Arsenal Vs Everton-Mambo matano niliyoyaona

Juzi jumapili Arsenal ilipata ushindi wake wa tano chini ya kocha Unai Emery baada ya kuifunga timu ya Everton kwa magoli 2-0.

Katika mchezo huo kuna mambo mengi sana yaliyotokea ila haya mabo matano ndiyo yaliyovuta fikra zangu zaidi.

Petr Cech bado kipa bora

Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakipinga uamuzi wa kocha Unai Emery wa kumuanzisha Petr Cech.

Lakini baada ya kumuangalia Bernd Leno kwenye Europa League na kumuangalia Petr Cech kwenye mechi za msimu huu , naamini kwa sasa Cech ndiye anayeshahili kuwa kipa namba moja.

Leno ni mzuri kwa kucheza mpira kwa miguu lakini Cech ni bora kuliko Leno linapokuja kwenye suala la kuzuia michomo na hicho ndicho mashabiki tunachokitaka.

Na kama kuna siku ambayo angeweza kuwafunga midomo mashabiki wote wanaombeza ni juzi ambapo alicheza kwa kiwango cha hali ya juu.

Aliweza kuokoa magoli ya wazi kutoka kwa washambuliaji wa Everton na pia alikuwa akifanya maamuzi sahihi linapokuja suala la kucheza krosi. Kwangu mimi juzi Petr Cech ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa mchezo.

Lucas Toreira anamfanya Granit Xhaka kuonesha ubora wake

Kwa mara ya kwanza Lucas Torreira alianza katika ligi kuu ya Uingeleza baada ya Matteo Guendouzi kupumzishwa.

Kama alivyofanya katika michezo ya nyuma ambayo alianza kama mchezaji wa akiba, mchezaji huyo alikichangamsha kiungo cha Arsenal na kuifanya timu icheze vizuri.

Cha msingi nilichokiona ni kwamba uwepo wa Torreira ulimpunguzia majukumu Xhaka na kumfanya acheze mpira kwa utulivu mkubwa huku majukumu ya kukaba akiachiwa Torreira na majukumu ya kuanzisha mashambulizi akiachiwa Xhaka.

Pamoja na kupata kadi ya njano mapema katika mchezo huo, Torreira alionesha ukomavu mkubwa na kuweza kuwapokonya mipira maadui bila kuwafanyia faulo.

Binafsi sina matatizo na Matteo Guendouzi ila naamini Torreira na Xhaka wanapaswa kuanza pamoja.

Uelewano kati ya Aaron Ramsey na Mesut Özil

Wakati mchezo ukianza Mesut Özil alianza kama winga wa kulia na Aaron Ramsey alianza kama kiungo mshambuliaji namba 10.

Lakini ukiangalia mchezo huo kwa makini walikuwa wakibadilishana kucheza winga wa kushoto ili kumsaidia Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye alianza mchezo huo kama winga wa kushoto.

Ukiangalia goli la kwanza la Arsenal Aubamayang anacheza kama mshambuliaji wa kati, Lacazette kama namba 10, na Ramsey kama winga wa kushoto.

Kubadilishana namba huko kuliisaidia Arsenal kutawala kipindi cha pili na huku Ramsey akipata asisti mbili katika mchezo huo. Hali hii pia niliiona katika kipindi cha pili dhidi ya Newcastle.

Kwa mtazamo wangu mimi uelewano bado haujawa mkubwa ila kuna kitu Unai Emery anakifanya na muda si mrefu tutaona matunda yake.

Rob Holding alicheza vizuri

Baada ya kuumia kwa Sokratis mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa na wasiwasi kama Arsenal ingeweza kuhimili vishindo vya washambuliaji wa Everton waliokuwa wanalisakama lango la Arsenal mara kwa mara.

Lakini Rob Holding aliweza kuwatuliza mashabiki hao baada ya kucheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu.

Bado Unai Emery anaendelea kuijenga timu

Arsenal Vs Everton-Mambo matano niliyoyaona

Cha msingi ni kukumbuka ya kwamba kila kocha ana falsafa zake na itachukua muda kwa wachezaji hawa kuelewa ni nini hasa mwalimu anataka, kwa sisi tunaoifuatilia Arsenal kwa karibu tumeanza kuona mabadiliko chanya katika uchezaji wa timu, ufanyaji wa mabadiliko na upangaji wa timu, cha msingi tumpe muda kocha Emery.

Hayo ni mambo niliyoyaona katika mchezo kati ya Arsenal na Everton, je wewe uliona nini ? tupia maoni yako hapa chini.

 

Cardiff Vs Arsenal-Mtazamo wangu

Leo mchana Arsenal itakuwa nchini Wales kucheza na timu ya Cardiff katika raundi ya nne ya ligu kuu ya Uingeleza.

