Granit Xhaka aiongoza Switzerland kufuzu fainali za Nations League

Kiungo wa Arsenal, Granit Xhaka akiwa nahodha wa timu ya taifa ya  Switzerland , jana usiku aliiongoza nchi hiyo kuishinda timu ya taifa ya Ubelgiji kwa jumla ya magoli 5-2 na kufanikiwa kufuzu katika fainali za kombe la  Nations League zitakazofanyika mwakani.

Alikuwa ni mchezaji Thorgan Hazard aliyefunga magoli mawili ndani ya dakika 17 za mchezo na kuwafanya wabelgiji waongoze kwa goli 2-0.

Ricardo Rodriguez alifunga kwa njia ya mkwaju wa penati katika dakika ya 26, kabla  Haris Seferovic hajasawazisha kwa shuti kali.

Ikiwa imebaki dakika moja kwenda mapumziko, Seferovic alifunga goli safi akitumia mguu wake wa kushoto.

Nico Elvedi aliifungia Switzerland goli la nne kabla ya Seferovic kufunga goli la tano, kwa matokeo hayo Xhaka atacheza katika fainali za kombe hilo zitakazofanyika mwakani.

Granit Xhaka aiongoza Switzerland kufuzu fainali za Nations League

Mchezaji mwingine wa Arsenal aliyecheza mechi za kimataifa hapo jana alikuwa ni beki wa kati Sokratis, aliichezea timu yake ya taifa ya Ugiriki ilipofunga na timu ya taifa ya Estoni kwa jumla ya goli 1-0.

Granit Xhaka aiongoza Switzerland kufuzu fainali za Nations League

Taarifa za wachezaji majeruhi Arsenal

Timu ya madaktari wa Arsenal leo kupitia tovuti ya timu walitoa taarifa kuhusu wachezaji majeruhi wa Arsenal, taarifa hizo ni kama ifuatavyo.

Taarifa za wachezaji majeruhi Arsenal

Nacho Monreal

Nacho ana matatizo ya msuli na leo anafanyiwa vipimo ili kuangalia uwezekano kama anaweza kucheza kesho ama la.

Sead Kolasinac
Kolasinac naye ana tatizo kama la Monreal naye atafanyiwa vipimo leo, pia kuna taarifa ya kwamba leo alifanya mazoezi kama kawaida na kikosi cha kwanza.

Hector Bellerin
Aliumia katika mchezo dhidi ya Palace, atakosa mchezo wa kesho, ila atafanyiwa vipimo kuangalia uwezekano wa kucheza katika mchezo dhidi ya Liverpool.

Mo Elneny
Ni majeruhi na anategemewa kurudi uwanjani ndani ya wiki mbili, hivyo kukosa michezo kama minne hivi.

Laurent Koscielny
Ameanza mazoezi na timu ya kwanza baada ya kuumia kifundop cha mguu, haijulikani lini atacheza mechi ya ushindani.

Dinos Mavropanos

Yupo katika hatua za mwisho za kupona anategemea kuanza mazoezi kamili mwezi ujao.

Katika michezo miwili sasa Arsenal ilicheza bila beki wa kushoto na kumlazimisha Granit Xhaka kucheza nafasi hiyo, ingawa hakufanya vibaya litakuwa jambo jema kama mabeki wa kushoto watarudi katika mchezo wa kesho.

Tukutane kesho Arsenal Vs Blackpool.

Taarifa ya wachezaji majeruhi wa Arsenal

Tatizo la majeruhi bado linaendelea kuikumba timu ya Arsenal, na timu ya madaktari  imetoa taarifa zifuatazo kuhusu wachezaji waliokuwa majeruhi.

Taarifa ya wachezaji majeruhi wa Arsenal

 

Mesut Ozil
Ozil alikuwa na maumivu ya mgongo, kwa sasa ameshapona na ameanza mazoezi na wachezaji ambao hawajaitwa katika timu za taifa.

Ainsley Maitland-Niles
Niles aliumia katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu ya Uingeleza mwezi wa nane mwaka huu na tayari amepona na ameshaanza mazoezi kamili.

