweli ni kwamba refa huyu haipendi Arsenal, pamoja na hayo tutawafunga Spurs jumapili ijayo.

Sol Campbell aanza kazi kama kocha wa Macclesfield Town

Mchezaji mkongwe wa Arsenal, Sol Campbell amepata kazi yake ya kwanza kama kocha baada ya kuteuliwa kuinoa timu ya Macclesfield Town iliyopo ligi daraja la pili la Uingeleza.

Sol Campbell aanza kazi kama kocha wa Macclesfield Town

Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Arsenal na Uingeleza amechukua mikoba katika timu hiyo inayotumia uwanja wa Moss Rose, timu hiyo ilitangaza leo jumanne.

Hii itakuwa kazi ya kwanza ya Campbell tangu astaafu kucheza soka mwaka 2011.

Sol Campbell mwenye umri wa miaka 44 anachukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mark Yates, ambaye alitimuliwa mwezi uliopita baada ya kuiongoza timu hiyo kucheza michezo 12 bila ya kushinda.

Hiyo siyo kazi rahisi kwa Cambpell kwani timu hiyo inashika nafasi ya 92 kati ya timu 92 zinazounda ligi zote nne za Uingeleza (ligi kuu, Champioship,Ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili).

Kila la heri Sol Campbell.

Bournemouth 1-2 Arsenal-Arsenal yaanza kushinda tena

Baada ya kutoka sare katika michezo mitatu ya ligi kuu, Arsenal imeanza kushinda tena baada leo mchana kuifunga timu ya Bournemouth kwa jumla ya goli 2-1.

Bournemouth 1-2 Arsenal-Arsenal yaanza kushinda tena

Arsenal iliingia uwanjani na mfumo tofauti na uliozoeleka wa 4-2-3-1 na kucheza 3-4-3 huku Mesut Özil na Aaron Ramsey wakikaa benchi na Lacazette akikosa kabisa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.

Kama kawaida Arsenal walianza mchezo huo kwa kasi ndogo hali iliyowafanya Bournemouth wautawale mchezo huo katika dakika 30 za mwanzo.

Pamoja na Arsenal kutokucheza vizuri sana lakini ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli, baada ya beki wa Bournemouth,Jefferson Lerma kujifunga katika harakati za kuokoa, kwa mtazamo wangu hilo ni goli bora zaidi la kujifunga nililowahi kuliona,bonge la goli.

Baada ya goli hilo, Arsenal walianza kucheza vizuri lakini kabla refa hajapuliza kipenga cha kumaliza kipindi cha kwanza Alex Iwobi alipoteza mpira ndani ya eneo la hatari la Bournemouth na timu hiyo kufanya shambulizi la kustukiza na kuwakuta wachezaji wa Arsenal wakiwa hawajajipanga na kuifanya timu hiyo kufunga goli la kusawazisha.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana goli 1-1.

Kipindi cha pili Arsenal ilianza kwa kasi na Bournemouth walirudi nyuma hatua moja hali iliyosaidia Arsenal kupata goli la pili na la ushindi lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Gabon, Pierre Emerick Aubamayang.

Pamoja na timu zote kufanya mabadiliko matokeo ya mchezo huo hayakubadilika hivyo hadi mwisho Bournemouth 1-2 Arsenal.

Baada ya ushindi huo Arsenal imefikisha michezo 17 bila ya kupoteza na Alhamisi itaelekea nchini Ukraine kucheza na timu ya Voskla katika raundi ya tano ya kombe la Europa League.

Kwa sasa Arsenal inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kuu ya Uingeleza, ikiwa na pointi moja nyuma ya Chelsea waliopoa nafasi ya nne na pointi tatu dhidi ya Totenham waliopoa nafasi ya tatu.

Mchezo ujao wa ligi utakuwa jumapili ijayo ambapo Arsenal itawakaribisha wapinzani wao wa jadi Totenham katika uwanja wa Emirates.

Hapo chini nimekuwekea video yenye magoli yote na matukio muhimu ya mchezo huo, uwe na jumapili njema mdau.

Robert Pires-Arsenal wanaweza kuwa mabingwa msimu huu

Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Robert Pires anaamini ya kwamba vijana wa Unai Emery wapo katika mbio za ubingwa msimu huu na anaamini itawashangaza watu wengi.