Arsenal ambayo ilianza ligi vibaya baada ya kufungwa na Manchester City na Chelsea, wiki iliyopita ilipata ushindi wake wa kwanza chini ya kocha Unai Emery baada ya kuifunga timu ya West Ham kwa jumla ya magoli 3-1.

Mchezo wa leo una umuhimu mkubwa sana, Arsenal inabidi icheze kufa na kupona ili kupata pointi tatu muhimu kwani ikishindwa kufanya hivyo itakuwa inazidi kuachwa na timu nyingine kubwa ambazo zote zilipata ushindi.

Kuelekea katika mchezo huo nitaangalia mambo muhimu ya kuzingatia na pia nitatoa mtazamo wangu kuhusu kikosi kitakachoanza na pia utabiri wa matokeo.

Arsenal haifanyi vizuri ugenini

Tangu mwaka huu uanze Arsenal imekuwa ikifany vibaya sana ugenini, kama sikosei mwaka 2018 Arsenal imeshinda mchezo mmoja tu (mchezo wa mwisho wa ligi msimu uliopita).

Katika msimu huu Arsenal imeshacheza mchezo mmoja wa ugenini na kufungwa 3-2 na Chelsea , kocha Unai Emery anatakiwa kuwapanga vizuri vijana wake ili kuondokana na rekodi hii mbaya na kushinda mchezo huu.

Cardiff hawafungi

Pamoja na Arsenal kuwa na rekodi mbaya ugenini, kitu kinachonipa matumaini leo ni kwamba Cardiff hawajafunga goli lolote tangu mwezi wa nne mwaka huu na tagu msimu huu uanze hawana goli hata moja (ingawa wana uwiano wa magoli ya kufungwa na kufunga bora kuliko Manchester United).

Wamekuwa wakifungwa ama kupata sare za 0-0, naamini mchezo wa leo watapaki basi na kutegemea kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Lucas Torreira

Kwa mashabiki wengi wa Arsenal, Lucas Torreira ni usajili bora wa timu katika dirisha lililopita la usajili, lakini mpaka sasaa bado hajaanza mchezo hata mmoja, hii ni kutokana na kwamba kocha anataka aizoee ligi kwanza kabla hajamuanzisha.

Lakini baada ya kusikiliza mahojiano kati ya kocha Unai Emery na waandishi wa habari ambapo Emery alisema ya kwamba mchezaji huyo yupo tayari kuanza.

Ukiangalia vizuri mchezo dhidi ya West Ham, Arsenal ilianza kucheza soka la kueleweka mara baada ya kuingia kwake na Xhaka kupanda juu kidogo.

Naamini Torreira leo ataanza kama kiungo mkabaji akicheza nyuma ya Xhaka na Ramsey huku dogo Guenduzi akianzia benchi.

Mesut Ôzil

Wiki iliyopita fundi Ôzil hakucheza kwa kile kilichodaiwa ya kwamba alikuwa aumwa na baadaye kukawa na tetesi za kwamba alikuwa amegombana na kocha Unai Emery na baadaye ikagundulika ya kwamba ni kweli alikuwa anaumwa.

Lakini kutoka jumanne ya wiki hii Ôzil ameanza mazoezi ya jana alituma ujumbe kupitia mitandao ya kijamii ya kwamba yupo tayari kwa mchezo wa leo.

Katika mahojiano ya waandishi wa habari,Unai Emery alisema ya kwamba anataka Ôzil awe anacheza nafasi mbili, moja kama namba 10 na nyinigine kama winga wa kulia namba 7, kulingana na mchezo na adui.

Leo naamini Emery atamtumia Ôzil kama winga wa kulia na kumhamisha Mkhitaryan winga wa kushoto huku Iwobi akianzia benchi.

Kikosi

Kama nilivyosema leo natagemea mabadiliko mawili tu kulinganisha na kikosi kilichoanza dhidi ya West Ham hivyo kikosi ninachotegemea kitaanza leo ni kama kinavyoonekana kwenye picha hapo chini.

Cardiff Vs Arsenal-Mtazamo wangu

Utabiri wa matokeo

Najua ya kwamba Cardiff watapaki basi na watajaribu kucheza faulo nyingi ili kuipunguza nguvu Arsena, lakini naamini ubora wa kikosi cha Arsenal ni wa hali ya juu na watashinda mchezo huo bila shida ingawa siwaamini sana mabeki wa Arsenal hivyo nitasema 4-1, Auba, Lacazette na Ôzil kufunga.

Je wewe unatabiri vipi tupia maoni yako hapa chini ukiweka kikosi chako na matokeo unayoamini timu itapata.