Danny Welbeck

Aliondolewa katika kikosi cha Uingeleza, kwa sasa bado anafanyiwa vipimo kuangalia kama kuna uwezekano wa kucheza katika mchezo ujao dhidi ya  Leicester City jumatatu ijayo ya tarehe 22 mwezi huu.

Petr Cech
Aliumia, naye kama Welbeck anafanyiwa vipimo kujua kama atakuwa tayari kucheza katika mchezo dhidi ya ya  Leicester City jumatatu ijayo ya tarehe 22 mwezi huu.

Dinos Mavropanos
Ana maumivu ya kifundo cha mguu anatazamiwa kuanza mazoezi mwishoni mwa mwezi huu.

Laurent Koscielny
Nahodha wa Arsenal tayari ameshaanza mazoezi mepesi na anatazamiwa kuanza mazoezi rasmi mwanzoni mwa mwezi ujao.

Hii ndiyo hali ya wachezaji waliokuwa majeruhi na tarehe wanazotarajiwa kuanza mazoezi.

Wachezaji wa Arsenal katika mechi za kimataifa

Wakati ligi kuu ya Uingeleza ikiwa imesimama kupisha mechi za kimataifa, baadhi ya wachezaji wa arsenal wameshiriki katika michezo hiyo na kuzisaidia timu zao za taifa katika michezo mbalimbali.

Alex Iwobi

Wachezaji wa Arsenal katika mechi za kimataifa

Alex Iwobi alitoa pasi ya mwisho kuisaidia Nigeria kuifunga timu ya taifa ya Libya kwa goli 4-0,mshambuliaji wa Ningeria Odion Ighalo alifunga magoli matatu katika mchezo huo.

Henrikh Mkhitaryan

Henrikh Mkhitaryan alikuwa nahodha wa Armenia wakati timu yake ya taifa ilipofungwa na 1-0 na timu ya taifa ya Gibraltar.

Bernd Leno

Bernd Leno alikuwa katika benchi la wachezaji wa akiba wakati timu ya taifa ya Ujerumani ilipopokea kipigo kikali kutoka kwa timu ya taifa ya Uholanzi.

Lucas Torreira

Wachezaji wa Arsenal katika mechi za kimataifa

Lucas Torreira alicheza dakika zote 90 wakati timu ya taifa ya Uruguay ilipopokea kipigo cha goli 2-1 kutoka katika timu ya taifa ya Korea ya Kusini.

Sokratis

Sokratis alikuwa nahodha wa Ugiriki wakati timu ya taifa ya nchi hiyo ilipoishinda timu ya taifa ya Hungary kwa goli 1-0.

Granit Xhaka

Granit Xhaka captains Switzerland

Granit Xhaka alicheza dakika zote 90 wakati timu yake ya taifa ya Switzerland ilipofingwa magoli 2-1 na timu ya taifa ya Ubelgiji.

Pierre-Emerick Aubameyang

Pierre-Emerick Aubameyang alikuwa nahodha wa Gabon wakati timu hiyo ilipoifunga timu ya taifa ya Sudan ya kusini kwa jumla ya magoli 3-0.

Mohamed Elneny

Mohamed Elneny alitoa pasi ya mwisho wakati timu ya taifa ya Misri ilipoifunga timu ya taifa ya Swaziland kwa jumla ya magoli 4-1.

David Ospina

David Ospina alicheza dakika zote 90 wakati timu ya taifa ya Colombia ilipoifunga timu ya taifa ya marekani kwa jumla ya magoli 4-2.

Hao ni wachezaji wa Arsenal walioshiriki katika michezo ya kimataifa.

KOSCIELNY AANZA KUCHEZA NA MPIRA & TORREIRA YUPO FITI

Baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutoka na kuwa majeruhi. Nahodha wa Arsenal, Laurent Koscielny ameanza mazoezi ya kucheza na mpira.

 KOSCIELNY AANZA KUCHEZA NA MPIRA & TORREIRA YUPO FITI

Katika ukurasa rasmi wa twitter wa Arsenal, kuliwekwa video inayomuonesha beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa akichezea mpira kwa kupigiana pasi na mchezaji mkongwe wa Arsenal Robert Pires.