Robert Pires-Arsenal wanaweza kuwa mabingwa msimu huu

Arsenal haijabeba taji la ligi kuu tangu mwaka 2004, kwa sasa wanacheza vizuri wakiwa wamecheza michezo 16 bila ya kufungwa katika mashindano yote.

Kabla ya mchezo wa kesho dhidi ya Bournemouth, Arsenal wapo na pointi 24 baada ya mechi 12, wakiwa pointi 11 nyuma ya vinara Manchester City na mechi moja mkononi.

“Hii timu na kikosi hiki wanauwezo wa kupambana na  Man City, Liverpool, Chelsea na Manchester United kwa sababu wana wachezaji wenye uwezo mkubwa na kocha mzuri ,” Pires alikiambia kituo cha luninga cha ESPN.

“Unai Emery anafanya vizui, hatujafunga katika miezi miwili na tunafurahia matokeo mazuri,” aliongezea. “Wachezaji wamepata aina mpya ya soka na wanaonekana wanajiamini.”Wana uwezo wa kugombea taji laubingwa na kulichukua.”

Pia katika mahojiano hayo Robert Pires aliongelea umuhimu wa Arsenal kuchagua kocha bora baada ya Arsene Wenger kuondoka na anaamini bodi ya Arsenal ilipatia kumchagua Unai Emery kwani anaamini ni kocha bora na mtu sahihi kuiongoza Arsenal kurudisha makali yake ya zamani.

Pires alikuwa ni mmoja ya wachezaji walioweka historia ya kumaliza msimu bila kufunga baada ya kucheza mechi 49 bila ya kupoteza na kutwaa taji hilo mwaka 2004.

Tangu hapo Arsenal haijawahi tena kutwaa taji hilo, Je Emery ataikata kiu ya mashabiki wa Arsenal na kutwaa taji hilo? muda ndiyo utakaotoa jibu.

Je unayaonaje mawazo ya mkongwe Robert Pires ? unaamini Arsenal inaweza ikamaliza juu ya Liverpool na Manchester City? tupia maoni yako hapa chini.

Mambo matano ambayo mashabiki wa Arsenal wanapaswa kushukuru

Kila alhamisi ya nne ya mwezi wa 11 ,baadhi ya nchi zikiwemo Marekani, Canada na nyinginezo husherehekea simu maalum ya kutoa shukrani. Wenyewe wanaiita Thankgiving.

Katikaa kuunga mkono siku hii tumeamua leo kukuletea mambo matano ambayo mashabiki wa Arsenal wanapaswa kushukuru.

Mashabiki wa Arsenal wamekua wepesi wa kupaza sauti na kukosoa pale mambo yanapoenda tofauti na matarajio yao, lakini msimu huu mambo yamekua sio mabaya sana na haya ndiyo mambo makuu matano ambayo mashabiki wa Arsenal wanapaswa kushukuru.

Unai Emery

Katika misimu michache iliyopita kulikuwa na vita kati ya mashabiki waliokuwa wanamuunga mkono Arsene Wenger na wali waliokua wanataka aondoke. Ameondoka na amekuja Unai Emery.

Wenger atabaki kuwa mmoja wa watu muhimu sana katika historia ya Arsenal, lakini ujio wa kocha Unai Emery umeonesha dalili njema, wachezaji wanajituma, mashabiki wanaonekana wapo pamoja.

Timu inajiamini

Nimeangalia mechi zote za Arsenal katika misimu mitano iliyopita na bila kupepesa macho naweza kusema ya kwamba msimu huu timu inaonesha kujiamini zaidi.

Inawezekana zikawa ni mbinu za Unai ama wachezaji wameacha utoto lakini ni jambo la kushukuru kwamba timu inajiamini na inaonesha moyo wa kujituma.

Lucas Torreira

Kwa muda sasa Arsenal ilikuwa haina kiungo mkabaji, mashabiki wengi wanadai ya kwamba Arsenal haina kiungo mkabaji toka Patric Vieira aondoke (ingawa Vieira hakuwa anacheza kama kiungo mkabaji, Gilberto Silva ndiye aliyekuwa kiungo mkabaji).

Ujio wa Lucas Torreira umeifanya Arsenal iwe timu bora zaidi na si ajabu ya kwamba Arsenal bado haijafungwa mchezo wowote ambayo mchezaji huyo ameanza.