#COYG

In Unai We Trust-Walete Manchester City

Ligi kuu ya Uingeleza ilianza ijumaa iliyopita na kwa upande wa Arsenal, Ligi hiyo inaanza leo ambapo jeshi la Arseanl chini ya kocha mkuu Unai Emery litawakabili mabingwa watetezi Manchester City.

Baada ya kufanya usajili wa wachezaji watano wapya na kuiandaa timu kwa wiki 6 na baada ya kucheza mechi za kirafiki na kufanya vizuri, umefika wakati wa ukweli, wakati ambapo kila mchezo usahesabika na utaamua nafasi ya Arsenal mwisho mwa msimu.

Ukizingatia umuhimu wa mchezo wa leo, Ninakuletea kiundani mambo muhimu unayotakiwa uyajue kuelekea katika mchezo huo na mwisho nitatoa utabiri wangu.

Historia

Najua unaweza usiamini hili, ila linapokuja pambano baina ya timu hizi mbili Arsenal anaibuka mbabe, kwa taarifa yako katika ligi kuu ya Uingeleza,Manchester City alimfunga Arsenal kwa mara ya kwanza mwaka 2006, baada ya kupokea vipigo 15 na sare 3 tu katika michezo 18 kabla ya hapo.

Pia Arsenal inaongoza katika magoli ya kufunga na pia michezo ambayo imecheza bila kuruhusu goli.Machester City walianza kubadilisha hali ya hewa baada ya kununuliwa na matajiri wa kiarabu ambapo timu hiyo imefungwa mara mbili tu katika michezo 12 iliyopita na ushindi wa mwisho wa Arsenal ulikuwa mwaka 2015.

Pamoja na utajiri wao wote, Ushindi wa Manchester City msimu uliopita katika uwanja wa Emirates ulikuwa wa kwanza tangu mwaka 2012.

Makocha

Kupambana na Guardiola sio kitu kigeni kwa kocha mpya wa Arsenal-Emery amekutana na timu zinazofundishwa na Pep mara 10.

Katika mara hizo 10, Pep kashinda michezo 6 na minne ilimalizika kwa sare,kwa kifupi ni kwamba Emery hajawahi kuifunga timu inayofundishwa na Pep Guardiola.

Lakini kumbuka ya kwamba mapambano hayo yalikuwa ni kati ya Valencia na Barcelona, ni makocha wachache sana waliweza kuisimamisha Barcelona ile ambayo kwa mtazamo wa wengi ni bora kabisa kuwahi kutokea.

Mchezo wa mwisho kati ya makocha hao ilikuwa ni mwaka 2012, baada ya hapo Emery ameenda kushinda makombe nane akiwa na timu za Sevilla na PSG.

Emery anapendelea mfumo wa  4-2-3-1 ambao alipata nao mafanikio makubwa akiwa Sevilla na Pep anatumia mfumo wa 4-3-3 anaoutumia tangu akiwa na Barcelona.

Mwamuzi-Michael Oliver

Mwamuzi katika mpambano huo si mwingine bali ni Michael Oliver,Refa huyo anasifika kwa wepesi wa kutoa penati ,hilo linaweza kuwa tatizo kubwa kwa Arsenal kwani kama Sokratis au Stephan Lichtsteiner iwapo wataanza kwani wana sifa ya kutumia nguvu kukaba.

Lakini Arsenal wanaweza kutumia hilo kwa faida yao kwani kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza wanaweza kuwakuta mabeki wa City bila kujipanga na kuwalazimisha kucheza faulo na kupata kadi.

 

Habari za timu 

Laurent Koscienly na Kolasinac watakosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi, Danny Welbeck, Nacho Monreal,Aaron Ramsey walikuwa hawana uhakika wa kucheza mchezo huu kutokana na kutokuwa fiti kutokana na majeraha au kushiriki kombe la dunia.

Kikosi

Ukweli ni kwamba hakuna anayejua mchezaji gani ataanza na nani ataanzia benchi, itagememea na mfumo atakaochagua kuanza nao na pia utayari wa wachezaji waliopo, ninaimani ya kwamba ataenda na mfumo wa 4-2-3-1 na kikosi kitakuwa kama ifuatavyo.

In Unai We Trust-Walete Manchester City

Utabiri

Najua Manchester City ni timu nzuri na walifikisha pointi 100 msimu uliopita na najua kila mchambuzi wa soka anaipa Machester City ushindi, na pia najua Unai hajapata muda wa kutosha kuiandaa timu, lakini nina imani leo hii Arsenal inashinda.In Unai We Trust.

Utabiri wangu Arsenal 2-1 Manchester City,Auba kutupia

COYG

Wito wangu kwa mashabiki wa Arsenal-Tumpe Unai Emery muda

Msimu mpya wa ligi kuu ya Uingeleza unaanza leo kwa mchezo kati ya Machester United na Leicester City, kwa sisi mashabiki wa Arsenal kuanza kwa msimu mpya ni mwanzo kwa kila kitu, kocha mpya, benchi jipya la ufundi, wachezaji watano wapya, mifumo mipya ya uchezaji, nyuma ya pazia pia kumefanyika mabadiliko mengi.

