KOSCIELNY AANZA KUCHEZA NA MPIRA & TORREIRA YUPO FITI

Baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutoka na kuwa majeruhi. Nahodha wa Arsenal, Laurent Koscielny ameanza mazoezi ya kucheza na mpira.

 KOSCIELNY AANZA KUCHEZA NA MPIRA & TORREIRA YUPO FITI

Katika ukurasa rasmi wa twitter wa Arsenal, kuliwekwa video inayomuonesha beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa akichezea mpira kwa kupigiana pasi na mchezaji mkongwe wa Arsenal Robert Pires.

Koscienly ambaye jana alitimiza miaka 33 ya kuzaliwa yupo nje ya uwanja kutoka mwazoni mwa mwezi wa tano mwaka huu na kuna taarifa ya kwamba anaweza asicheze hadi mwezi wa 11.

Kuonekana kwa mchezaji huyo kumeibua matumaini mapya kwa mashabiki wa Arsenal , hasa baada ya ukuta wake unaoongozwa na Sokratis na Mustafi kuonekana kuyumba katika mechi zote nne zilizochezwa msimu huu.


Katika taarifa nyingine ni kwamba kiungo wa Arsenal kutoka Uruguay, Lucas Torreira leo alionekana akifanya mazoezi katika viwanja vya London Colney.

Kuonekana huko kwa Lucas kunaendana na taarifa kutoka Uruguay zinazodai ya kwamba mchezaji huyo yupo fiti na tayari kucheza katika mchezo wa jumamosi dhidi ya Newcastle.

Awali kulikuwa na wasiwasi wa kwamba huenda mchezaji huyo ameumia baada ya kutolewa wakati wa mapumziko ijumaa iliyopita wakati timu yake ya taifa ilipoifunga timu ya taifa ya Mexico kwa jumla ya magoli 4-1.

Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Uruguay, Fabian Coito, alisema ya kwamba aliamua kumtoa mchezaji huyo kama njia ya kumlinda ili asipate majeraha kwani anajua ya kwamba yupo kwenye vita vya kuingia katika kikosi cha Arsenal na kuvunja uvumi wa kwamba mchezaji huyo alitolewa kwa sababu ya majeraha.

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery alitumia ukurasa wake wa twitter na kuweka picha za wachezaji waliokuwepo mazoezini leo na kwenye picha hiyo yupo Lucas Torreira.


Arsenal itacheza na Newcastle katika raundi ya tano ya ligi kuu ya Uingeleza jumamosi ijayo.

 

Mechi za kimataifa-Aaron Ramsey afunga

Wakati ligi mbali mbali duniani zikiwa zimesimama kupisha mechi za kimataifa, jana Arsenal iliwakilishwa na wachezaji wawili katika mechi hizo.

Mechi za kimataifa-Aaron Ramsey afunga

Aaron Ramsey

Ramsey aliifungia Wales katika mchezo wa kwanza wa  UEFA Nations League , na kuisaidia timu yake ya taifa kupata ushindi wa jumla ya goli 4-1  dhidi ya timu ya taifa ya jamhuri ya Ireland.

Tom Lawrence aliiandikia Wales goli la kwanza kabla ya mchezaji wa Real Madrid, Gareth Bale kufunga goli la pili.

Dakika chache baadaye  Ramsey alifanikiwa kuingia katika orodha ya wafungaji baada ya kupokea mpira ndani ya enero la hatari la jamhuri ya Ireland na kupiga shuti lililomshinda golikipa Darren Randolph na kujaa wavuni.

Connor Roberts alifunga goli la nne huku Ireland wakipata goli la kufutia machozi lililofungwa na Shaun Williams.Hadi mwisho wa mchezo Wales 4-1 Ireland.

Henrikh Mkhitaryan

Henrikh Mkhitaryan pia alicheza michuano hiyo ya  UEFA Nations League ambapo alicheza katika dakika zote 90 wakati timu yake ya taifa ya Armenia ilipoifunga timu ya taifa ya Liechtenstein kwa jumla ya magoli 2-1.

Marcos Pizzelli aliipatia Armenia goli la kuongoza kabla ya Liechtenstein kusawazisha kupitia kwa  Sandro Wolfinger dakika ya 33.

Mkhitaryan ambaye aliisumbua safu ya ulinzi ya Liechtenstein na alifanikiwa kuipatia nchi yake penati ambayo alipoenda kuipiga alikosa baada ya kupanguliwa na golikipa wa Liechtenstein,Benjamin Buchel.