Lacazette and Aubameyang

Mambo matano ambayo mashabiki wa Arsenal wanapaswa kushukuru

Unajua jinsi mashabiki wa  timu pinzani wanavyoionea wivu Arsenal? siku ingia katika mtandao wa twitter na tafuta ”i hate Arsenal but” utaona mashabiki wengi wa timu pinzani wanavyoionea wivu safu ya ushambuliaji ya timu ya Arsenal.

Arsenal tumebarikiwa kuwa na washabuliaji wa wawili wa kiwango cha Dunia, ukiondoa Manchester City wenye Aguero na Jesus pale kwa malkia hakuna timu nyingine yenye safu kali ya ushambuliaji kuishinda Arsenal.

Alexis Sanchez hayupo tena Arsenal

Usinielewe vibaya, nilimpenda Alexis alipokuwa Arsenal, nilikuwa shabiki wake mkubwa, lakini miezi 18 ya mwisho akiichezea Arsenal alinikera sana, kuanzia kutabasamu wakati Arsenal ilipofungwa, kupoteza mipira mara 70 kila mechi, kuwalazimisha wachezaji wampasie yeye tu pia bila kusahau aliondoka wa dharau.

Lakini mambo hayo yote hayapo Arsenal kwa sasa, tangu Alexis Sanchez aamine Manchester United cha muhimu alichofanya ni kupiga piano, tunashukuru sana kwa hilo.

Hayo ndiyo mambo matano ambayo mashabiki wa Arsenal wanapaswa kushukuru katika Alhamisi hii ya nne ya mwezi wa  11, je wewe unaona kuna jambo jingine la kushukuru? tuambie hapo chini.

 

Wachezaji wa Arsenal waanza mazoezi-Madogo wanne waitwa

Wachezaji wa Arsenal waanza mazoezi-Madogo wanne waitwa

Wachezaji wa Arsenal wakiwa mazoezini

Baada ya kumalizika kwa mechi za kimataifa wachezaji wa Arsenal leo jumatano walianza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Bournemouth utakaofanyika jumapili.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika katika viwanja vya London Colney wachezaji wanne wa timu ya vijana walionekana wakifanya mazoezi na timu ya wakubwa na pia kuna baadhi ya wachezaji muhimu walikosekana.

Madogo wanne waitwa

Jordi Osei-Tutu,mwenye umri wa miaka 20 anayecheza kama beki alifanya vizuri katika mechi za maandalizi ya ligi kuu lakini alipata majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda kwa sasa amepona na anafanya mazoezi na timu ya wakubwa.

Makinda wengine ambao walionekana kwenye mazoezi hayo ni Charlie Gilmour ambaye anafanya vizuri akiwa na timu ya vijana wenye umri wa miaka 23 na beki wa kati Zech Medley ambaye alikuwa kama mchezaji wa akiba katika mchezo dhidi ya Leicester.

Mchezaji wa nne aliyeonakana mazoezini leo ni beki wa kushoto Dominic Thompson.

Nacho Monreal akosekana

Nacho Monreal na Lichsteiner hawakuonekana katika mazoezi hayo, wachezaji hao walikuwa ni majeruhi na haijulikani ni lini watarudi uwanjani, labda kesho kwenye mkutano na waandishi wa habari, Unai Emery anaweza kuelezea kwa undani.

Lacazette afanya mazoezi

Habari njema ni kwamba wachezaji wa Arsenal,  Alexandre Lacazette, Pierre-Emerick Aubameyang na Laurent Koscielny wote walifanya mazoezi kama kawaida.

Kulikuwa na tetesi za kwamba Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang wangeweza kukosa mchezo huo kutokana na kupatwa na majeraha, lakini kwa sasa inaonekana ya kwamba wamepona.

Laurent Koscielny yeye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu na sasa ameanza mazoezi ingawa bado haijulikani ni lini ataanza kucheza mechi za ushindani

Sven Mislintat na Huss Fahmy wapandishwa vyeo Arsenal

Sven Mislintat na Huss Fahmy wapandishwa vyeo Arsenal

Sven Mislintat

Gazeti la Independent limeandika ya kwamba watendaji wawili wa Arsenal, Sven Mislintat na Huss Fahmy wamepandishwa vyeo na timu ya Arsenal.

