Wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia

Wakati kombe la dunia likiendelea nchini Urusi, leo nimeamua kukuletea ninavyoona mimi kuhusu ushiriki wa wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia.

Wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia

Arsenal ina jumla ya wachezaji 9 wanaoziwakilisha nchi zao katika fainali hizi za kombe la dunia na nikiwa mkweli wengi wao hawajafanya vizuri sana.

Kati ya wachezaji hao tisa, watano tu ndio walioanza katika raundi ya kwanza na wanne wameanza katika raundi ya pili.

Mchezaji wa kwanza wa Arsenal kufanya vizuri katika fainali za mwaka huu alikuwa ni Granit Xhaka, baada ya kufunga bonge la goli la kusawazisha wakati Switzerland ilipocheza dhidi ya Serbia.Baadaye Switzerland walishinda mchezo huo kufuatia goli la pili lililofungwa na Xherdan Shaqiri.

Pia katika mchezo huo Xhaka aliingia katika matatizo na fifa wakati akishangilia hilo goli, amepigwa faini ya dola elfu 10 kwa kosa la kuchanganya siasa na soka.

Katika kikosi hicho pia kuna mchezaji mpya wa Arsenal,Lichsteiner ambaye alicheza vizuri katika mechi zote mbili na alinifurahisha sana katika mechi ya kwanza kwani aliweza kumzuia kwa ufanisi mkubwa mchezaji kutoka Brazil,Neymar.

David Ospina  aliisaidia timu yake ya Colombia kushinda kwa goli 3-0, katika mchezo wa kwanza timu yake ilifungwa huku Ospina akicheza vibaya lakini katika mchezo wa juzi alibadilika baada ya kufanya kazi ya ziada kuzuia ya wachezaji wa Poland.

Pia katika mchezo huo aliumia huku nafasi za kufanya mabadiliko zikiwa zimeisha na bado alifanikiwa kuokoa mpira wa shuti kali uliopingwa na Lewandoski katika dakika za mwisho za mchezo huo.

Mohamed Elneny yeye amecheza michezo yote mitatu akiwa na timu yake ya taifa ya Misri lakini kwa bahati mbaya walifungwa katika michezo yote huku Elneny akishindwa kung’ara.

Nacho Monreal yeye bado hajacheza hata dakika moja moja katika michuano hiyo ya kombe la dunia, hali ambayo pia imemkuta Dany Welbeck ambaye hakugusa mpira wakati Uingeleza wakiifumua Panamá goli 6-1.

Mesut Özil ambaye alianza wakati Ujerumani walipofungwa na Mexico, hakucheza katika mchezo wa pili walipoishinda timu ya Sweden goli 2-1.

Alex Iwobi akiiwakilisha Nigeria aliingia dakika za mwisho wakati tai hao wa kijani walipoifunga timu ya Iceland kwa jumla ya magoli 2-0.Iwobi alianza katika mchezo wa kwanza ambapo walifungwa goli 2-0 dhidi ya Croatia.

Joel Campbell hakucheza wakati timu yake ya taifa ya Costa Rica ilipofungwa katika muda wa nyongeza na Brazil,Joel Campbell aliingia kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa kwanza ambapo hakuna la maana alilolifanya.

Huo ndio mchango wa wachezaji wa Arsenal mpaka sasa katika kombe la dunia, Je kwako wewe ni mchezaji gani wa Arsenal aliyefanya vizuri mpaka sasa? tupia maoni yako hapa chini.