Freddie Ljungberg apata ushindi wa kwanza kama kocha wa Arsenal U23

Mchezaji mkongwe wa Arsenal,  Freddie Ljungberg, jana alipata ushindi wa kwanza kama kocha wa timu ya vijana ya Arsenal kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23.

Katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa London, vijana hao wa Ljungberg waliibuka na ushindi wa goli 3-2 dhidi ya vijana wenzao wa West Ham.

Mchezaji aliyeng’ara katika mchezo huo hakuwa mwingine zaidi ya Eddie Nketiah ambaye alifunga magoli mawili katika mchezo huo.Goli lingine lilifungwa na beki  Pleguezuelo.

Freddie Ljungberg apata ushindi wa kwanza kama kocha wa Arsenal U23

Pia wachezaji Nelson na Emile Smith Rowe walishiriki katika mchezo huo.

Pamoja na ushindi huo, bado Freddie Ljungberg hajafanikiwa kuiongoza timu hiyo kumaliza mchezo bila kuruhusu goli.

Kikosi cha Arsenal kilikuwa kama ifuatavyo

                                                  Iliev

                    Olowu-Ballard-Pleguezuelo-Bola

                              Gilmour-Willock

                Amaechi-Smith Rowe-Nelson

                                        Nketiah

Mfumo:4-2-3-1

Akiba: Saka (alichukua nafasi ya  Amaechi dakika ya 73). ambao hawakutumika: Hein, John-Jules, Medley, Olayinka.

 

Arsenal yailazimisha Arsenal Fan TV kubadilisha jina

Timu ya Arsenal imewalazimisha Arsenal Fan TV kubadilisha jina baada ya kufanyika kwa kikao baina ya pande hizo mbili.

Robbie Lyle pichani juu ndiye aliyeanzisha Arsenal Fan TV

Robbie Lyle pichani juu ndiye aliyeanzisha Arsenal Fan TV

Arsenal Fan TV ambayo ni kituo cha Youtube kilichoanzishwa na Robbie Lyle, akiwa na lengo ya kuwapa sauti mashabiki wa Arsenal ili wapate kutoa ya moyoni, lakini katika miaka ya hivi karibuni kimekuwa kikutuhumiwa ya kwamba kimekuwa kikisambaza picha mbaya ya timu.

Mchezaji wa kwanza kukisema hadharani alikuwa Hector Bellerin ambapo alisema ya kwamba wamejipatia umaarufu kupitia matatizo ya Arsenal.

Wahusika wakuu wa kituo hicho wamekuwa pia wakituhumiwa kutafuta vitu vibaya vya timu na kuvitilia mkazo, mfano ni kwamba iwapo Arsenal ikifungwa huwa wanapata watazamaji wengi kwenye video zao na timu ikishinda mapato yanapungua.

Watu wengi wenye akili zao waliacha kuwaangalia hao jamaa kitambo na sasa inaonekana ya kwamba Arsenal pia wamewachoka ambapo wamewataka kubadili jina na kuacha kutumia nembo au jina Arsenal katika video zao.

Kwa sasa kituo hicho kitakuwa kikiitwa AFTVMEDIA.

Arsenal yafungwa na Manchester City

Leo Arsenal ilianza zama mpya chini ya kocha Unai Emery kwa kufungwa 2-0 na timu ya mabingwa watetezi, Manchester City.

Kikosi kilichoanza Arsenal: Cech, Bellerin, Sokratis, Mustafi, Maitland-Niles, Guendouzi, Xhaka, Ramsey, Ozil, Mkhitaryan, Aubameyang.
Wachezaji wa akiba: Leno, Holding, Lichtsteiner, Elneny, Torreira, Iwobi, Lacazette.

Arsenal yafungwa na Manchester City

katika mchezo huo wa ligi kuu ya Uingeleza Arsenal ilianza na wachezaji wapya wawili ambapo Sokratis na Guendouzi walianza.

Binafsi sikutegemea ya kwamba Guenduzi angeanza kutokana na kutozoea kucheza mechi za kimashindano lakini inaonekana mwalimu alimuamini na kumuanzisha katikati pamoja na Xhaka.

Arsenal waliuanza mchezo huo vizuri, lakini hali hiyo ilidumu kama dakika nne au tano kwani City walibadilika na kuanza kuinyanyasa ngome ya Arsenal ambayo ilikuwa ikikatika mara kwa mara.