Armenia waliendelea kulishambulia lango wa wageni hao ambao walikuwa pungufu na katika dakika ya 76 walifanikiwa kupata goli la ushindi lililofungwa na mchezaji aliyeingia katika kipindi cha pili Tigran Barseghyan.

Kuna wachezaji wengine wa Arsenal ambao wanategemewa kuziwakilisha nchi zao katika wiki hizi mbili, tutakuletea habari zao mara tutakapozipata.

 

Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Wakati Arsenal ikimsajili Matteo Guendouzi mwezi wa saba mwaka huu wengi wetu tuliamini ya kwamba kiungo huyo mwenye umri wa mikiaka 19 alikuwa anasajiliwa kwa wakati ujao.

Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Nilitegemea ya kwamba jambo la maana lilikuwa ni kumtoa kwa mkopo timu zinazoshika nafasi za 10-20, ili akacheze katika mazingira yasiyo na ushindani mkubwa wa namba ili apate kuzoea soka la kasi la kiingeleza. Hasa ukizingatia ya kwamba Arsenal ilikuwa inabadilisha kocha na pia kulikuwa na ulazima wa kuanza vizuri hivyo kumtumia mchezaji wa miaka 19 lisingekuwa jambo la busara.

Lakini nakumbuka wakati wa mkutano na waandishi wa habari kocha mkuu wa Arsenal alisema ya kwamba mchezaji huyo alikuwa katika mipango yake kwa msimu huu.Binafsi sikuamini, nilijua ndiyo yale yale makocha wanasema kitu flani na wanafanya kitu tofauti kabisa na walichosema.

Kama utani dogo alicheza vizuri sana katika mechi za kirafiki na baada ya msimu kuanza dogo alionesha kiwango kikubwa tofauti na umri alionao.

Ni kweli alifanya makosa, kutokana na ugeni na pia kukosa uzoefu lakini kwa ujumla amecheza vizuri kuliko wachezaji wengi wakubwa na wazoefu wa Arsenal.

Kiwango chake kiliwafurahisha mashabiki wengi wa Arsenal kiasi cha kumchagua kuwa mchezaji bora wa mwezi wa nane na wasomaji wa tovuti rasmi ya timu arsenal.com

Kwa kweli mchezaji huyo alistahili tuzo hiyo, inatia moyo ya kwamba mchezaji huyo ameanza vizuri maisha yake kama mchezaji wa Arsenal na pia nina imani ya kwamba tuzo hiyo itamfanya mchezaji huyo ajitume zaidi mazoezini na kwenye michezo ya ushindani.

Hongera Matteo Guendouzi.

Eddie Nketiah afanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha Uingeleza

Mshambuliaji kinda wa Arsenal Eddie Nketiah jana aliitwa na kufanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya Uingeleza.

Eddie Nketiah afanya mazoezi na kikosi cha wakubwa cha Uingeleza

Eddie Nketiah akiwa mazoezini na timu ya wakubwa ya Uingeleza

Mshambuliaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga alipata nafasi hiyo baada ya kuwa katika kikosi cha Uingeleza kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ambapo jana alikua benchi wakati wakicheza na vijana wenzao wa Switzerland.

Tangu mwaka jana Eddie amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Arsenal na pia alipata nafasi kadhaa za kucheza katika timu hiyo.

Nketiah ambaye ana asili ya Ghana tayari ameishawakilisha Uingeleza katika timu za vijana wa chini ya umri wa miaka 18, 19 na 21 na mara kwa mara amefanikiwa kufunga bila kujali ni ngazi ipi anacheza.

Mchezaji huyo bado hajaichezea Arsenal katika mchezo wowote wa maana msimu huu lakini hali hiyo inaweza ikabadilika mwezi huu kwani kuna michuano ya Europa ligi na pia kombe la Carabao linaanza hivyo lazima atapewa nafasi ya kuonesha kiwango chake.

 

Reiss Nelson asaini mkataba mpya Arsenal

Kinda wa Arsenal, Reiss Nelson amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na timu hiyo ya kaskazini mwa London.

Reiss Nelson asaini mkataba mpya Arsenal

Nelson ambaye amekuwa ni mchezaji wa Arsenal tangu akiwa na miaka 8, ameshazichezea timu mbalimbali za vijana za Arsenal na anahesabika kama mmoja ya vipaji vikubwa kutoka katika chuo cha soka cha Arsenal kwa miaka ya hivi karibuni.

Nelson alikuwa katika mwaka wa mwisho katika mkataba wake na mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa na wasiwasi wa kwamba angeondoka moja kwa moja, lakini Nelson alimaliza ubishi baada ya kusaini mkataba mpya unaosemekana ya kwamba ni wa miaka mitatu huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi iwapo timu itaona inafaa.

