Eddie Nketiah ajiunga na Leeds United hadi mwisho wa msimu

Timu ya Leeds United inayofundishwa na kocha Marcelo Bielsa imeshinda vita ya kumsajili mashambuliaji wa Arsenal Eddie Nketiah kwa mkopo hadi mwisho wa msimu unaoanza leo.

Eddie Nketiah ajiunga na Leeds United hadi mwisho wa msimu

Vita vya kumuwania kinda huyo wa Arsenal ilikuwa kubwa kwani kulikuwa na timu 23 kutoka Uingeleza, Italia, Hispania na Ujerumani zilizokuwa zinamuhitaji mchezaji huyo.

Lakini inasemekana ya kwamba mkurugenzi wa ufundi wa Leeds United aliandaa hotuba kali ya kumshawishi mchezaji huyo ajiunge na timu yao kwani wana maradi mkubwa na wangependa awe sehemu ya mipango yao kwa msimu mpya na mchezaji huyo alikubali.

Arsenal imeamua kumuachia mchezaji huyo baada ya kumsajili kinda wa Brazil, Martinelli na pia inaonekana ya kwmba Reiss Nelson atabaki Arsenal msimu huu.

Kucheza chini ya kocha anayesifika kwa mbinu kali za soka kama Marcelo Bielsa kunaweza kuwa na manufaa makubwa kwa mchezaji huyo kwani kutasaidia kumjenga kama mshambuliaji wa kati na pia atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na kama angebaki Arsenal.

Kila la Heri Eddie, tunategemea msimu ujao utarudi ukiwa umekomaa na tayari kuisaidia Arsenal.

Dominic Thompson ajiunga na timu ya Brentford

Beki kinda wa Arsenal, Dominic Thompson amejiunga na timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza Uingeleza ya  Brentford kwa mkataba wa kudumu.

Dominic Thompson ajiunga na timu ya  Brentford

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, pia ni uzao wa chuo cha soka cha Arsenal, Hale End Academy ambacho alijiunga nacho mwaka 2012.

Dominic alisaini mkataba wake wa kwanza na Arsenal mwezi wa 6 mwaka 2018 na tayari amechacheza mechi 39 katika timu za vijana wenye umri wa miaka 18 na 23, hakuwani kuichezea timu ya wakubwa katika michezo rasmi ya kimashindano.

Kutokana na ujio wa beki William Saliba mwenye umri wa miaka 18, pia na mabeki wengine vijana kama Konstantinos Mavropanos ambao wana uwezo mkubwa kumliko ingekuwa ni vigumu kwa mchezaji huyo kupata nafasi katika kikosi cha Arsenal katika miaka mingi ijayo na ndiyo maana uongozi wa Arsenal ukaamua kumuuza.

Ada ya uhamisho bado haijawekwa wazi ingawa taarifa tulizonazo ni kwamba timu hiyo itailipa Arsenal ada inayoweza kufikia paundi milioni tatu, kiasi kamili kitategemea na mafanikio ambayo mchezaji huyo atayapata na timu yake mpya na pia Arsenal watapata sehemu ya malipo ya ada iwapo Brentford itaamua kumuuza mchezaji huyo.

Kila la heri Dominic.

Rasmi: Alex Iwobi ajiunga na Everton

Mchezaji wa kimataifa wa Nigeria Alex Iwobi ameihama timu ya Arsenal na kujiunga na timu ya Everton baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano kuichezea timu hiyo ya jijini Liverpool.

Rasmi: Alex Iwobi ajiunga na Everton

Iwobi ambaye ni zao la chuo cha soka cha Arsenal, Hale End Academy, alipandishwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal mwaka 2015 na aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger baada ya kufanya vizuri katika kikosi cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 23.
Alex Iwobi mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Arsenal akiwa mtoto wa miaka 8 miaka 15 iliyopita na amefanikiwa kuzichezea timu zote za Arsenal kuanzia ngazi ya awali kabisa.