Man City walipata goli lao la kwanza kupitia kwa Sterling baada ya mabeki wa Arsenal kushindwa kumkaba na kupiga shuti lililombabatiza Sokratis na kutinga nyavuni.

Pamoja na Man City kutawala kipindi cha kwanza hadi mapumziko mchezo huo ulikiwa 1-0.

Pigo kubwa la Arsenal katika kipindi cha kwanza lilikuwa ni kuumia kwa Ainsley Maitland-Niles aliyecheza kama beki wa kushoto , ambaye alilazimika kutoka na nafasi yake kuchukulia Lichtsteiner ambaye ni beki wa kulia.

Arsenal ilikianza kipindi cha pili kwa nguvu hasa baada ya kutoka kwa Ramsey na kuingia Lacazette ambaye alionekana kuwasumbua sana mabeki wa Man City.

Wakati Arsenal wakifanya mashambulizi na mabeki wa Man City wakionekana kutojua la kufanya, timu hiyo ilifanya shambulio la maana na kufanikiwa kufunga gooli la pili kupigia kwa Bernado.

Arsenal ilionekana kucheza vizuri hasa walipokuwa wanakaba lakini walionekana kukosa umakini walipopata mpira hasa katika eneo la ushambuliaji ambapo walikosa nafasi kadhaa za wazi ambazo zingetumiwa vizuri matokeo yangekuwa mengine.

Mesut Ozil na Lacazette walikosa nafasi ambazo wakati mwingine wowote wangeweza kufunga.

Timu ilicheza vizuri na ilionekana kujipanga vyema, kuna makosa madogo madogo ambayo naamini yakifanyiwa marekebisho watafanya vizuri sana katika michezo ijao.

Tumegungwa na timu bora, cha msingi ni kujipanga kwa mchezo ujao #COYG

Alisher Usmanov aamua kuuza hisa za Arsenal kwa Stan Kroenke

Bilionea wa Kirusi,Alisher Usmanov ameamua kuziuza hisa zote alizokuwa anamiliki kwa bilionea wa kimarekani Stan Kroenke.

Alisher Usmanov

Alisher Usmanov (pichani juu) ameamua kuuza hisa zake

Kroenke,ambaye kwa sasa ndiye mwenye hisa nyingi za Arsenal, anamiliki asilimia 67 ya hisa zote na ana mpango wa kununua asilimia 30 kutoka kwa Usmanov na kufikisha asilimia 97 ya umiliki wa Arsenal.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Usmanov amesema ya kwamba amekubali kuuza hisa hizo kwa paundi milioni 550 na anaamini Arsenal itakuwa moja ya timu bora kabisa duniani chini ya Uongozi wa Kroenke na mwanae.

Habari hizo za Usmanov kuuza hisa zimepokelewa vibaya na asilimia kubwa ya mashabiki wa Arsenal, kwani wengi wao wanaamini ya kwamba Stan Kroenke hana nia njema na timu na lengo lake ni kutengeneza faida tu.

Baada ya kusoma kwa makini kila upande baadaye ama kesho nitaandika maoni yangu juu ya mpango huu, je wewe mwana Arsenal unaonaje Kroenke kuwa mmiliki pekee wa Arsenal, ni jambo zuri ama baya? tupia maoni yako hapa chini.

Tetesi-Calum Chambers anakaribia kutua Fulham kwa mkopo

Beki wa kati wa Arsenal, Calum Chambers anakaribia kutua Fulham kwa mkopo wa mwaka mmoja.Katika taarifa tulizozipata kutoka kwa vyanzo mbalimbali ni kwamba leo jumatatu mchezaji huyo atafanyiwa vipimo vya afya na kukamilisha uhamisho huo.

Tetesi-Calum Chambers anakaribia kutua Fulham kwa mkopo

Chambers, mwenye umri wa miaka 23, alisaini mkataba mpya wa miaka minne mwezi wa saba mwaka huu na kulikuwa na tetesi za kwamba alikuwa kwenye mipango ya kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery.

Mimi binafsi sikutegemea kuondoka kwa mchezaji huyo kwani kwa mtazamo wangu mimi naona alicheza vizuri katika michezo ya kirafiki na nilikuwa nafikiria ya kwamba atakuwa ni beki wa akiba, huku akicheza kwenye michuano ya Europa ligi hasa hatua ya makundi na kombe la ligi.