Baada ya kusaini mkataba huo mchezaji huyo  alielekea Ujerumani kujiunga na timu ya  Hoffenheim kwa mkopo wa mwaka mmoja.

 

David Ospina ajiunga na Napoli kwa mkopo

David Ospina ameondoka Arsenal na amejiunga na timu ya Napoli ya Italiakwa mkopo wa mwaka mmoja. Kipa huyo kutoka Colombia anaondoka baada ya kuwasili kwa Berndt Leno kutoka  Bayer Leverkusen, na hivyo kumfanya awe chaguo la tatu la mwalimu Unai Emery.

David Ospina ajiunga na Napoli kwa mkopo

Ospina alijiunga na Arsenal mwaka 2014 akitokea timu ya  OGC Nice ya Ufaransa baada ya kufanya vizuri katika kombe la dunia akiwa na timu yake ya taifa.

Napoli ilikuwa na kipa wa zamani wa Liverpool, Pepe Reina kama golikipa wake wa kwanza kwa misimu mitatu iliyopita lakini kwa sasa mhispania huyo ametimukia katika timu ya AC Milan baada ya aliyekuwa kocha wake Maurizio Sarri kuhamia Chelsea ya Uingeleza.

Kuna tetesi ya kwamba mkataba huo wa mwaka mmoja una dhamani ya paundi milioni moja na kuna kipengele ambacho kitawaruhusu Napoli kumnunua mchezaji huyo kwa paundi milioni 3.

Katika tovuti ramsi ya Arsenal walimtakia kila la heri mchezaji huyo katika timu ya Napoli ambao na wao wana kocha mpya baada ya Sarri kuondoka sasa inanolewa na muitaliano mwingine  Carlo Ancelotti.

Kila la heri David Ospina.

Stephy Mavididi ajiunga na Juventus ya Italia

Mshambuliaji wa Arsenal,Stephy Mavididi  ameihama timu hiyo na kujiunga na mabingwa wa Italia,Juventus.

 Stephy Mavididi wakati akiwa Charlton kwa mkopo

Stephy Mavididi wakati akiwa Charlton kwa mkopo

Mavididi ambaye alishindwa kucheza mchezo wowote na timu ya wakubwa ni zao la chuo cha soka cha Arsenal, na sasa anaenda kujaribu bahati yake kutoka kwa mabingwa hao wa Italia.

“Stephy Mavididi amejiunga na Juventus, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ataanza kwa kukichezea kikosi cha pili cha timu hiyo,” Taarifa fupi katika tovuti rasmi ya Arsenal ilisema.

Mavididi ambaye amewahi kuzichezea timu za Preston, na mara mbili aliichezea timu ya Charlton ambayo aliitumikia katika nusu ya pili ya msimu uliopita, pia ni mchezaji wa kimataifa wa Uingeleza baada ya kuichezea timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

Mchezaji huyo alifunga magoli mawili wakati akiitumikia timu ya Charlton katika ligi daraja la kwanza maarafu kama  Sky Bet League One msimu uliopita.

Kuondoka kwa Mavidi ni muendelezo wa kuondoka kwa wachezaji wengi vijana kutoka katika timu ya Arsenal, Wachezaji wengi ambao iliaminika ya kwamba wana vipaji vikubwa wameshindwa kupata namba katika kikosi chwa kwanza na kuamua kwenda sehemu nyingine kujaribu bahati yao.

Unai Emery atangaza manahodha watano wa Arsenal

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery ametangaza wachezaji watano ambao watakuwa manahodha wa Arsenal katika msimu huu.

Unai Emery atangaza manahodha watano wa Arsenal

Petr Cech kuvaa kitambaa jumapili dhidi ya Manchester City

Katika habari iliyoandikwa na mtandao wa telegraph  inadaiwa ya kwamba kocha huyo ameamua kumuacha Laurent Koscienly kama nahodha mkuu wa timu hiyo huku akisaidia wa Petr Cech, Aaron Ramsey,Mesut Özil na Granit Xhaka.

Mapema baada ya kuteuliwa, kocha huyo alitangaza ya kwamba alikuwa na nia ya kuteua wachezaji watano ambao wangekuwa viongozi wa timu uwanjani na inaelekea ametimiza nia yake hiyo.

Pia taarifa hiyo inaendelea kuelezea ya kwamba golikipa wa Arsenal Petr Cech ndiye atakayevaa kitambaa cha Unahodha jumapili wakati Arsenal itakapocheza na Manchester City.

Kama taarifa hizo ni za kweli ina maana Cech ataanza golini na golikipa mpya Bernd Leno ataanza kama mchezaji wa akiba.