Aliichezea timu ya wakubwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015, na baadaye kuichezea Arsenal katika jumla ya michezo 148 ambapo alifanikiwa kufunga magoli 15, alizoa pasi za mwisho zilizozaa magoli mara 27, akiwa katika kikosi kilichobeba kombe la FA mara mbili na kushinda ngao ya hisani mara moja.

Pia ameishaichezea timu ya taifa ya Nigeria katika michezo 36 ambapo hivi karibuni aliisaidia kushika nafasi ya tatu katika kombe la mataifa huru ya Africa.

Ujio wa Nicolas Pepe na Dan Ceballos, kungepunguza muda wake wa kuwa uwanjani na pia kwa upande wa Arsenal ilikuwa ni vigumu kuacha dau la paundi milioni 40 ambalo Everton imetoa ili kumpata mchezaji huyo.

Ni vigumu kuona mchezaji ambaye ni shabiki wa Arsenal na amekulia ndani ya Arsenal akiondoka ila naamini hili dili ni zuri kwa pande zote tatu, Arsenal wanapata pesa kusaidia kufidia pesa walizotoa kufanya usajili msimu huu, Iwobi anaenda kucheza mara kwa mara katika timu nzuri kama Everton na Everton wanapata mchezaji ambaye ana kiwango kizuri na mwenye umri mdogo.

Kila la heri Naija Boy.

Oooh Alexiiii Iwoobi

#COYG

 

Rasmi-David Luiz ajiunga na Arsenal

Arsenal imekamilisha usajili wake wa mwisho katika dirisha hili la usajili baada ya kumnasa beki wa kati wa Chelsea David Luiz kwa dau linalokadiliwa kufikia paundi milioni 8.

David Luiz

David Luiz alianza kucheza soka katika timu ya Vitoria ya kwao Brazil, kabla ya kuhamia Ureno ambapo aliichezea timu ya Benfica. Pia ameishaichezea timu ya Chelsea katika vipindi viwili tofauti, pia aliichezea timu ya PSG ya ufaransa kwa miaka miwili ambapo alikuwa chini ya kocha wa sasa wa Arsenal, Unai Emery.

Pia Luiz ameishaichezea timu ya taifa ya Brazil katika michezo 56.

Mara baada ya kukamilika kwa usajili huo kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery alisema, “David Luiz ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ninategemea kufanya nae kazi kwa mara nyingine tena, ni mchezaji mwenye jina kubwa na ataongea nguvu katika safu yetu ya ulinzi.”

David Luiz atavaa jezi namba 23.

David

Katibu katika chama la wana David.

#COYG

Rasmi-Kieran Tierney atua Arsenal

Hatimaye Arsenal imefanikiwa kumnasa beki wa kushoto wa Celtic, Kieran Tierney ambaye jana usiku alikamilisha usajili kwa dau linalokadiliwa kufikia paundi milioni 25 ambapo alisaini mkataba wa miaka mitano.

Kieran Tierney

Beki huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 22 alizaliwa katika kisiwa cha Man na amekuwa mchezaji wa Celtic tangu akiwa na miaka 7.

Mchezaji huyo aliichezea timu ya Celtic katika michezo 170 na pia ameishaichezea timu ya taifa ya Scotland mara 12.

Usajili wa mchezaji huyo ni muhimu sana kwani Arsenal ilikuwa inapengo upande wa beki wa kushoto, Nacho Monreal umri unamtupa mkono, wakati Sead Kolasinac hana uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto katika mfumo wa mabeki wanne hali iliyomlazimisha Unai Emery kutumia mabeki watano katika michezo mingi msimu uliopita.

Kieran Tierney alifanyiwa vipimo vya afya jana jiona katika viwanja vya mazoezi vya Arsenal, London Colney, na mara baada ya kufuzu vipimo hivyo alijiunga na wachezaji wengine wa Arsenal.

Mchezaji huyo atavaa jezi namba tatu ambayo ilikuwa haina mtu.