Sven Mislintat, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa idara ya usajili tangu ajiunge na Arsenal akitokea Dortmund ya Ujerumani, kwa sasa atakuwa mkurugenzi wa ufundi, wakati Huss Fahmy, ambaye kazi yake ilikuwa ni kufanya mazungumzo ya mikataba, kwa sasa atachukua nafasi iliyoachwa wazi na Raul Sanllehi, kama mkuu wa mambo yote yanayohusiana na soka katika timu ya Arsenal.

Kupandishwa vyeo kwa Mislintat na Fahmy kunatokana na kazi kubwa waliyoifanya katika miezi 12 iliyopita, Mislintat ndiye aliyefanikisha usajili wa wachezaji wote wapya wa Arsenal tangu mwezi wa kwanza mwaka huu. Usajili wa wachezaji kama Pierre-Emerick Aubameyang, Henrikh Mkhitaryan, Sokratis, Lucas Torreira, Matteo Guendouzi na Bernd Leno ni kazi yake.

Fahm ndiye aliyehusika na kujadili mikataba ya wachezaji waliotajwa hapo juu,pia anahusika na kujadili mitakaba mipya ya wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Arsenal.

Uteuzi huo ni muendelezo ya mabadiliko ambayo yanaendelea kutokea ndani ya uongozi wa ngazi za juu wa Arsenal, baada ya aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Arsenal Ivan Gazidis, kuachia ngazi na kujiunga na timu ya AC Milan ya Italia.

Je unaonaje mabadiliko hayo? tupia maoni yako hapa chini.

ARSENAL 0-0 SPORTING-ARSENAL YAFUZU HUKU WELBECK AKIUMIA

Arsenal jana ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya Sporting Lisbon na kufanikiwa kuingia katika hatua ya mtoano ya kombe la Europa League.

ARSENAL 0-0 SPORTING-ARSENAL YAFUZU HUKU WELBECK AKIUMIA

Kutokana na sare hiyo na pia  Vorskla kufungwa na Qarabag, Arsenal imefanikiwa kuingia katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo ingawa bado haijakikishia kuongoza kundi kitu ambacho kocha wa Arsenal, Unai Emery alisema ndilo lengo kuu ya Arsenal kwa sasa.

Katika mchezo huo Arsenal ilicheza vizuri kiasi lakini ilishindwa kufanya mashambulizi ya maana na hivyo kushindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga.

Dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza mchezaji wa Arsenal Danny Welbeck aliumia wakati alipojaribu kupiga mpira wa kichwa na kugongana na mlinzi wa Sporting Lisbon.

Ilikuwa ni rahisi kugundua ya kwamba mambo yalikuwa mabaya kwani alianguka huku akionesha maumivu makubwa na pia sura za wachezaji wa Arsenal zilionesha hali ya hudhuni sana.

Baada ya kutibiwa na kupewa mashine maalumu ya kumsaidia kupumua Welbeck alitolewa nje ya uwanja na kukimbizwa Hospitali.

Akiongea baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Arsenak, Unai Emery alisema hali ya mchezaji huyo bado ilikuwa mbaya na bado aikuwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Wasiwasi mkubwa ulitanda kati ya mashabiki wa Arsenal huku wengi wao wakiamini ya kwamba majeraha aliyoyapata mchezaji huyo yanaweza kumfanya tusimuone uwanjani tena akiwa na jezi ya Arsenal.

Ikumbukwe ya kwamba Welbeck yupo katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na anaweza kuondoka bure katika msimu wa usajili wa majira ya joto.

Sisi kama mashabiki wa Arsenal tungependa kumuombea Danny Welbeck apone haraka ili tumuone tena akivaa jezi za Arsenal uwanjani.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Arsenal ilicheza soka la kiwango kikubwa katika mchezo ambao uliishia kwa sare ya goli 1-1 dhidi ya Liverpool.

Arsenal yaupiga mwingi ikitoka sare na Liverpool

Goli la kusawazisha kutoka kwa mshambuliaji wa Arsenal, Alexandre Lacazette lilimaanisha ya kwamba Arsenal wangeondoka na pointi moja katika mchezo huo uliokuwa mkali na na kusisimua.