Je unasemaje kuhusu uteuzi huu? tupia maoni yako hapa chini.

Tetesi-Reiss Nelson akubali mkataba mpya wa miaka mitano

Mchezaji kinda wa Arsenal,Reiss Nelson inasemekana amepewa mkataba mpya wa muda mrefu huku akiongezewa mshahara.

Tetesi-Reiss Nelson akubali mkataba mpya wa miaka mitano

Katika taarifa tulizopata muda mchache uliopita ni kwamba Nelson amepewa mkataba huo mpya baada ya kuonesha kiwango kizuri katika michezo ya kirafiki ambapo alifunga magoli mawili na kusaidia kupatikana mengine matatu.

Mara baada ya kuibuka kwa habari hizo mashabiki wengi wa Arsenal mitandaoni walionekana kuzifurahia kwani kulikuwa na wasiwasi wa kwamba angetataa mkataba mpya ili aende timu ambayo itampatia nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

Hivyo inaonekana ya kwamba kocha Unai Emery amekikubali kiwango cha mchezaji huyo na amefanikiwa kumshawishi mchezaji huyo ili abaki katika kikosi cha Arsenal.

Wakati huo huo kuna tetesi za kwamba kocha Unai amemwambia Danny Welbeck ya kwamba hana nafasi katika kikosi cha kwanza na anaweza asipate nafasi ya kucheza michezo mingi na hivyo ameruhusiwa kutafuta timu.

Pia kuna tetesi za kwamba Lucas Perez ameuzwa West Ham kwa dau la paundi milioni 10.

Ni wazi ya kwamba benchi ya ufundi la Arsenal linajaribu kupunguza wachezaji hasa kwenye nafasi za viungo wa pembeni ili kuwapa nafasi vijana kama Nelson na Eddie Nketiah.

Pia inawezekana ya kwamba Arsenal wapo njiani kusajili winga mwingine.

Bado siku tatu tu tupate jibu kamili.

Joao Virginia ajiunga na Everton

Arsenal imeendelea kusafisha kikosi chake baada ya golikipa wa timu ya vijana Joao Virginia kukamilisha usajili na kujiunga na timu ya Everton inayoshiriki ligi kuu ya Uingeleza.

Joao Virginia ajiunga na Everton

Habari za kuhama kwa Joao Virginia zimewaacha kwa mshangao mashabiki wengi wa Arsenal wanaofuatilia timu za vijana kwani alikuwa ni mmoja ya wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu katika kikosi hicho na hakuna aliyetegemea ya kwamba atahama moja kwa moja.

Joao Virginia,mwenye umri wa miaka 18, alishinda kombe la Euro 2018 kwa timu za vijana akiwa na timu ya taifa ya vijana ya Ureno jumapili iliyopita.

Katika taarifa rasmi ya tovuti ya Arsenal, hawajaelezea dau la uhamisho la mchezaji huyo, ila wamemtakia kila la heri katika timu yake mpya.

Labda kuuzwa kwa mchezaji huyo ni dalili za kwamba Arsenal inajaribu kukusanya pesa kwa ajili ya mchezaji mpya, tusubiri tuone.

Alex Iwobi asaini mkataba mpya wa muda mrefu ili kubaki Arsenal

Alex Iwobi amesaini mkataba mpya na wa muda mrefu ili kuendelea kuichezea Arsenal.Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ni mhitimu wa chuo cha soka cha Arsenal cha Hale End na amekuwa katika timu tangu akiwa na miaka 9.

Alex Iwobi asaini mkataba mpya wa muda mrefu ili kubaki Arsenal

Iwobi ambaye ameishaichezea Arsenal katika michezo 98 ndani ya miaka mitatu na ameshafunga magoli nane.

Mkataba huo wa Alex Iwobi ambaye ni Mnigeria umekuja siku ambayo rafiki yake mkubwa Chuba Akpom ambaye pia ana asili na Nigeria kuhama Arsenal na kujiunga na PAOK.

Baada ya kusaini mkataba huo wa muda mrefu Iwobi alisema.

“Siku zote imekuwa ndoto zangu kuiwakilisha Arsenal tangu nikiwa mtoto.Nina furaha kubwa kuongeza mkataba na ninategemea kufanya vizuri ili kuwafurahisha mashabiki wa Arsenal na familia yangu”

Iwobi anaweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Arseanal kutokana na timu kukosa mawinga halisi.

Kocha mkuu wa Arsenal, Unai Emery anaamini ya kwamba Iwobi ana kipaji kikubwa na ni sehemu ya mipango yake kwa msimu ujao.