Kwa nini Arsenal haitasajili mchezaji yeyote wa maana dirisha hili la usajili

Kwanza kabisa ningependa kuwatakia heri ya mwaka mpya kwa mashabiki wote wa Arsenal na wasomaji wetu kwa ujumla.

Kwa nini Arsenal haitasajili mchezaji yeyote wa maana dirisha hili la usajili

Leo ikiwa tarehe moja ya mwezi kwa kwanza, ina maana ya kwamba dirisha dogo la usajili limefunguliwa na timu mbali mbali zinaanza kutafuta wachezaji wapya kwa ajili ya kujiimalisha.

Kwa upande wa timu ya Arsenal ni kwamba mashabiki wengi wamekuwa na kiu ya kuona timu yao ikisajili wachezaji katika baadhi ya nafasi kama beki wa kati, beki wa kushoto na winga, ingawa mimi ninaamini ya kwamba Arsenal haitasajili mchezaji yeyote wa maana katika dirisha hili na baadaye kidogo nitakuambia kwa nini.

Jana mwandishi wa BBC, David Ornstein aliandika makala ndefu sana kuhusu sakata la Aaron Ramsey na usajili wa Arsenal na baada ya kuisoma makala ile ninaamini ya kwamba tusitegemee usajili mpya katika dirisha hili.

Ornstein anaanza kwa kusema ya kwamba Aaron Ramsi leo ataanza rasmi mazungumzo na timu za Juventus, Bayern, Inter, PSG, na Real Madrid kuhusu kuhamia moja ya timu hizo mara baada ya mkataba wake kumalizika tarehe 30 ya mwezi wa sita mwaka huu.

Juventus ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kumsajili Ramsey kutokana na kwamba mchezaji wao wa kiungo Sami Khedira amekuwa akicheza chini ya kiwango msimu huu na pia umri umeanza kumtupa mkono (anatimiza miaka 32 mwaka huu).

Pia wanaamini ya kwamba uwepo wa Szczesny katika kikosi chao unaweza ukawa kivutio cha Ramsey kuichagua timu hiyo ya Italia.

Aaron Ramsey ni mmoja ya wachezaji wanaowagawanya mashabiki wa Arsenal, kuna wale wanaoamini ya kwamba mchezaji huyo ni mmoja ya wachezaji muhimu kabisa katika kikosi hicho na anastahili kulipwa mshahara mkubwa, huku wengine wakiamini ni mchezaji asiyejielewa uwanjani na bora aondoke, lakini ukiangalia orodha za timu zinazomtaka unaweza kujua upande upi upo sahihi.

Sakata la usajili wa Aaron Ramsey linaonesha ni kwa kiasi gani timu ya Arsenal inavyoendeshwa vibaya.

Katika makala hiyo ambayo ukiisoma kwa makini inaonekana ya kwamba alifanya mahojiano na mmoja ya viongozi wa juu wa Arsenal inaweka wazi ya kwamba Arsenal haitegemea kuuza mchezaji yeyote na pia hawana pesa za kutosha za kununua wachezaji katika dirisha hili la usajili.

Usajili wowote wa kudumu, ada kwa ajili ya mikopo ya wachezaji na mishahara yao itatokana na bajeti ndogo ambayo timu imetenga kuitumia katika kipindi hiki cha usajili, hivyo mategemeo ya kumpata mchezaji mpya ni madogo labda aje kwa mkopo.

Mchezaji ambaye Arsenal wanamuangalia kwa sasa ni kiungo wa Barcelona, Denis Suarez mwenye umri wa miaka 24.

Huo ndio ukweli, usitegemee usajili wowote katika dirisha hili la usajili, Arsenal haikumchagua Unai Emery kama kocha wa Arsenal ili wampatie pesa za kununulia wachezaji.

Yupo kwenye timu ili akuze vipaji vya wachezaji ili badaye wauzwe na kuiingizia timu faida kubwa au kama Ornstein alivyoandika: “Emery atapewa muda wa kufundisha mfumo wake na kukitengeneza kikosi kutokana na muono wake, atapewa madirisha kadhaa ya usajili ili aweze kutimiza nia hiyo kama Liverpoo walivyoendeleza kikosi chao tangu Jurgen Klop alipowasili katika timu hiyo mwezi wa 10 mwaka 2015.”

Kwa hiyo mashabiki wenzangu wa Arsenal kazeni mikanda, anzeni kuzoea.

Ukitaka kusoma kwa undani zaidi makala hiyo utaikuta katika ukurasa wa BBCsports: https://www.bbc.com/sport/football/46722051

Sasa baada ya kuipitia makala hiyo ya BBC nikakumbuka makala nyingine iliyoandikwa na kikundi cha mashabiki wa Arsenal cha  AST (Arsenal Supporter’s Trust) mwishoni mwa mwaka jana ambayo ilikuwa inaelezea hali ya uchumi ndania ya timu ya Arsenal.

kwa wanaopenda kusoma link hii hapa: https://www.arsenaltrust.org/news/2017/arsenals-financial-position-for-201718-assessed

Kwa kifupi jamaa wa AST wanakadiria ya kwamba Arsenal ilipata faida ya paundi milioni 70 katika msimu uliopita (2017/2018 au msimu wa mwisho wa Arsene Wenger).