Rasmi-Kieran Tierney atua Arsenal

Mara baada ya kukamilika kwa usajili huo, kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery alisema, “Tuna furaha kubwa ya kwamba Kieran ameamua kujiunga na sisi, ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa ambaye ataendelea kuboresha kiwango chake, atasaidia kuiongezea nguvu safu ya ulinzi.”

Karibu katika chama la wana Kieran Tierney.

#COYG

Arsenal wakubaliana na Celtic kuhusu ada ya uhamisho wa Kieran Tierney

Arsenal imekubaliana na timu ya Celtic kuhusu ada ya uhamisho wa beki wa kushoto Kieran Tierney.

Arsenal wakubaliana na Celtic kuhusu ada ya uhamisho wa  Kieran Tierney

Awali kulikuwa na tetesi za kwamba Arsenal ilitaka kumsajili mchezaji huyo lakini Celtic walikataa ofa mbili za mwanzo zilizotolewa na Arsenal.

Lakini sasa vyanzo vingi vya habari vikiwemo BBC na Sky Sport wanahabarisha ya kwamba timu hizo zomeshafikia makubaliano juu ya ada wa uhamisho na mchezaji huyo tayari alikuwa safarini kuelekea London kwa ajili ya kuwanyiwa vipimo kabla ya kusaini mkataba wa miaka mitano wa kuichezea Arsenal.

Baada ya kuruhusu magoli 52 msimu uliopita Arsenal ina mpango wa kuongeza nguvu katika safu yake ya ulinzi na usajili wa mchezaji huyo ni dalili njema za kupatiwa ufumbuzi kwa tatizo hilo.

Pia Arsenal ipo njiani kutafuta beki wa kati na kulikuwa na tetesi za kwamba David Luiz huenda akawa mchezaji wa Arsenal kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili leo hii.

Iwapo Arsenal itakamilisha usajili wa wachezaji hao wawili itakuwa imepiga hatua kubwa kwani tayari imeshawasajili Martineli, Pepe, William Saliba (ametolewa kwa mkopo ) na Dan Ceballos (amesajiliwa kwa mkopo).

 

Takuma Asano ajiunga na Partizan Belgrade

Arsenal imetangaza kuachana na mchezaji wake ambaye ni raia wa Japan, Takuma Asano ambaye amejiunga na timu ya Partizan Belgrade ya Serbia.

Takuma Asano ajiunga na Partizan Belgrade

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Japan, mwenye umri wa miaka 24 alijiunga na Arsenal akitokea timu ya Sanfrecce Hiroshima mwezi wa saba mwaka 2016.

Alijiunga na timu ya daraja la pili ya Ujerumani, VfB Stuttgart timu ambayo aliichezea hadi mwisho wa msimu wa mwaka 2017/2018.

Mwezi wa nane mwaka 2018 alijiunga na timu nyingine ya ligi daraja la pili ya Ujerumani ya Hannover 96.

Takuma anaondoka Arsenal bila ya kuwahi kuichezea katika mchezo wowote, sababu kubwa ni kukosa kwa kibali cha kufanya kazi nchini Uingeleza.

Pia miaka miwili amekubwa na balaa la majeraha hali iliyomfanya kukosa sehemu kubwa msimu na kushindwa kuishawishi timu ya Hannover 96 kumnunua moja kwa moja.

Kila la Heri Takuma Asano.

#COYG

#PepeIsHere-Rasmi Nicolas Pepe ni mchezaji wa Arsenal

Ni kama ndoto vile, Arsenal imekamilisha usajili wa winga Nicolas Pepe kutoka katika timu ya Lille ya Ufaransa kwa dau la uhamisho linalokadiliwa kufikia paundi milioni 72.

Kusajiliwa kwa mchezaji huyo kunamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na timu ya Arsenal na pia anakuwa mchezaji wa kiafrika ghali zaidi Duniani.