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kucheza vizuri lakini Liverpool ndio waliopata nafasi nzuri zaidi za kufunga, kwani walicheza kwa kujihami na kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Kama nilivyosema asubuhi, sehemu ya kiungo ndiyo sehemu ambayo ingeamua matokeo na Lucas Torreira alimpoteza kabisa Fabinho na kutawala eneo la katikati ya uwanja.

Kipindi cha kwanza Liverpool waligongesha miamba mara mbili kupitia kwa wachezaji  Roberto Firmino na Virgil van Dijk.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Arsenal walikianza kipindi cha pili kwa nguvu lakini walikuwa ni Liverpool waliopata goli la kuongoza baada ya golikipa wa arsenal Bernd Leno kufanya makosa ambapo aliutema vibaya mpira na kumkuta James Milner ambaye aliipatia Liverpool goli la kuongoza.

Mabadiliko yaliyofanya na kocha wa Arsenal Unai Emery, ya kumtoka Henrik Mkhitryan na kumuingiza Alex Iwobi yaliisaidia sana Arsenal kwani ilianza kufanya mashambulizi ya hatari zaidi kiasi cha Liverpool kupaki basi.

Alikuwa ni mshambuliaji wa Arsenal,Alexandre Lacazette aliyeipatia Arsenal goli la kusawazisha katika dakika ya 82 baada ya kuwazunguka mabeki wa Liverpool na kupiga shuti kifundi ambalo kipa wa Liverpool,Allison hakuweza kuliona.

Hadi mwisho wa mchezo Arsenal 1-1 Liverpool.

Baada ya kuisha kwa mchezo huo nilifanikiwa kuongea na baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambapo wengi wao walionekana kuridhika na hali ya kujituma kulikooneshwa na timu yao na pia wengi wanaamini ya kwamba Arsenal ilishahili kushinda mchezo huo.

Kwangu mimi Granit Xhaka ndiye aliyekuwa mchezaji nyota katika mchezo wa leo kwani yeye na Lucas Torreira walidhibiti sehemu ya kiungo, Xhaka alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote, aliondoa mipira mingi ya hatari na pia alimsaidia sana Sead Kolasinac upande wa kushoto.

Baada ya mchezo wa leo, Arsenal itaingia dimbani tena Alhamisi ijayo kupambana na timu ya Sporting Lisbon katika michuano ya kugombea kombe la Europa League.

Pia sare ya leo inamaanisha Arsenal imecheza michezo 14 bila ya kufungwa, ikishinda 12 na kutoka sare katika michezo miwili.

Kwa wale ambao hawakuona mchezo huo hapo chini kuna video inayoonesha vipande muhimu vya mchezo huo na magoli yote mawili.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Arsenal leo itakuwa na kibarua kigumu wakati watakapowakaribisha vijana wa Jurgen Klop, Liverpool katika uwanja wa Emirates.

Arsenal vs Liverpool-Muda wa kuwanyamazisha mdomo wapinzani

Pamoja na Arsenal kucheza michezo 13 bila ya kufugwa (imeshinda 12 na kutoka sare 1) bado wachambuji wengi wa soka hawaipi nafasi ya kushinda katika mchezo wa leo. Ukweli ni kwamba  kuna baadhi mashabiki wa Arsenal wanaoamini ya kwamba Arsenal itapoteza mchezo huu.

Ni kweli kwamba Liverpool chini ya Klop wameimalika sana hasa baada ya kumsajili beki kisiki kutoka Southampton Virgil Van Dijk na golikipa Allison. Wakati Arsenal ndio kwanza wana miezi mitatu tangu waanze kujipanga.

Nimekuwa nikiwaangalia Liverpool katika mechi zao nyingi msimu huu, nikiwa mkweli sio timu ya kutisha sana kama wachambuzi wengi wanavyotaka tuamini, kuna mechi dhidi ya Leicester na Huddlefield walishinda kibahati, pia safu yao ya ushambuliaji sio kali kama mwaka jana, ingawa safu yao ya ulinzi imeimarika sana.

Rekodi

Unai Emery amewahi kuifunga Liverpool ya Klop kwenye fainali ya kombe la Europa League baada ya kumzidi ujanja Klop katika kipindi cha pili, Ingawa Arsenal haijawahi kuifunga Liverpool tangu ianze kufundishwa na Klop.

