Mtazamo wangu-Msimu wa Arsenal mpaka sasa

Wakati ligi ikiwa imesimama kwa wiki mbili ili kupisha mechi za kimataifa nimeona leo bora niongelee kuhusu mwenendo wa Arsenal tangu msimuu huu uanze. Huu ni mtazamo wangu kuhusu msimu wa Arsenal mpaka sasa.

Unai Emery amevuka matarajio yangu

Mtazamo wangu-Msimu wa Arsenal mpaka sasa

Huu umekuwa msimu tofauti sana  kwa sisi mashabiki wa Arsenal, Arsene Wenger aliondoka mwishoni mwa msimu uliopita na akaletwa kocha mpya Unai Emery.

Bila kujali kama unaamini ya kwamba uwezo wa Wenger ulifikia kikomo ama la, kuchukua mikoba ya kocha aliyeiongoza timu kwa miaka 22 si kazi rahisi, lakini kwangu mimi naona mpaka sasa Unai Emery kafanya kazi nzuri.

Alianza msimu vibaya baada ya kufungwa mechi mbili za mwanzo na baada ya hapo hakuangalia nyuma tena kwani timu imekuwa ikipata matokeo mazuri, mpaka sasa Arsenal ni ya tano kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingeleza ikiwa na pointi 24, tatu nyuma ya wapinzani wao wa jadi Totenham wanaoshika nafasi ya nne.

Wachezaji walifanya vizuri

Safu ya ushambuliaji ya Arsenal ikiongozwa na Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang imefanya vizuri msimu huu, tayari wameshafunga magoli 12 kati yao msimu huu, ambayo yanakaribia kufikia nusu ya magoli yote yaliyofungwa na Arsenal mpaka sasa 26.

Lacazzete ameonekana akiwa hatari zaidi akicheza kama namba 9 hali iliyomfanya kocha Unai Emery kumchezesha Auba kama kiungo mshambuliaji, licha ya hao bado wamefanikiwa kufanya vizuri.

Lucas Torreira amekuwa kama gundi ambayo inaiunganisha timu, kwani tangu aanze kucheza katika kikosi cha kwanza Arsenal bado haijapoteza mchezo hata mmoja, ana uwezo mkubwa wa kuwapokonya maadui mpira na kuanzisha mashambulizi ya haraka.Uwepo wake uwanjani umemfanya Granit Xhaka kucheza vizuri pia.

Alex Iwobi pia anaonekana amebadilika sana msimu huu na kucheza kwa kujiamini sana ingawa bado anatakiwa aongeze bidii hasa katika uzalishaji na ufungaji wa mabao.

Upande wa makinda Emile Smith Rowe na Matteo Guendouzi wamefanya vizuri sana na wamezitumia vizuri nafasi zote walizopata na kuonesha uwezo wao.

Waliocheza chini ya kiwango

Mkongwe Stephan Lichtsteiner aliletwa ili kumsaidia Hector Bellerin, mpaka sasa ameshacheza michezo mitatu katika ligi kuu na kama nikiwa mkweli nimemuona kama ni mchezaji ambaye hawezani na kasi ya ligi kuu ya Uingeleza.

Inawezekana ikawa ni umri au bado hajazoea ligi, sioni kama ataweza kuwa chaguo la kwanza la Arsenal, si ajabu kusikia tetesi za kwamba Arsenal wanatafuta beki mpya wa kulia wa kusaidiana na Bellerin.

Mchezaji mwingine ambaye ameshindwa kunishawishi ni Sokratis Papastathopoulos, mchezaji huyo wa zamani wa Dortumund alitua kwa dau la paundi milioni 16. Nilitegemea ya kwamba yeye ndiye angekuja na kuwa mhimili wa safu ya ulinzi ya Arsenal na mpaka sasa hajafikia matarajio.

Amepoteza namba katika kikosi cha kwanza na sasa Rob Holding na Mustafi ndiyo wanaoanza kama mabeki wa kati.

Mbinu za mchezo

Mwalimu Emery ameendelea kuutumia mfumo aupendao wa 4-2-3-1, pamoja ya kuanza vibaya na mfumo huo matunda yake tumeyaona ambapo Arsenal imecheza michezo 10 ya ligi bila kufungwa, imeshinda mara 7 na kutoa sare mara 3.

Ukiondoa mchezo wa mwisho dhidi ya Wolves uliomalizika kwa sare ya 1-1, safu ya ushambuliaji ya Arsenal imeimalika zaidi kutokana na mfumo huu, sababu kubwa ni kwamba timu inaposhambulia mfumo huu hubadilika na kuwa 4-2-2-2, hivyo kuwafanya wachezaji wa Arsenal kujaza nafasi zinazoachwa wazi na walinzi wa timu pinzani (angalia vizuri goli la kusawazidha dhidi ya Wolves utaona), hali inayowafanya Lacazette na Auba kucheza kama washambuliaji (ndiyo sababu kubwa inayowafanya wafunge magoli mengi).

Ingawa mambo yamekuwa magumu kidogo katika mechi zilizopita ambapo Arsenal ina michezo mitatu ya ligi bila kushinda.

Neno la mwisho

Najua Arsenal imetoka sare nne katika mechi tano zilizopita na kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wameanza kuingiwa na wasiwasi, kwangu mimi naona timu bado inajengwa na kocha Unai Emery anaonekana kama mtu ayayejua anachofanya naamini timu itaendelea kuimalika.

Kwa nilichokiona mpaka sasa siamini kama Arsenal itakuwa bingwa msimu huu ila nina imani kubwa itashika nafasi ya tatu ama ya nne na kufudhu kwa michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya kwa msimu ujao.

Na huu ndio mtazamo wangu kuhusu msimu wa Arsenal mpaka sasa.

Je wewe umeionaje timu ya Arsenal mpaka sasa? tupia maoni yako hapa chini.

 

Speak Your Mind

*