Hakuna haja ya mashabiki wa Arsenal kupaniki

Baada ya Arsenal kufungwa na Southampton sikuweza kuingia mtandaoni au kuandika chochote katika ukurasa huu kutokana na kuwa na majukumu mengine.

Hakuna haja ya mashabiki wa Arsenal kupaniki

Jana usiku niliingia katika mitandao ya kijamii na kuona ya kwamba mashabiki wa Arsenal wakianza mchezo wa kumtafuta mchawi kutokana na Arsenal kupoteza mchezo huo.

Kuna wengine wanamnyooshea vidole kocha mkuu, Unai Emery kwa kupanga timu vibaya, wengine wanadai timu ilipoteza kwa kuwa Laurent Koscienly alicheza kama beki wa kati, wengine wanadai Mesut Özil ndiye tatizo, cha msingi ni kwamba asilimia kubwa ya mashabiki wameshapata mtu wa kumtupia lawama.

Huwezi ukamlaumu Unai Emery kwa kupoteza mchezo ule, ni msimu wake wa kwanza Arsenal, baada ya kufungwa michezo miwili ya mwanzo aliiongoza Arsenal kucheza michezo 22 bila ya kufungwa, Mustafi na Sokratis walikuwa wamefungiwa, Kolasinac majeruhi, Bellerin aliumia mapema, na zaidi ya yote Rob Holding ambaye kwa mtazamo wangu ndiye beki wa kati bora wa Arsenal kwa sasa ni majeruhi hadi mwisho wa msimu.

Mwalimu alikuwa na wakati mgumu na alijitahidi kuipanga timu aliyoweza.

Kwa upande wa wachezaji, kama binadamu wanaweza kuwa na siku mbaya, kila mchezaji ana mapungufu yake, lakini hicho sio kigezo cha kuwatukana na kuwazomea.

Nimeona mtu kaposti eti Koscienly auzwe kwa sababu kaisha na kuwa beki mbovu, hiki ndicho nilichomjibu, Koscienly aliumia mguu akiiteteza Arsenal, alikuwa akicheza akiwa na maumivu ya mguu lakini kutokana na Arsenal kutokuwa na mabeki katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid,Arsene Wenger alimuomba acheze , akaamua kucheza na bahati mbaya aliumia na kupoteza ndoto yake ya kucheza kombe la dunia.

Emery amekuwa na Arsenal katika dirisha moja tu la usajili, anatakiwa apewe muda ili ajuwe ni mchezaji gani atamuamini na nani atamuacha pia wachezaji wanatakiwa wapewe muda wa kujifunza ni nini mwalimu anataka, haya mambo hayawezi kufanyika katika miezi 6.Jurgen Klop alimaliza nafasi ya nane katika msimu wake wa kwanza, Pep Guardiola hakubeba hata kombe moja katika msimu wake wa kwanza.

Wahenga walisema ya kwamba kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi na mimi naamini ya kwamba kufungwa na Southampton sio mwisho wa Arsenal na bado naamini itamaliza ndani ya nne bora.

Wito wangu kwa mashabiki wa Arsenal, tulieni kocha Unai Emery anajua anachokifanya, baada ya misimu miwili mtanona matunda yake.

Leo tunacheza dhidi ya Totenham Hotspurs katika robo fainali ya kombe la Carabao, #COYG

 

Speak Your Mind

*