Koscienly ambaye jana alitimiza miaka 33 ya kuzaliwa yupo nje ya uwanja kutoka mwazoni mwa mwezi wa tano mwaka huu na kuna taarifa ya kwamba anaweza asicheze hadi mwezi wa 11.

Kuonekana kwa mchezaji huyo kumeibua matumaini mapya kwa mashabiki wa Arsenal , hasa baada ya ukuta wake unaoongozwa na Sokratis na Mustafi kuonekana kuyumba katika mechi zote nne zilizochezwa msimu huu.


Katika taarifa nyingine ni kwamba kiungo wa Arsenal kutoka Uruguay, Lucas Torreira leo alionekana akifanya mazoezi katika viwanja vya London Colney.

Kuonekana huko kwa Lucas kunaendana na taarifa kutoka Uruguay zinazodai ya kwamba mchezaji huyo yupo fiti na tayari kucheza katika mchezo wa jumamosi dhidi ya Newcastle.

Awali kulikuwa na wasiwasi wa kwamba huenda mchezaji huyo ameumia baada ya kutolewa wakati wa mapumziko ijumaa iliyopita wakati timu yake ya taifa ilipoifunga timu ya taifa ya Mexico kwa jumla ya magoli 4-1.

Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Uruguay, Fabian Coito, alisema ya kwamba aliamua kumtoa mchezaji huyo kama njia ya kumlinda ili asipate majeraha kwani anajua ya kwamba yupo kwenye vita vya kuingia katika kikosi cha Arsenal na kuvunja uvumi wa kwamba mchezaji huyo alitolewa kwa sababu ya majeraha.

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery alitumia ukurasa wake wa twitter na kuweka picha za wachezaji waliokuwepo mazoezini leo na kwenye picha hiyo yupo Lucas Torreira.


Arsenal itacheza na Newcastle katika raundi ya tano ya ligi kuu ya Uingeleza jumamosi ijayo.

 

Mechi za kimataifa-Aaron Ramsey afunga

Wakati ligi mbali mbali duniani zikiwa zimesimama kupisha mechi za kimataifa, jana Arsenal iliwakilishwa na wachezaji wawili katika mechi hizo.

Mechi za kimataifa-Aaron Ramsey afunga

Aaron Ramsey

Ramsey aliifungia Wales katika mchezo wa kwanza wa  UEFA Nations League , na kuisaidia timu yake ya taifa kupata ushindi wa jumla ya goli 4-1  dhidi ya timu ya taifa ya jamhuri ya Ireland.

Tom Lawrence aliiandikia Wales goli la kwanza kabla ya mchezaji wa Real Madrid, Gareth Bale kufunga goli la pili.

Dakika chache baadaye  Ramsey alifanikiwa kuingia katika orodha ya wafungaji baada ya kupokea mpira ndani ya enero la hatari la jamhuri ya Ireland na kupiga shuti lililomshinda golikipa Darren Randolph na kujaa wavuni.

Connor Roberts alifunga goli la nne huku Ireland wakipata goli la kufutia machozi lililofungwa na Shaun Williams.Hadi mwisho wa mchezo Wales 4-1 Ireland.

Henrikh Mkhitaryan

Henrikh Mkhitaryan pia alicheza michuano hiyo ya  UEFA Nations League ambapo alicheza katika dakika zote 90 wakati timu yake ya taifa ya Armenia ilipoifunga timu ya taifa ya Liechtenstein kwa jumla ya magoli 2-1.

Marcos Pizzelli aliipatia Armenia goli la kuongoza kabla ya Liechtenstein kusawazisha kupitia kwa  Sandro Wolfinger dakika ya 33.

Mkhitaryan ambaye aliisumbua safu ya ulinzi ya Liechtenstein na alifanikiwa kuipatia nchi yake penati ambayo alipoenda kuipiga alikosa baada ya kupanguliwa na golikipa wa Liechtenstein,Benjamin Buchel.