Lakini pia kama ni kweli ya kwamba mchezaji huyo anaondoka linaweza likawa ni jambo jema kwani inaonesha ya kwamba Arsenal wapo sokoni kutafuta beki mwingine wa kati, kwani mabeki wote waliopo hawanishawishi sana.

Pia litakuwa jambo jema kwa Chambers kwani kwa umri wake anatakiwa acheze mara kwa mara na sioni akipata nafasi ya kufanya hivyo akiwa na kikosi cha Arsenal.

Kama nilivyosema hizo ni tetesi tu, wiki hii tutajua kama ni kweli anaondoka ama anabaki.

Arsenal yaifunga Lazio 2-0

Arsenal leo ilicheza mchezo wake wa mwisho wa kirafiki na kufanikiwa kumaliza kwa ushindi baada ya kuifunga timu ya Lazio ya Itali kwa jumla ya goli 2-0.

Arsenal yaifunga Lazio 2-0

wachezaji wa arsenal wakishangilia goli la Reiss Nelson dhidi ya Lazio

Goli la Reiss Nelson katika kipindi cha kwanza na la Aubamayang katika kipindi cha pili yalitosha kuwazamisha mabingwa hao wa zamani wa Italia.

Stephan Lichtsteiner, Lucas Torreira na Granit Xhaka walianza kwa mara ya kwanza msimu huu, huku kocha wa Arsenal Unai Emery akijaribu mfumo wa 4-4-2 ambapo Lacazette na Eddie Nketiah walianza kama washambuliaji wa kati.

Kwa wachezaji wapya Stephan Lichtsteiner alinivutia sana kwani alionekana kucheza kwa kujituma sana na alionesha ya kwamba alikuwa anajua anachokifanya uwanjani.

Upande la Lucas Torreira alikuwa na mchezo wa kawaida, hakuonesha moto kama nilivyotarajia, lakini inaeleweka ya kwamba ndiyo kwanza ameanza mazoezi jumatatu iliyopita itahitaji muda kidogo ili azoee.

Xhaka naye hakufanya vizuri sana kwani alifanya makosa yake ya kawaida na kupoteza mpira katika eneo la hatari la Arsenal.

Kipindi cha pili baada ya kuingia kwa Mkhitaryan,Ôzil Guendouzi na Auba timu ilionekana kuchangamka zaidi na kucheza vizuri.

Baada ya mchezo huu wa leo Arsenal inasafiri kurudi London na kesho wanaendelea na mazoezi ya mwisho mwisho kabla ya kupambana na Manchester City jumapili ijayo.

Arsenal yaifunga Chelsea katika mchezo wa kirafiki

Alex Iwobi alifunga penati ya ushindi na kuisaidia Arsenal kuifunga Chelsea kwa penati 6-5 katika mchezo mkali kuwania kombe la kimataifa uliofanyika mjini Dublin.

Arsenal yaifunga  Chelsea katika mchezo wa kirafiki

Second-half substitute Iwobi held his nerve to clinch victory for the Gunners at the Aviva Stadium after the match finished 1-1 at 90 minutes.

Mchezaji mwingine aliyeingia kipindi cha pili, Alexandre Lacazette,alifunga goli la kusawazisha katika dakika za mwisho,akifuta goli la Chelsea lililofungwa na Antonio Rudiger, mapema kipindi cha kwanza.

Timu zote mbili zilipata penati tano za mwanzo kabla ya kiungo wa kiingeleza Ruben Loftus-Cheek penati ya sita huku Iwobi akifunga na kuipa Arsenal ushindi.
Pamoja na ushindi huo, Arsenal hawakuwa na furaha sana kwani kiungo Aaron Ramsey aliumia dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Smith Rowe.

Chelsea walianza kipindi cha kwanza vizuri na kufanikiwa kupata goli dakika ya tano ya mchezo huo na pia katika kipindi cha kwanza walipata penati na Alvaro Morata alipiga penati hiyo iliyodakwa na golikipa wa Arsenal Petr Cech.

Chelsea walicheza vizuri sana kipindi cha kwanza ambapo walikosa nafasi kama mbili tatu za kufunga goli nyingine huku kinda Callum Hudson-Odoi,akimkimbiza sana Hector Bellerin.