Hivyo pesa hiyo itaongezea pesa ya akiba ambayo Arsenal inayo ambayo ni paundi milioni 200, lakini ikumbukwe ya kwamba sehemu ya pesa hiyo haiwezi kutumika kwani ni sehemu ya makubaliano ya deni la uwanja, ambalo ni paundi milioni 20.

Hii faida ilitokana na kuuzwa kwa wachezaji, ikumbukwe ya kwamba Arsenal inatumia mfumo uitwao Amortization ( waliosoma uhasimu wanajua namaanisha nini ila kwa wale ambao hawajasomea uhasimu nitajaribu kuelezea), unapouza mchezaji unaandika pesa yote kwenye kitabu chako cha hesabu ya mapato na matumizi lakini unaponunua mchezaji pesa inatoka kwa mafungu ( kwa kiswahili rahisi Arsenal inanunua wachezaji kwa mafungu, mfano Lucas Torreira alinunuliwa kwa paundi milioni 27 lakini hazikulipwa zote, zililipwa paundi milioni 9 wakati wa ununuzi, zitalipwa zingine 9 mwezi wa saba 2019 na tisa za mwisho zinalipwa mwakani 2020, hivyo Arsenal kwenye vitabu vyake ilitoa paundi milioni 9 tu, ndiyo maana ilipata faida).

Pesa ya mauzo ilikuja baada ya kuwauza akina Ox, Giroud na Theo Walcott, hivyo Arsenal isingeuza wachezaji ingeingia hasara ya paundi milioni 44.

Hasar hiyo ilitokana na timu kushindwa kufudhu kucheza katika ligi ya mabingwa ( timu zinashoshiriki makundi hupewa paundi milioni 30) na pia kukosa pesa ya matangazo, wadhamini na mauzo ya tiketi katika michuano hiyo.

Ili kufudia pengo hilo Arsenal ililazimika kuwauza baadhi ya nyota wake. Pamoja na kwamba kuuza wachezaji kunaleta pesa lakini huu sio mfumo bora wa kuunda timu bora na ya ushindani na viongozi wa Arsenal wanalijua hili.

Kitu kingine walichoandika AST ni kwamba Arsenal inategemea kupata hasara ya kati ya paundi £60-70m mwishoni mwa msimu huu, hiyo ni kama Arsenal haitasajili mchezaji yeyote, ikitokea ikafanya usajili hasara inaweza ikawa kubwa zaidi.

Hiyo ndiyo sababu kubwa kwa nini Arsenal haitafanya usajili katika majira haya ya baridi.

Kwani faida iliyopatikana mwaka jana ndiyo iliyotumika kununulia wachezaji katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi na pesa hizo zimeisha.

Lakini tutajua zaidi wakati Arsenal itakapotoa ripoti ya mapato na matumizi mwezi wa pili mwaka huu.

Ukisoma ripoti ya BBC utaona ya kwamba Arsenal itaongeza pesa za usajili katika dirisha kubwa la usajili hii ni kwa sababu katika muda huo pesa za udhamini za Adidas zitakuwa zimeingia,pesa za mishahara ya mwachezaji wanaoodoka, na pia pesa za matangazo ya vituo vya luninga na kama Arsenal itafanikiwa kuingia katika ligi ya mabingwa wa Ulaya pesa itaongezeka zaidi.

Hii ni kwa mara ya kwanza ndani ya miaka zaidi ya 20 Arsenal inajiendesha kwa hasara na kama itashindwa kujifufua kiuchumi kuna uwezekano mkubwa wa kwamba tukaona mastaa wakiuzwa na kuletwa makinda ili timu iweze kujiendesha.

Baada ya kusoma hayo nikajiuliza kwa nini Kroenke asitoe pesa mfukoni mwake na kusaidia usajili, baada ya kufanya uchunguzi nikaona ni sababu kuu tatu.

Moja ni kwamba Arsenal ni timu inayojiendesha kwa kutumia mapato yake yenyewe na hicho kimekuwa kivutio kikubwa kwa wadhamini na wawezekaji, akiweka pesa atakua ameondoa kivutio hicho.

Mbili, sheria za ligi kuu ya Uingeleza inazitaka timu za ligi kuu ya Uingeleza zisiongeze zaidi ya paundi milioni 7 katika bajeti yake ya mishahara, zinaweza kuongeza zaidi iwapo zitauza wachezaji ama zitapata faida, Arsenal inajiendesha kwa hasara hivyo hawezi kufanya hivyo.

Tatu,shirikisho la soka la Ulaya linazitaka timu kujiendesha kwa kutumia mapato yao na sio kutegemea pesa kutoka nje, ndiyo maana Machester City na PSG kila mwaka wako kwenye matatizo na shirikisho hilo, sidhani kama Kroenke anaweza kuweka pesa na kuvunja hiyo sheria.

Lengo langu sio kuwakatisha tamaa mashabiki wa Arsenal, au kuwaharibia sherehe zenu za mwaka mpya , lengo langu kuu ni kuwaambia ukweli kwa nini Arsenal haitasajili mchezaji yeyote wa maana katika dirisha hili la usajili, labda awe kinda au mchezaji wa mkopo, ili ikitokea haujafanyika usajili watu wasipaniki na kuanza kutukana kwenye mitandao.

Pia kumbukeni ya kwamba Arsenal inajiendesha kwa hasara kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 20, miezi 6 tu baada ya Arsene Wenger kuondoka, unaamini ni bahati mbaya? Mimi sina jibu, mwaka mpya mwema.

#COYG

 

Speak Your Mind

*