Liverpool imeshinda mara mbili tu katika michezo kumi na nane iliyofanyika Emirates na Arsenal haijaifunga Liverpool katika michezo 6 ya mwisho.

Vikosi

Wao wana Allison ambaye si kipa mbaya lakini anafaungika,ikumbukwe ya kwamba ni kipa ambaye amecheza michezo 100 tu ndani ya miaka mitano iliyopita na kati ya hiyo 50 ilikuwa ni mwaka jana, pia ikumbukwe ya kwanza alikuwa anawekwa benchi na Wojciech Szczęsny.Kwenye suala la makipa naamini ngoma droo.

Linapokuja kwenye mabeki hapo ndipo vijana hao wa Klop wanapoishida Arsenal, kusajiliwa kwa Van Dijk na Allison kumewaimalisha sana, siku hizi hawafungwi magoli ya kijinga kama zamani,Arsenal ina majeruhi wengi upande wa mabeki, sina taarifa kama Kolasinac, Monreal,Sokratis na Bellerin wamepita vipimo vya afya, kama hawajapita inaweza ikawa jioni mbaya sana kwa sisi mashabiki wa Arsenal.

Kwenye kiungo naamini Torreira, Xhaka na Ôzil ni bora kuliko kiungo chote cha Liverpool kama huamini subiri baadaye uone, ila kutokana na beki kuwa mbovu itabidi viungo wa Arsenal wacheze kwa juhudi kubwa kama Arsenal inataka kushinda mchezo wa leo.

Linapokuja kwenye ushambuliaji naamini hakuna tofauti kubwa sana wao wana Manè , Bob Firminho na Moh Salah na sisi tuna Auba,Lacazette na Iwobi.

Utabiri

Ni mchezo mgumu sana kutabiri, lakini naamini katika uwezo wa kikosi cha Arsenal na pia nina imani na kocha Unai, kama nilivyosema tuna kiungo bora kuliko Liverpool na hapo ndipo tunapoweza kuwafungia, ingawa sina imani na safu ya ulinzi kama inaweza kuwazuia Moh Salah na wenzie.

Naani mchezo wa leo utakuwa na magoli mengi na Arsenal itashinda na kuwafunga midomo wapinzani wote waliokuwa wanadai tunazifunga timu dhaifu, naamini Arsenal atashinda kwa goli 3-2.

Je wewe una maoni gani? tupia maoni yako na utabiri hapo chini.

 

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Mchezaji na nahodha wa zamani wa Arsenal,  Per Mertesacker amepandishwa cheo na sasa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Arsenal.

Per Mertesacker Apandishwa Cheo Arsenal

Katika mahojiano na gazeti la Telegraph,Mkuu wa kitengo cha soka katika timu ya Arsenal,Raul Sanllehi alisema ya kwamba Per Mertesacker amejiunga na timu ya wakurugenzi wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa  Raul Sanllehi uteuzi wa Matersacker ni sehemu ya jitihada za uongozi wa Arsenal kuongeza watu wa soka katika ngazi za juu za uongozi wa Arsenal.

Mertesacker anakuwa mtu wa nne ambaye anajua soka kujiunga na timu ya wakurugenzi 15 ambao kwa sasa ndio wanaofanya maamuzi yote yanayoihusu Arsenal kwa sasa.

Kiongozi mwandamini wa Arsenal,Vinai Venkatesham anasema ya kwamba Per anajiunga na Huss Fahmy, Sven Mislintat,na Raul Sanllehi kama vichwa vya soka katika uongozi huo.

Sanllehi hakuweza wazi kama Mertesacker ataendelea na majukumu yake kama mkuu wa kituo cha soka cha Arsenal cha Hale End, lakini tunaamini ya kwamba ataendelea na majukumu yake kama kawaida kwani wakurugenzi wote wa Arsenal wana majukumu tofauti ndani ya Arsenal na sioni sababu kwa nini iwe tofauti kwa Mertesacker.

Kuongezwa kwa Per mwenye uzoefu mkubwa kama mchezaji kwani ameichezea Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani michezo mingi na pia amewahi kushinda kombe la dunia ni jambo zuri kwa timu kwani miaka miaka ya karibuni timu imekuwa ikufanya maamuzi ya ajabu hasa linapokuja suala la mikataba ya wachezaji.

Je unasemaje kuhusu uteuzi huo? tupia maoni yako hapa chini.