Armenia waliendelea kulishambulia lango wa wageni hao ambao walikuwa pungufu na katika dakika ya 76 walifanikiwa kupata goli la ushindi lililofungwa na mchezaji aliyeingia katika kipindi cha pili Tigran Barseghyan.

Kuna wachezaji wengine wa Arsenal ambao wanategemewa kuziwakilisha nchi zao katika wiki hizi mbili, tutakuletea habari zao mara tutakapozipata.

 

Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Wakati Arsenal ikimsajili Matteo Guendouzi mwezi wa saba mwaka huu wengi wetu tuliamini ya kwamba kiungo huyo mwenye umri wa mikiaka 19 alikuwa anasajiliwa kwa wakati ujao.

Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Nilitegemea ya kwamba jambo la maana lilikuwa ni kumtoa kwa mkopo timu zinazoshika nafasi za 10-20, ili akacheze katika mazingira yasiyo na ushindani mkubwa wa namba ili apate kuzoea soka la kasi la kiingeleza. Hasa ukizingatia ya kwamba Arsenal ilikuwa inabadilisha kocha na pia kulikuwa na ulazima wa kuanza vizuri hivyo kumtumia mchezaji wa miaka 19 lisingekuwa jambo la busara.

Lakini nakumbuka wakati wa mkutano na waandishi wa habari kocha mkuu wa Arsenal alisema ya kwamba mchezaji huyo alikuwa katika mipango yake kwa msimu huu.Binafsi sikuamini, nilijua ndiyo yale yale makocha wanasema kitu flani na wanafanya kitu tofauti kabisa na walichosema.

Kama utani dogo alicheza vizuri sana katika mechi za kirafiki na baada ya msimu kuanza dogo alionesha kiwango kikubwa tofauti na umri alionao.

Ni kweli alifanya makosa, kutokana na ugeni na pia kukosa uzoefu lakini kwa ujumla amecheza vizuri kuliko wachezaji wengi wakubwa na wazoefu wa Arsenal.

Kiwango chake kiliwafurahisha mashabiki wengi wa Arsenal kiasi cha kumchagua kuwa mchezaji bora wa mwezi wa nane na wasomaji wa tovuti rasmi ya timu arsenal.com

Kwa kweli mchezaji huyo alistahili tuzo hiyo, inatia moyo ya kwamba mchezaji huyo ameanza vizuri maisha yake kama mchezaji wa Arsenal na pia nina imani ya kwamba tuzo hiyo itamfanya mchezaji huyo ajitume zaidi mazoezini na kwenye michezo ya ushindani.

Hongera Matteo Guendouzi.

Eddie Nketiah afanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha Uingeleza

Mshambuliaji kinda wa Arsenal Eddie Nketiah jana aliitwa na kufanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya Uingeleza.

Eddie Nketiah afanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha Uingeleza

Eddie Nketiah akiwa mazoezini na timu ya wakubwa ya Uingeleza

Mshambuliaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga alipata nafasi hiyo baada ya kuwa katika kikosi cha Uingeleza kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ambapo jana alikua benchi wakati wakicheza na vijana wenzao wa Switzerland.

Tangu mwaka jana Eddie amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Arsenal na pia alipata nafasi kadhaa za kucheza katika timu hiyo.

Nketiah ambaye ana asili ya Ghana tayari ameishawakilisha Uingeleza katika timu za vijana wa chini ya umri wa miaka 18, 19 na 21 na mara kwa mara amefanikiwa kufunga bila kujali ni ngazi ipi anacheza.

Mchezaji huyo bado hajaichezea Arsenal katika mchezo wowote wa maana msimu huu lakini hali hiyo inaweza ikabadilika mwezi huu kwani kuna michuano ya Europa ligi na pia kombe la Carabao linaanza hivyo lazima atapewa nafasi ya kuonesha kiwango chake.

 

Reiss Nelson asaini mkataba mpya Arsenal

Kinda wa Arsenal, Reiss Nelson amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na timu hiyo ya kaskazini mwa London.

