Mambo Matano niliyoyaona katika mchezo dhidi ya Chelsea

Arsenal ilirudi katika hali ya ushindi mwishoni mwa wiki baada ya kuifunga timu ya Chelsea kwa jumla ya magoli 2-0. Katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Emirates kuna mengi yalitokea lakini haya ni mambo matano niliyoyaona kwa upande wa Arsenal.

Master Unai Emery alionesha ustadi wake

Ninachompendea Unai Emery ni uwezo wake wa kubadilisha timu kulingana na aina ya mchezo unaocheza timu pinzani. Emery aliwasoma vilivyo Chelsea na akaja na mfumo ambao uliwafanya wachezaji muhimu wa Chelsea wapoteane.

Chelsea huwa wanacheza pasi nyingi kupitia kwa Jorginho, Emery alichofanya ni kumcheza Ramsey nafasi ya kiungo mshambuliaji na Ramsey aliitumia vizuri nafasi hiyo kwani kila alipokuwepo Jorginho, Ramsey alikuwepo, kuna kipindi nilimuona Jorginho akirusha mikono hewani kuonesha kukelwa na ukabaji wa Ramsey, kwa hilo nampa tano Master Unai Emery.

Wachezaji walionesha kupania kushinda mchezo huo

Tangu mwamuzi apulize kipenga cha kuanza kwa mchezo huo, wachezaji wa Arsenal walionesha nia ya kushinda mchezo huo, walikuwa wanakaba kwa nguvu na kwa pamoja na pia walicheza kwa umakini mkubwa, wangefanya hivyo dhidi ya West Ham sasa tungekuwa tunaongea hadithi tofauti.

Koscienly bado wamo

Mambo Matano niliyoyaona katika mchezo dhidi ya Chelsea

Baada ya kuumia na kukaa nje kwa muda mrefu, Koscienly alirudi uwanjani, kuna baadhi ya mechi hakucheza vizuri hadi kufikia hatua ya kwamba baadhi ya mashabiki wa Arsenal walikuwa wanataka asipangwe, lakini juzi aliwajibu kwani alicheza mchezo huo kwa kiwango kikubwa, alifanikiwa kumficha Eden Hazard na kupewa zawadi ya mchezaji bora wa mchezo.

Kuumia kwa Hector Bellerin kulipunguza radha ya ushindi

Pamoja ya mambo mazuri yote yaliyojitokeza katika mchezo huo, kuumia kwa beki wa kulia wa Arsenal, Hector Bellerin ni pigo kubwa sana kwa kikosi hicho, mchezaji huyo ambaye alikuwa ndiyo kwanza amerudi baada ya kukosa michezo kadhaa, ameumia tena na anaweza asicheza kabisa katika mechi zilizobaki msimu huu.

Mashabiki wa Arsenal waliimba jina la Olivier Giroud

Mwaka mmoja uliopita mchezaji wa kifaransa Olivier Giroud alijiunga na Chelsea akitokea Arsenal,na juzi alikuwa anarudi Emirates kwa mara ya kwanza akiwa na jezi ya Chelsea.

Wakati akijiandaa kuingia uwanjani uwanja mzima ulilipuka na kuanza kuimba na na na Giroud, mimi nikiwa mmoja ya mashabiki waliokuwa wakimtetea sana Giroud wakati akiwa Arsenal, nilifarijika kuona ya kwamba mashabiki wengi wanaudhamini mchango wa Giroud kwa Arsenal ingawa sikukubaliana na kuimba jina lake wakati mchezo unaendelea, wangefanyaje iwapo Giroud angeisaidia Chelsea kurudisha magoli na kushinda? kuimba sio mbaya ila wangeimba wakati mchezo umeisha wakati anaingia kumpigia makofi kungetosha.

Hayo ndiyo mambo matano niliyoyaona katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Chelsea, je wewe uliona mambo gani? tupia maoni yako hapa chini.

Speak Your Mind

*