#PepeIsHere-Rasmi Nicolas Pepe ni mchezaji wa Arsenal

Mara baada ya kukamilika kwa usajili huo, kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery alisema,”Kusajili winga mwenye kiwango kikubwa ilikuwa ni moja ya matarajio yetu katika dirisha hili la usajili na ninafuraha kubwa ya kwamba ameamua kujiunga na sisi.”  “Ataongeza mbio nguvu na utengenezaji wa nafasi za magoli na kuongeza idadi ya magoli ya kufunga” alimalizia kocha huyo.

Pepe alizaliwa katika mji wa Mante-la-Jolie, nchini Ufaransa, wazazi wake wote wawili wakiwa wanatoka Ivory Coast.
Pepe, mwenye umri wa miaka 24 alijiunga na timu ya Lillle mwaka 2017 akitokea katika timu ya Angers.
Katika misimu miwili aliyeyoichezea timu ya Lille, Pepe amefunga magoli 37 katika micheza 79 aliyoichezea timu hiyo.

Aliitwa katika timu ya Ivory Coast kwa mara ya kwanza mwaka 2016, mpaka sasa amekwishawachezea tembo hao wa Ivory Coast mara 15.

Pepe anakuwa mchezaji wa nne kujiunga na Arsenal msimu huu akiwafuata, Martinelli, William Saliba na Dani Ceballo ambao wote wamejiunga na Arsenal msimu huu.

Karibu katika chama la wana Pepé.

#PepeIsHere

Arsenal ipo katika hatua za mwisho za kumsajili Nicolas Pepe

Arsenal imefikia makubaliano ya dau la paundi milioni 72 na timu ya LOSC Lille ili kumsajili winga matata mzaliwa wa Ivory Cost, Nicolas Pepe.

Arsenal ipo katika hatua za mwisho za kumsajili Nicolas Pepe

Habari hizo zilizopolewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wengi wa Arsenal zilitolewa na mtangazani wa BBC,David Ornstein wakati wa kipindi cha michezo cha BBC radio.

Katika mahojiano na kipindi hicho, David alisema ya kwamba  tayari Lille na Arsenal walikuwa wameshakubaliana na Arsenal kuhusu uhamisho wa mchezaji huyo ingawa kulikuwa bado hakuna makubaliano rasmi kati ya kambi ya mchezaji huyo na timu ya Arsenal.

 

Mara baada ya kutoka kwa taarifa hizo, zilikuja taarifa nyingine ambazo zinadai ya kwamba tayari mchezaji huyo ameshaafikiana na Arsenal kuhusu mshahara na pia mwakilishi wake atapokea Euro milioni 10 kama asante kwa mshawishi Pepe kuja Arsenal.

Winga huyo ambaye alifunga magoli 22 na kusaidia kupatikana kwa mengine 11 inasemekana ya kwamba alikuwa anawaniwa na timu nyingi kubwa barani Ulaya zikiwemo, Liverpool, Manchester United, Bayern Munich na Napoli na kuamua kuja Arsenal ni ishara tosha ya kwamba bado Arsenal ina mvuto linapokuja suala la kusajili wachezaji wenye mvuto mkubwa.

Pia katika taarifa hizo David aligusia ya kwamba Arsenal haina mpango wa kumuuza mmoja kati ya Aubamayang au Lacazette ili kulipia gharama za usajili huo habari ambazo ni kama mziki mtamu mbele ya mashabiki wa Arsenal.

Baada ya Arsenal kuwapoteza Alexis Sanchez na Theo Walcott, Arsenal ilikuwa haina mawinga na kulazimisha kuwachezesha viungo washambuliaji kama mawinga kitu ambacho kilisababisha timu kushindwa kufanya mashambulizi kupitia pembeni mwa uwanja hasa inapocheza na timu ndogo zinazokusanya wachezaji kati kati ya uwanja na kusababisha kupata matokea yasiyo ridhisha, usajili wa Pepe utakuja kuondoa tatizo hilo.