Arsenal walikianza kipindi cha pili kwa nguvu na huku chelsea wakionekana kurudi nyuma kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele.

Zikiwa zimebaki sekunde chache kumalizika kwa pambano hili,Ôzil alipiga bonge la pasi iliyomkuta Reiss Nelson,ambaye alipiga krosi iliyomkuta Lacazette ambaye bilia ajizi aliujaza mpira kimiani.Mpaka kipenga cha mwisho kinapulizwa Arsenal 1- 1 Chelsea.

Arsenal ilienda na kushinda penati 6-5.

Arsenal itacheza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Lazio utakaofanyika jumamosi ijayo.

kwa wale ambo hawakuona mchezo huo, hapo chini nimekuwekea magoli na penati zote.

Lucas Torreira na Stephan Lichtsteiner waanza mazoezi Arsenal

Wachezaji wapya wa Arsenal,Lucas Torreira na Stephan Lichtsteiner jana walianza rasmi  mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi na michezo mingine.

Lucas Torreira na Stephan Lichtsteiner waanza mazoezi Arsenal

Torreira akiwa mazoezini

Nacho Monreal, Joel Campbell na Granit Xhaka pia wamerudi na kuanza mazoezi katika uwanja wa mazoezi wa Arsenal, London Colney baada ya kushiriki katika hatua za mtoano za kuwania kombe la dunia zilizofanyika nchini Urusi.

Mshambuliaji wa Uingeleza  Danny Welbeck, ndiye mchezaji pekee wa Arsenal ambaye hajaanza mazoezi kwa sasa baada ya kufika nusu fainali ya kombe hilo, na anategemewa kuanza mazoezi wiki ijayo.

Macho na masikio ya mashabiki wengi wa Arsenal yalikuwa kwa Torreira , kwani wengi wao wamefurahishwa sana na usajili huo.

Torreira alisafiri jumamosi kutoka kwao Uruguay na kuingia Uingeleza jumapili na jana jumatatu alianza rasmi mazoezi ya wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza.

Itakuwa ni vigumu kwa wachezaji hao kucheza mchezo wa kesho dhidi ya Chelsea ila naamini watahusika katika mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Lazio jumamosi ijao.

Arsenal itaanza kampeni za ligi kuu ya Uingeleza kwa kuikaribisha Machester City ndani ya siku 13 zijazo na ni mategemeo makubwa ya mashabiki wengi ya kwamba wachezaji hao watakuwa tayari kucheza dhidi ya mabingwa watetezi.

Arsenal yaipiga mkono PSG

Timu ya Arsenal imewafunga mabingwa wa Ufaransa PSG, kwa jumla ya magoli 5-1 katika mchezo wa kirafiki kugombea kombe la kimataifa.

Arsenal yaipiga mkono PSG

wachezaji wa Arsenal wakishangilia goli la Mesut Özil dhidi ya PSG

Katika mchezo huyo tulishuhudia Mesut Özil akianza na pia akivaa kitambaa cha unahodha wa Arsenal kwa mara ya kwanza,pia katika mchezo huo wachezaji wa Arsenal waliokuwa katika kombe la dunia,Alex Iwobi na Ustaadhi Elneny walianza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kupata goli baada ya Mesut Özil kumalizia krosi nzuri ya Aubamayang.Hadi kipindi cha kwanza kinaisha Arsenal walikuwa wanaongoza kwa goli hilo moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko na PSG ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli la kusawazisha kupitia mkwaju wa penati baada ya Kolasinac kumuangusha mchezaji wa PSG.

Magoli mawili kutoka kwa Alexandre Lacazette yaliifanya Arsenal iongoze kwa goli 3-1 katika dakika ya 67 na 70.

Dakika ya 86 Rob Holding aliifungia Arsenal goli la nne kwa kichwa kutoka umbali wa mita 18 , kabla ya Eddie Nketiah kufunga kitabu cha magoli baada ya kuifungia Arsenal goli la tano.

Hadi mwisho wa mchezo huo Arsenal 5-1 PSG.

Katika mchezo huo Matteo Gandeuzi alicheza kwa kiwango cha hali ya juu na pia kinda Smith Rowe aliyeingia kipindi cha pili alicheza vizuri na pia ndiye aliyetengeneza goli la kwanza la Lacazette.

