Manchester United Vs Arsenal-Je Arsenal wapo tayari kuvunja mwiko?

 

Manchester United Vs Arsenal-Je Arsenal wapo tayari kuvunja mwiko?

Nakumbuka miaka ile ambapo mechi kati ya Arsenal na Manchester United ilikuwa ni mechi ambayo ilitumika kuamua bingwa wa Uingeleza. Kipindi hicho kabla ya Machester City na Chelsea hazijaundwa, kipindi cha Arsene na Ferguson.

Mpaka leo hii ni mechi kubwa kwa timu zote mbili, ingawa sio kubwa kama kipindi kile, Wenger na Ferguson walishaondoka, Arsenal haijachukua kombe kwa miaka 14 sasa na Manchester United wanaelekea mwaka wa 7 bila ndoo.

Timu hizo mbili zinakutana katika hali tofauti, Manchester United wao wakiwa wanaendelea kuporomoka na kushuka kiwango tangu aondoke Fergie, wakati Arsenal wanaonekana kuimalika na kucheza vizuri tangu aondoke Arsene Wenger na kuja Unai Emery.

Mwenendo wa timu

Arsenal inaingia katika mchezo wa leo ikiwa ina mwenendo mzuri , kwani tangu wafungwe mechi mbili za mwanzo hawajafungwa tena, wamecheza mechi 19 bila kufungwa na leo wanaweza kufikisha mechi 20.Waliwafungwa Bournemouth 2-1, Vorskla 3-0 kabla ya kuwashushia kipigo Totenham cha 4-2.

Manchester United wao wana mwenendo usioridhisha sana, kwani katika mechi tatu zilizopita walifungwa na watani wao wa jadi Manchester City 3-1, Waliishinda Young Boys 1-0 kwa mbinde na goli la mkono,walitoa sare ya 2-2 na Southampton na kupelekea kocha wa Southampton kupoteza kibarua chake.

Makocha

Arsenal kwa sasa inafundishwa na Unai Emery ambaye sifa yake kubwa ni kuwasoma wapinzani na kuwapangia kikosi ambacho anaamini kitampa ushindi, na pia ameifanya Arsenal icheze soka la kuvutia na iwe ni timu ambayo haifungwi kirahisi.

Kwa upande wa Man Utd, kocha wao Jose Mourinho, kwanza hana kikosi cha kwanza, amegombana na nusu ya wachezaji na pia msimu huu wamekuwa wakicheza soka lisiloeleweka, tofauti na Mourinho wa zamani ambaye timu zake zilikuwa hazifungwi ovyo, timu hii ya Mourinho huyu imekuwa ikifungwa hovyo kiasi cha kwamba imefungwa magoli mengi kuliko iliyofungwa katika ligi kuu mwaka huu.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery hajawahi kumfunga Mourinho katika michezo mitano waliyocheza, Mourinho akiwa na Real Madrid aliifunga Valencia ya Unai mara tatu na kutoka sare mara moja , pia Mourinho kawahi kumfunga Unai akiwa na timu ya Sevilla mara moja.

Lakini nitamtetea Unai hapa kwani Mourinho alikuwa na timu yenye wachezaji wakubwa na wenye vipaji ya Real Madrid wakati Unai alikuwa na timu za kuungaunga za Sevilla na Valencia.

Mashabiki

Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka minne nimeona mashabiki wa Arsenal wameungana na kuwa kitu kimoja, niliangalia mchezo dhidi ya Spurs, mashabiki walikuwa nyuma ya timu wakati wote, hata wakati timu ipo nyuma 2-1 wakati wa mapumziko bado waliendelea kushangilia kwa nguvu, ni jambo jema kuona hali ya umoja imerudi ndani ya Arsenal.

Kwa upande wa Machester United mashabiki wao wanaonekana kugawanyika sana, kuna wasiomtaka Jose Mourinho na wengine wanaotaka aendelee, wananikumbusha kipindi cha Wenger In na Wenger Out, ni vigumu sana timu kufany vizuri katika mazingira haya ndiyo maana sishangai timu yao ipo nafasi ya 7.

Majeruhi

Jana Koscienly alicheza katika timu ya vijana na kulazimika kutolewa mapema baada ya kuumia, Nacho Monreal jana alifanya mazoezi na kikosi cha kwanza, Mesut Özil leo anatarajiwa kufanyiwa vipimo kwani bado alikuwa na maumivu ya mgongo,Dinos Mavporanos bado anauguza mguu na Danny Welbeck ni majeruhi wa muda mrefu, hao wachezaji wanategemewa kukosekana leo.

Pia Granit Xhaka hatacheza leo kutokana na kuwa na kadi tano za njano.

Kwa upande wa Manchester United nako kuna majeruhi, Alexis Sancheza ataukosa mchezo huu pamoja na Lindelof, kuhusu wachezaji wengine wanaodhaniwa ya kuwa ni majeruhi katika ukurasa wa MUTV hakuna taarifa rasmi kwani Mourinho alikataa kutoa taarifa za wachezaji.

Vikosi

Arsenal

Kwa upande wa Arsenal ningependa sana kianze kikosi kilichomaliza mchezo dhidi ya Totenham, na pia niliupenda ule mfumo 3-4-1-2, Ramsey akicheza nyuma ya Aubamayang na Lacazette na Matteo Guendouzi akichukua nafasi ya Xhaka kucheza na Torreira pale kati. Wachezaji wengine wote wabaki vile vile.

Kwa upande wa Manchester United, katika mchezo dhidi ya Southampton aliwatumia Matic na Scott kama mabeki wa kati, nipo hapa nafanya maombi awapange tena, sijali wachezaji wengine akiwapanga hao wawili kama mabeki wa kati roho yangu itakuwa na furaha.

Utabiri wa matokeo

Arsenal ina miaka 11 bila ya kushinda Old Traffod katika mchezo wa ligi kuu na mara ya mwisho kushinda katika uwanja huo ilikuwa ni mwezi wa nne mwaka 2015 katika kombe la FA baada ya Danny Welbeck kuizamisha Manchester United iliyokuwa ikifundishwa na Louis Van Gal.

Hata Arsenal iwe nzuri vipi, imekuwa ikipata tabu kuwafunga Manchester United kwao, kwangu mimi naona hili ni tatizo la kisaikologia zaidi kuliko uwezo.

Kwa sasa mambo yamebadilika Arsenal, timu ina mwalimu tofauti na mwenye mbinu tofauti hivyo naamini ya kwamba umefika wakati wa kuuvunja huu mwiko na kuwafunga Manchester United kwao.

Hivyo natabiri ya kwamba Arsenal itashinda mchezo huu kwa jumla ya magoli 3-1, Auba na Lacazette kutupia.

Je wewe una maoni gani kuhusi mchezo huu? tupia maoni yako hapa chini.

Speak Your Mind

*