Mambo matano niliyoyaona katika mechi za kirafiki

Jumamosi iliyopita Arsenal ilimaliza mechi za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi na michezo mingine baada ya kuifunga timu ya Lazio ya Italia kwa jumla ya magoli 2-0.

Nimebahatika kuiangalia kwa makini michezo yote ambayo ilioneshwa hadharani (kuna habari ya kwamba Arsenal ilicheza michezo miwili kwa siri ambapo mmoja matokeo na picha zilivuja na mwingine mpaka leo sina uhakika na kilichotokea).

Katika michezo hiyo mambo mengi yalitokea, yalifungwa magoli mengi na mazuri na pia timu ilicheza vizuri na pia kuna mabadiliko mengi ambayo niliyaona, hivyo nimeamua kukuletea mambo matano ambayo mimi niliyaona.

Mambo matano niliyoyaona katika mechi za kirafiki

Arsenal ilitumia mifumo minne

Katika michezo hii ya kirafiki Arsenal ilitumia mifumo minne ambayo ni 4-3-3, 4-2-3-1,4-4-2 na 5-3-2.

Hili ni jambo jema sana kwani timu kuwa na mifumo tofauti linawafanya wapinzani kushindwa kutabiri mfumo gani timu itatumia na pia jambo jingine lililonivutia ni kuweza kuitumia mifumo mingi ndani ya mechi moja kulingana na timu pinzani na pia matokeo ya muda huo.

Mfano mzuri ulikuwa ni mchezo dhidi ya Atletico Madrid ambapo timu ilianza na mfumo wa 4-2-3-1, kipindi cha pili ikacheza 5-3-2 na dakika za mwisho za mchezo ikacheza 4-3-3.

Kutokana na Unai alivyokuwa anapanga vikosi vyake naamini mifumo ambayo timu itatumia msimu ujao ni 4-2-3-1 kama tukiwa na mpira, mabeki wannne na viungo wawili ambao wanaweza kuwa Xhaka na Torreira huku Ramsey au Özil mmoja akicheza nyuma ya mashambuliaji wa kati.

Na kama tukiwa hatuna mpira tutakuwa tukichez mfumo wa 4-4-2, mshambuliaji na kiungo mshambuliaji wakisaidia kukaba kuanzia mbele,hii itasaidia Arsenal kukaba haraka na kufanya mashambulizi mengi ya kustukiza.

Pia sidhani kama tutaona Auba na Laca wakianza kama washambuliaji wa kati, naamini mmoja atakuwa akianza kama mshambuliaji na mwingine kama winga au mmoja akianza mwingine anasubiri benchi.

Safu kali ya ushambuliaji

Arsenal ilifanikiwa kufunga katika kila mchezo iliocheza katika michezo ya kujipima nguvu, hii ni dalili njema kwani wachezaji walionekana kucheza kwa hali ya juu.

Unne mtakatifu wa Özil,Mkhitaryan,Auba na Laca ulionekana ukishirikiana vizuri ambapo walikuwa wakifunga na kuasist bila matatizo, kwangu mimi tatizo ni moja tu, ni vigumu kuwaanzisha wote wanne kwa wakati mmoja ingawa kwenye mechi dhidi ya Lazio kuna wakati kupindi cha pili wote wanne walikuwa uwanjani na wote tuliona kilichotokea.

Safu ya Ulinzi bado inahitaji maboresho

Moja ya sababu kubwa ya Arsenal kufanya vibaya ni kukatika kwa safu yake ya ulinzi hali iliyopelekea timu kufungwa magoli mepesi sana, wengi tulitegemea ya kwamba kusajiliwa kwa Sokratis kungeondoa tatizo hilo,na hadi mchezo wa mwisho wa kirafiki tatizo hilo lilikuwa bado lipo.

Mimi ninachoamini ni kwamba Mustafi, Chambers na Sokratis wote wana uwezo mzuri tu, ila tatizo ni kwamba hawajazoea kucheza upande wa kushoto wa beki ya kati, hivyo wanamuacha beki wa kushoto bila msaada na kusababisha mashambulizi mengi kupitia upande huo.

Holding ana uwezo wa kucheza upande wa kushoto ila sidhani kama amekomaa kiasi cha kucheza kila mchezo,Mavro bado hajazoea soka la kiingeleza na Koscienly ni majeruhi hadi mwaka mpya.

Hapa Unai anaweza kufanya mambo matatu, moja kumchezesha mmoja kati ya Sokratis na Mustafi nafasi hiyo na kuomba wasifanye makosa,mbili kumchezesha Rob Holding na kutegemea makosa kutoka kwa mchezaji kijana au kuingia sokoni na kuleta beki wa kati mwenye uwezo wa kucheza upande wa kushoto(LCB).

Timu ina makipa wazuri

Arsenal ilimsajili Bernd Leno ili kuongeza nguvu katika upande wa makipa na katika mechi hizi za kirafiki naweza kusema ya kwamba nimeridhika na makipa wote watatu.

Petr Cech ndiye kipa aliyepata mikiki mikiki mingi kwenye hizi mechi,aliokoa penati katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid (kwenye penati tano tano) na pia aliokoa penati ya Morata katika mchezo dhidi ya Chelsea kabla ya kuokoa tena katika penati tano tano kwenye mchezo huo, nilimuona Cech aliyebadilika, akiwapanga mabeki na pia anaonekana ya kwamba mwili umejengeka zaidi kutokana na mazoezi kwangu mimi ndiye aliyekuwa kipa bora wa Arsenal katika michezo hii ya kirafiki.

Bernd Leno pia alicheza vizuri ingawa yeye hakupata nafasi ya kuokoa michomo mingi kama Cech, lakini alinifurahisha sana linapokuja suala la kutawanya mipira na pia kucheza mpira kwa miguu, hiki ni kitu muhimu sana kama Arsenal itacheza counter attack. Kwani uwezo wake wa kujua ampe mpira mchezaji gani hata kabla hajadaka ni siraha kubwa ambayo itaifanya Arsenal iwakute wabeki wengi hawajajiandaa, mfano mzuri ulikuwa ni goli la Özil dhidi ya PSG kaliangalie vizuri utaona ninachokuambia.

Martinez na yeye alicheza vizuri hakufanya makosa yeyote ila kwa sasa nadhani atakuwa kipa wa tatu ama atatolewa kwa mkopo Cech na Leno ni bora kuliko yeye.

Kwangu mimi ningependa Leno awe kipa wa kwanza na Cech msaidizi.

Mattéo Guendouzi

Kwangu mimi Mattéo Guendouzi ndiye aliyekuwa mchezaji bora katika mechi za kirafiki, uwezo wake wa kupiga pasi kwa utulivu wa hali ya juu, kupokonya mipira bila kufanya madhambi na kuanzisha mashambulizi ni vitu ambavyo ni vigumu kuviona kutoka kwa mtoto wa miaka 19.

Kwa dau la paundi milioni 7 tu naamini hapa Arsenal walilamba dume, najua ilikuwa ni michezo ya kirafiki na ningependa kumuona atacheza vipi kwenye mechi zenye ushindani mkubwa, na sintoshangaa kama ataanza jumapili ijayo dhidi ya Manchester City.

Pia madogo Smith Rowe na Reiss Nelson walinivutia sana.

Hayo ndiyo mambo matano niliyoyaona  katika mechi za kirafiki. Je wewe uliyeagalia mechi za kirafiki, ni mambo gani uliyoyaona yaliyokuvutia na ambayo hukuyapenda , tupia maoni yako hapa chini.

Speak Your Mind

*