Rasmi Sven Mislintat kuondoka Arsenal

Timu ya Arsenal imetangaza ya kwamba mjerumani Sven Mislintat ataondoka tarehe nane ya mwezi ujao baada ya kuitumikia Arsenal kwa miezi 14 tu.

Rasmi Sven Mislintat kuondoka Arsenal

Katika taarifa rasmi katika tofuti ya Arsenal, hawakuweka wazi sababu za Sven Mislintat kuondoka licha ya kuandika ujumbe mfupi wa kumshukuru kwa kazi yake kubwa na kumtakia mafanikio huko aendako.

Mislintat ambaye anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kutafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa na kuweza kuwasajili kwa bei rahisi kiasi cha kupewa jina la utani la jicho la dhahabu.

Akiwa Arsenal aliweza kusaidia kupatikana kwa wachezaji ambao walikuwa hawajulikani kama Matteo Guendouzi na Mavporanos, pia inasemekana yeye ndiye aliyefanikiwa mpango wa kuwasajili wachezaji Pierre Emerick Aubamayang, Henrik Mkhitryan na Papa Sokratis.

Wakati akiajiliwa na Arsenal mnano tarehe moja ya mwezi wa 12 mwaka 2017 alionekana ya kwamba alikuwa mtu sahihi ambaye angeweza kuisaidia Arsenal kuvumbua vipaji hasa katika kipindi hiki ambacho timu haina pesa.

Pamoja na timu kutokuweka wazi sababu za kuondoka kwa Sven, mitandaoni kila mtu anajaribu kuweka sababu ambazo anaamini ndizo zilizosababisha kuondoka kwa Sven Mislintat.

Kutokupewa chezo cha mkurugenzi wa soka

Arsenal ipo mbioni kumteua mkurugenzi wa soka na taarifa tulizonazo ni kwamba bodi ya Arsenal inataka kumteua mtu ambaye ana uhusiano na Arsenal (mchezaji wa zamani) au mtu ambaye ana uhusiano mzuri na kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery.

Taarifa kutoka Brazil zinadai ya kwamba tayari Arsenal imeshawasiliana na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Mbrazil Edu ili achukue nafasi hiyo, ikumbukwe ya kwamba Edu ndiye mkurugenzi wa soka wa shirikisho la soka la Brazil, pia kuna taarifa za kwamba iwapo Edu atakataa nafasi hiyo atapewa winga wa zamani wa Arsenal, Marc Overmars ambaye ana cheo kama hicho katika timu ya Ajax Armsterdam.

Taarifa hizo zinaendelea kudai ya kwamba Sven alitegemea ya kwamba yeye ndiye ambaye angepewa cheo hicho na uamuzi wa bodi wa kutafuta mtu mwingine umemuuzi na ameamua kuachana na Arsenal kwani wanaonesha ya kwamba hawaudhamini mchango wake.

Kukosana na Emery na Raul

Baada ya kuondoka Wenger, Ivan Gazidis ndiye aliyekuwa mwamuzi wa mwisho kuhusu usajili wa Arsenal, na baadaye Gazidis naye akaondoka na rungu hilo likaangukia mikononi mwa mhispania Raul Sahleli.

Taarifa zilizopo ni kwamba wawili hao wanapishana aina ya wachezaji wanaotaka kuwasajili Arsenal, wakati Sven yeye anaamini sana katika namba za wachezaji ( magoli wanayofunga, asisti, dakika wanazokimbia nk) , Raul yeye anaamini sana katika mtandao alionao ndani na nje ya ulaya unaomuwezesha kupata wachezaji wengi.

Kuna taarifa za kwamba Sven alipinga usajili wa Denis Suarez, wakati Raul na Unai wanamtaka mchezaji huyo, ameona ya kwamba wachezaji anaowataka hawasajiliwi na Arsenal hivyo ameona ya kwamba bora aondoke.

 

Arsena kukosa pesa za usajili

Hili nililiona katika mtandao wa Reddit ambapo kuna jamaa anadai ya kwamba baada ya kukaa na Arsenal mwaka mmoja Sven hajarizishwa na uendeshwaji wa Arsenal na haoni kama ni timu yenye uelekeo mzuri na suala la timu kukosa pesa la usajili limemlazimisha kuondoka kwani anaamini hata akitafuta wachezaji wazuri Arsenal haiwezi kuwasajili.

Binafsi sijui sababu ipi kati ya hizo tatu ni ya kweli, ila nauheshimu uamuzi wake na kumtakia kila la heri aendako.

 

Per Mertesacker aanza kazi Arsenal

Per Mertesacker ameanza kazi rasmi kama meneja wa chuo cha soka cha arsenal baada ya kuishuudia timu ya Arsenal ya vijana wenye umri wa miaka 18 ikicheza na Chelsea jumamosi iliyopita.

Baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo mwanzoni kwa mwaka huu. Mertesacker ambaye alistaafu kuichezea Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita alichukua likizo ya miezi miwili kabla ya kuanza rasmi kazi ya kuwanoa madogo hao.

Juzi ukurasa rasmi wa twitter wa Arsenal ulithibitisha ya kwamba nahodha huyo mstaafu amerudi na yupo tayari kufanya kazi ambapo waliweka picha akiwa katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea wa Cobham akiwaangalia watoto hao walipopambana na watoto wenzao wa Chelsea.


Katika mchezo huo vijana wao wa Arsenal walipoteza mchezo huo kwa jumla ya goli 3-1.

Katika miaka ya karibuni chuo cha soka cha Arsenal kimejitahidi kutoa wachezaji vijana ambao wametumika katika kikosi cha kwanza.

Hector Bellerin na Alex Iwobi wanacheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, wachezaji kama Eddie Nketiah, Reiss Nelson na Ainsley Maitland-Niles walipata nafasi ya kucheza katika timu ya wakubwa msimu uliopita.

Kazi kubwa ya Per Metersacker na jopo la makocha katika chuo cha soka cha HALE END itakuwa ni kuzalsiha wachezaji wengi zaidi wataotumika katika kikosi cha kwanza katika miaka mingi ijayo.

 

Patrick Vieira adhibitisha kuongea na Arsenal

Kiungo na nahodha wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira, amedhibitisha ya kwamba alifanya mazungumzo na Arsenal juu ya Uwezekano wa kuchukua mikoba ya Arsene Wenger na kuwa kocha mkuu wa Arsenal.

Patrick Vieira adhibitisha kuongea na Arsenal

Vieira, ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya  New York City FC  inayoshiriki ligi ya soka ya Marekani MLS, alikuwa ni moja ya watu waliokuwa wanahusishwa na kuwa makocha wa Arsenal kabla ya Arsenal kuamua kumchagua Unai Emery kuwa kocha mkuu.

Lakini, Vieira anadai ya kwamba mazungumzo wa mabosi wa Arsenal yalikuwa ni mafupi na hayakuendelea zaidi ya hapo kwani timu iliamua kuangalia makocha wengine.

“Wakurugenzi wa Arsenal walikutana na nilifanya nao mazungumzo, lakini hakukua na maendeleo zaidi , Vieira aliuambia mtandao wa  The Times.

Sababu kubwa ya Vieira kutopewa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa Arsenal ni kwamba ana mtazamo wa soka tofauti na wakurugenzi wa Arsenal na ndiyo maana wakaamua kuachana naye na kumchukua Unai Emery.

Vieira aliichezea Arsenal zaidi ya michezo  400 kati ya mwaka 1996 na 2005, akiiongoza timu kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingeleza mara tatu na ubingwa wa kombe la FA mara tatu.