Mambo matano niliyoyaona katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Burnley

Jumamosi iliyopita Arsenal ilianza kushinda tena baada ya kuifunga timu ya Burnley kwa idadi ya magoli 3-1, baada ya kufungwa na Southampton kwenye ligi na Totenham kwenye kombe la Carabao, ilikuwa ni muhimu kwa Arsenal kushinda ili kuendeleza matumaini ya kumaliza ndani ya timu nne za mwanzo katika ligi kuu.

Katika mchezo kuna mambo mengi sana yaliyotokea ila kwangu mimi haya ndiyo mambo matano ambayo niliyaona.

1: Hatimaye Arsenal ilifanikiwa kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza

Tangu msimu huu uanze, Arsenal ilikuwa haijawahi kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza, mara nyingi walikuwa wakienda mapumziko wakiwa nyuma ama wakiwa sare, kwa mara ya kwanza msimu huu tulishuhudia hali hiyo ikibadirika baada ya goli la Pierre Emerick Aubamayang kumaliza mkosi huo.

2: Burnley walibipu, Arsenal walipokea

Nchini Uingeleza kuna imani ya kwamba wachezaji wa Arsenal ni dhaifu, na hali hii imepelekea timu nyingi kwenda Emirates na kuwachezea rafu wachezaji wa Arsenal hivyo kuwafanya washindwe kucheza kwa uhuru na kuishia kupoteza mchezo.

Hali hiyo ilikuwa ikitokea sana kipindi cha nyuma wakati Arsene Wenger alipokuwa kocha wa Arsenal, kwa mtazamo wangu naamini kocha wa Burnley aliwaambia wachezaji wake wacheze kibabe na kwa mara ya kwanza nikaona wachezaji wa Arsenal wakijibu, Sokratis, Xhaka, Torreira na Kolasinac wameongeza kitu kwenye hii timu, kwanituliona jinsi wachezaji wa Arsenal walivyoweza kucheza soka la kutumia nguvu na kuwazidi Burnley hadi kufikia hatua ya kocha wao kupaniki.

3: Kupaniki kwa Sean Dyche

Baada ya mchezo kuisha kocha wa Burnley, Sean Dyche aliwaacha watu wengi hoi jinsi alivyompa mkono kocha wa Arsenal, Unai Emery.

Sean Dyche alionekana ni mwenye hasira na akiwafokea waamuzi mara kwa mara, katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo huo alionekana kuwashambulia wachezaji wa Arsenal kwa kukosa uanamichezo na kujiangusha, na alipoulizwa kuhusu uhuni waliokuwa wanafanya wachezaji wake alikosa jibu la maana.

4: Umuhimu wa Granit Xhaka

Kwa sasa Granit Xhaka ni mchezaji muhimu kuliko wote ndani ya kikosi cha Arsenal, katika mchezo wa juzi alianza kama kiungo wa kati na kuifanya Arsenal icheze vizuri, mara baada ya Unai kuamua kucheza na mabeki watatu, Xhaka alicheza kama beki wa kati,pia tumeona Xhaka akicheza kama beki wa kushoto.

kuwa na mchezaji ambaye anaweza kucheza vizuri katika nafasi mbalimbali ni baraka kubwa kwa kocha kwani kocha anaweza kufanya mabadiliko ya kimfumo au kiufundi bila ya kubadilisha wachezaji kama ilivyotokea jumamosi iliyopita na kuisaidia Arsenal kupata ushindi.

5: Mesut Özil

Kocha Unai Emery aliamua kumuacha nje Mesut Özil katika mechi dhidi ya Southampton na Totenham kwa madai ya kwamna ni sababu za kiufundi.

Lakini katika mchezo wa juzi Özil alionesha kwa nini ni mchezaji anayelipwa pesa nyingi kuliko wote ndani ya Arsenal.

Ana uwezo wa kipekee katika kuona pasi ambazo wachezaji wengi hawawezi kuona, ili kudhibitisha hilo angalia ile pasi aliyompigia Kolasinac iliyosababisha goli la kwanza la Arsenal.

Arsenal ni bora lakini wanakuwa bora zaidi Mesut Özil akicheza.

Mambo matano niliyoyaona katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Burnley

 

Hayo ndiyo mambo matano niliyoyaona katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Burnley, je wewe uliona kipi? tupia maoni yako hapa chini.

 

Speak Your Mind

*