Rasmi-William Saliba ajiunga na Arsenal

Arsenal imekamilisha usajili wa beki kinda wa Kifaransa, William Saliba akitokea timu ya Saint Etienne kwa mkataba wa miaka 6.

Rasmi-William Saliba ajiunga na Arsenal

Beki huyo ambaye ni mmoja ya mabeki vijana bora kabisa atarudi nyumbani kwao Ufaransa ambapo ataichezea timu ya Saint-Entienne kwa mkopo wa mwaka mmoja ambapo mwakani atajiunga na timu ya Arsenal kwa miaka mitano.

Mara baada ya kukamilika kwa usajili huo, kocha mkuu wa Arsenal alisema: “Tuna furaha kubwa ya kwamba William ameamua kujiunga nasi. Timu nyingi kubwa zilikuwa zinamtaka lakini aliamua kuja Arsenal na kuwa sehemu ya timu tunayoitengeneza kwa miaka mingi ijayo. Atabaki Ufaransa kwa msimu ujao ili apate uzoefu zaidi, baadaye tunategemea atajiunga nasi.”

Saliba akiwa na jezi ya Arsenal

Saliba pichani akiwa na jezi ya Arsenal

William alisaini mkataba wake wa kwanza akiwa na miaka 17. Aliichezea timu ya Saint-Etienne katika mchezo ambao walishinda kwa goli 3-2 dhidi ya Toulouse tarehe 25 ya mwezi wa 9 mwaka 2018.

Katika msimu uliopita mchezaji huyo alianza katika michezo 13 ya ligi kuu ya Ufaransa, Ligue 1.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18, ni sehemu ya timu ya taifa ya Ufaransa ya wachezaji wenye umri wa miaka 20 akicheza na kinda mwingine wa Arsenal, Matteo Guendouzi.

Karibu katika chama la wana William Saliba. #COYG

 

Rasmi-Dani Ceballos ajiunga na Arsenal kwa mkopo

Kiungo wa kihispania Dani Ceballos amejiunga na Arsenal kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea kwa wakali wa Hispania, Real Madrid.

Rasmi-Dani Ceballos ajiunga na Arsenal kwa mkopo

Dani Ceballos mwenye umri wa miaka 22 aliianza katika michezo 13 ya la Liga akiwa na Real Madrid msimu uliopita.

Akiongea mara baada ya kikamilika kwa usajili huo, kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery alisema,: “Tuna furaha kubwa ya kwamba Dani ameamua kujiunga nasi, ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na ana uwezo mkubwa katika kutengeneza nafasi na kupiga pasi zinazomfikia mlengwa.”

Dani alijiunga na timu ya vijana ya Sevilla mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka nane, baadaye alienda kuchezea timu ya mji alikozaliwa ya CD Utrera, na alimaliza mafunzo yake ya soka katika timu ya Real Betis, ambapo alisaini mkataba wake wa kwanza mwezi wa pili mwaka 2014.

Mwezi wa 7 mwaka 2017, Dani alisaini timu ya Real Madrid katika mkataba wa miaka 6 ambapo aliichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza mwezi mmoja baadaye.

Kiungo huyo wa kati pia ameishawakilisha timu ya taifa ya Hispania ya wakubwa, aliichezea kwa mara ya kwanza mwezi wa 9 mwaka 2018 na kufanikiwa kuifungia nchi yake goli la kwanza miezi miwili baadaye.

Mchezaji huyo ambaye ni kiungo mtengenezaji (kama Santi Cazorla) alikuwa ni sehemu ya timu ya taifa ya Hispania iliyobeba taji la Ubingwa wa Ulaya kwa vijana chini ya miaka 21 ambapo alifunga magoli mawili.

Dani atavaa jezi namba 8 katika msimu ujao, na anaweza akaichezea Arsenal kwa mara ya kwanza jumapili hii katika kombe la Emirates.

Karibu katika chama la wana Dani Ceballos.

#HolaDani #COYG