Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Wakati Arsenal ikimsajili Matteo Guendouzi mwezi wa saba mwaka huu wengi wetu tuliamini ya kwamba kiungo huyo mwenye umri wa mikiaka 19 alikuwa anasajiliwa kwa wakati ujao.

Matteo Guendouzi awa mchezaji bora wa mwezi wa nane

Nilitegemea ya kwamba jambo la maana lilikuwa ni kumtoa kwa mkopo timu zinazoshika nafasi za 10-20, ili akacheze katika mazingira yasiyo na ushindani mkubwa wa namba ili apate kuzoea soka la kasi la kiingeleza. Hasa ukizingatia ya kwamba Arsenal ilikuwa inabadilisha kocha na pia kulikuwa na ulazima wa kuanza vizuri hivyo kumtumia mchezaji wa miaka 19 lisingekuwa jambo la busara.

Lakini nakumbuka wakati wa mkutano na waandishi wa habari kocha mkuu wa Arsenal alisema ya kwamba mchezaji huyo alikuwa katika mipango yake kwa msimu huu.Binafsi sikuamini, nilijua ndiyo yale yale makocha wanasema kitu flani na wanafanya kitu tofauti kabisa na walichosema.

Kama utani dogo alicheza vizuri sana katika mechi za kirafiki na baada ya msimu kuanza dogo alionesha kiwango kikubwa tofauti na umri alionao.

Ni kweli alifanya makosa, kutokana na ugeni na pia kukosa uzoefu lakini kwa ujumla amecheza vizuri kuliko wachezaji wengi wakubwa na wazoefu wa Arsenal.

Kiwango chake kiliwafurahisha mashabiki wengi wa Arsenal kiasi cha kumchagua kuwa mchezaji bora wa mwezi wa nane na wasomaji wa tovuti rasmi ya timu arsenal.com

Kwa kweli mchezaji huyo alistahili tuzo hiyo, inatia moyo ya kwamba mchezaji huyo ameanza vizuri maisha yake kama mchezaji wa Arsenal na pia nina imani ya kwamba tuzo hiyo itamfanya mchezaji huyo ajitume zaidi mazoezini na kwenye michezo ya ushindani.

Hongera Matteo Guendouzi.

Speak Your Mind

*