Kesho Arsenal inasafiri kurudi London ambapo kujiandaa na michezo mingine ya kirafiki dhidi ya Chelsea na Lazio wiki ijayo.

Kama unataka kuangalia magoli nimekuwekea hapa chini #COYG

Rasmi Jeff Reine-Adelaide ajiunga na Angers

Mchezaji kiungo wa Arsenal Jeff Reine-Adelaide, amejiunga na timu ya Angers, inayoshiriki ligi ya Ufaransa Ligue 1, ambayo aliichezea kwa mkopo msimu ulioisha.

Rasmi Jeff Reine-Adelaide ajiunga na Angers

Katika taarifa rasmi ya Arsenal, hawajasema mchezaji huyo ameuzwa kwa kiasi gani cha pesa lakini inasemekana timu hiyo ya Ufaransa imetoa dau la paundi milini 2 ili kumpata mchezaji huyo.

Jeff aliachwa kwenye kikosi cha Arsenal kilichopo Singapore kucheza michezo yake ya kirafiki.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Arsenal mwezi wa saba mwaka 2015 mwezi wa saba akitokea timu ya ligue 2, Racing Club ambayo aliichezea katika timu za vijana na za wachezaji wa akiba.
Jeff aliichezea Arsenal katika michezo nane ya kikosi cha kwanza kwa miaka mitatu aliyokaa katika timu.Katika msimu wa mwaka 2016/17 alicheza michezo mitatu kati ya minne katika michuano ya kombe la ligi kabla ya kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 23.

Mwishoni mwa msimu huo alipata majeraha ambayo yalimuweka nje ya uwanja kwa karibu mwaka mzima na aliporudi akaenda kwa mkopo na inaonekana ameshindwa kumshawishi kocha mpya Unai Emery na hivyo Arsenal kuamua kumuuza.

Sisi kama mashabiki wa Arsenal tunamtakia Jeff kila la heri katika timu yake mpya .

 

Mechi za kirafiki-Arsenal 1-1 Atletico Madrid

Arsenal imeendelea kucheza mechi za kirafiki kujiandaa na msimu ujao baada ya leo kucheza na timu ya Atletico Madrid ambapo timu hizo zilitoka sare ya goli 1-1 na Arsenal kufungwa kwa mikwaju ya penati.

Mechi za kirafiki-Arsenal 1-1 Atletico Madrid

Arsenal ilicheza mfumo wa 4-3-3, Rob Holding Mustafi,Kolanasic na Bellerin waliunda mabeki wanne, Ramsey,Gendauzi na Emile Smith Rowe waliunda safu ya kiungo na Lacazette,Reiss Nelson na Auba waliunda safu ya ushambuliaji.

Arsenal waliuanza mchezo huo kwa kasi huku kiungo kinda Emile Smith Rowe akionesha umahiri wa hali ya juu,ambapo mara nyingi alionekana kuwasumbua wachezaji wa Atletico Madrid.

Baada ya dakika ya 25 Atletico walianza kucheza vizuri huku Arsenal wakionekana kuanza kupunguza moto,Lacazette alikaribia kufunga mara mbili katika kipindi cha kwanza lakini walikuwa ni Atletico Madrid waliopata goli ya kuongoza baada ya Vietto kupiga mpira wa kichwa na kumuacha golikipa wa Arsenal Bernd Leno akiruka bila ya mafanikio.

Smith Rowe ambaye alicheza vizuri katika kipindi cha kwanza alianza vizuri kipindi cha pili baada ya kifungia Arsenal goli la kusawazisha baada ya kuwapiga chenga wachezaji watatu wa Atletico Madrid na kuachia kombora ambalo golikipa wao alishindwa kulitoa.

Baada ya hapo timu zote zilifanya mabadiliko makubwa na kuufanya mchezo huo kupoa na hadi mwisho wa mchezo ilikuwa Arsenal 1-1 Atletico Madrid.

Baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare, zilipigwa penati ambapo Arsenal walikosa penati 3 (waliokosa ni Mkhitaryan,Nketiah na Joe Willock na hivyo Arsenal kufunga 3-1 kwenye penati.

Katika mchezo huo wachezaji walionivutia zaidi ni Matteo Gendauzi na Emile Smith.

Arsenal itaendelea na michezo ya kirafiki jumamosi ambapo itapambana na timu ya PSG kutoka Ufaransa.