Reiss Nelson asaini mkataba mpya Arsenal

Nelson ambaye amekuwa ni mchezaji wa Arsenal tangu akiwa na miaka 8, ameshazichezea timu mbalimbali za vijana za Arsenal na anahesabika kama mmoja ya vipaji vikubwa kutoka katika chuo cha soka cha Arsenal kwa miaka ya hivi karibuni.

Nelson alikuwa katika mwaka wa mwisho katika mkataba wake na mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa na wasiwasi wa kwamba angeondoka moja kwa moja, lakini Nelson alimaliza ubishi baada ya kusaini mkataba mpya unaosemekana ya kwamba ni wa miaka mitatu huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi iwapo timu itaona inafaa.

Baada ya kusaini mkataba huo mchezaji huyo  alielekea Ujerumani kujiunga na timu ya  Hoffenheim kwa mkopo wa mwaka mmoja.

 

David Ospina ajiunga na Napoli kwa mkopo

David Ospina ameondoka Arsenal na amejiunga na timu ya Napoli ya Italiakwa mkopo wa mwaka mmoja. Kipa huyo kutoka Colombia anaondoka baada ya kuwasili kwa Berndt Leno kutoka  Bayer Leverkusen, na hivyo kumfanya awe chaguo la tatu la mwalimu Unai Emery.

David Ospina ajiunga na Napoli kwa mkopo

Ospina alijiunga na Arsenal mwaka 2014 akitokea timu ya  OGC Nice ya Ufaransa baada ya kufanya vizuri katika kombe la dunia akiwa na timu yake ya taifa.

Napoli ilikuwa na kipa wa zamani wa Liverpool, Pepe Reina kama golikipa wake wa kwanza kwa misimu mitatu iliyopita lakini kwa sasa mhispania huyo ametimukia katika timu ya AC Milan baada ya aliyekuwa kocha wake Maurizio Sarri kuhamia Chelsea ya Uingeleza.

Kuna tetesi ya kwamba mkataba huo wa mwaka mmoja una dhamani ya paundi milioni moja na kuna kipengele ambacho kitawaruhusu Napoli kumnunua mchezaji huyo kwa paundi milioni 3.

Katika tovuti ramsi ya Arsenal walimtakia kila la heri mchezaji huyo katika timu ya Napoli ambao na wao wana kocha mpya baada ya Sarri kuondoka sasa inanolewa na muitaliano mwingine  Carlo Ancelotti.

Kila la heri David Ospina.

Stephy Mavididi ajiunga na Juventus ya Italia

Mshambuliaji wa Arsenal,Stephy Mavididi  ameihama timu hiyo na kujiunga na mabingwa wa Italia,Juventus.

 Stephy Mavididi wakati akiwa Charlton kwa mkopo

Stephy Mavididi wakati akiwa Charlton kwa mkopo

Mavididi ambaye alishindwa kucheza mchezo wowote na timu ya wakubwa ni zao la chuo cha soka cha Arsenal, na sasa anaenda kujaribu bahati yake kutoka kwa mabingwa hao wa Italia.

“Stephy Mavididi amejiunga na Juventus, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ataanza kwa kukichezea kikosi cha pili cha timu hiyo,” Taarifa fupi katika tovuti rasmi ya Arsenal ilisema.

Mavididi ambaye amewahi kuzichezea timu za Preston, na mara mbili aliichezea timu ya Charlton ambayo aliitumikia katika nusu ya pili ya msimu uliopita, pia ni mchezaji wa kimataifa wa Uingeleza baada ya kuichezea timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

Mchezaji huyo alifunga magoli mawili wakati akiitumikia timu ya Charlton katika ligi daraja la kwanza maarafu kama  Sky Bet League One msimu uliopita.

Kuondoka kwa Mavidi ni muendelezo wa kuondoka kwa wachezaji wengi vijana kutoka katika timu ya Arsenal, Wachezaji wengi ambao iliaminika ya kwamba wana vipaji vikubwa wameshindwa kupata namba katika kikosi chwa kwanza na kuamua kwenda sehemu nyingine kujaribu bahati yao.