Wito wangu kwa mashabiki wa Arsenal-Tumpe Unai Emery muda

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996,Arsenal itaanza msimu mpya bila ya mfaransa Arsene Wenger, hili ni jambo zuri kwani kwa mara ya kwanza nimeona mashabiki wengi wakiwa na matumaini mapya na timu hii.

Unai Emery anaanza maisha yake rasmi kama kocha wa Arsenal kwa kupambana na mabingwa watetezi, Manchester City.Baadaye ataenda darajana kucheza na Chelsea, ni mechi ngumu sana kwa kocha mgeni, lolote linaweza kutokea, tunaweza kushinda na kuondoka na point 6 na pia ni rahisi kufungwa mechi zote mbili na kuondoka na point 0.

Hapo ndipo ninapoanza kupatwa na wasiwasi, mimi binafsi naamini tutawafunga City na Chelsea,lakini soka ni mchezo wenye matokea matatu, kushinda,kufungwa na kutoa sare, wasiwasi wangu unakuja kutokana na tabia ya mashabiki wa Arsenal kukosa subira.

Yakitokea matokeo hasi nisingependa kuona matusi kuelekea kwa kocha Emery au mchezaji yeyote, ikumbukwe ya kwamba Emery amekakaa na timu kwa miezi isiyozidi miwili, itachukua muda kwa wachezaji kuuelewa mfumo wake na jinsi anavyotaka wacheze.

Kumbuka ya kwamba Pep Guardiola ilimchukua mwaka msima na paundi milioni 500 kuibadilisha Manchester City na Klop katumia zaidi ya paundi milioni 400 hajachukua hata kombe la mbuzi.Kumbuka Emery katumia paundi milioni 66 tu na ana miezi miwili na timu.

Cha msingi sisi wote kama mashabiki wa Arsenal tunatakiwa tuungane wote, tuisapoti timu yetu bila ya kujali matokeo, vaa jezi yako tembea kifua mbele naamini msimu huu tutafanya vizuri.

Cha msingi tumpe muda Unai Emery ili ajenge timu ambayo itatupatia furaha na makombe. #GoUnaiGO #COYG

Mambo matano niliyoyaona katika mechi za kirafiki

Jumamosi iliyopita Arsenal ilimaliza mechi za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi na michezo mingine baada ya kuifunga timu ya Lazio ya Italia kwa jumla ya magoli 2-0.

Nimebahatika kuiangalia kwa makini michezo yote ambayo ilioneshwa hadharani (kuna habari ya kwamba Arsenal ilicheza michezo miwili kwa siri ambapo mmoja matokeo na picha zilivuja na mwingine mpaka leo sina uhakika na kilichotokea).

Katika michezo hiyo mambo mengi yalitokea, yalifungwa magoli mengi na mazuri na pia timu ilicheza vizuri na pia kuna mabadiliko mengi ambayo niliyaona, hivyo nimeamua kukuletea mambo matano ambayo mimi niliyaona.

Mambo matano niliyoyaona katika mechi za kirafiki

Arsenal ilitumia mifumo minne

Katika michezo hii ya kirafiki Arsenal ilitumia mifumo minne ambayo ni 4-3-3, 4-2-3-1,4-4-2 na 5-3-2.

Hili ni jambo jema sana kwani timu kuwa na mifumo tofauti linawafanya wapinzani kushindwa kutabiri mfumo gani timu itatumia na pia jambo jingine lililonivutia ni kuweza kuitumia mifumo mingi ndani ya mechi moja kulingana na timu pinzani na pia matokeo ya muda huo.

Mfano mzuri ulikuwa ni mchezo dhidi ya Atletico Madrid ambapo timu ilianza na mfumo wa 4-2-3-1, kipindi cha pili ikacheza 5-3-2 na dakika za mwisho za mchezo ikacheza 4-3-3.

Kutokana na Unai alivyokuwa anapanga vikosi vyake naamini mifumo ambayo timu itatumia msimu ujao ni 4-2-3-1 kama tukiwa na mpira, mabeki wannne na viungo wawili ambao wanaweza kuwa Xhaka na Torreira huku Ramsey au Özil mmoja akicheza nyuma ya mashambuliaji wa kati.

Na kama tukiwa hatuna mpira tutakuwa tukichez mfumo wa 4-4-2, mshambuliaji na kiungo mshambuliaji wakisaidia kukaba kuanzia mbele,hii itasaidia Arsenal kukaba haraka na kufanya mashambulizi mengi ya kustukiza.

Pia sidhani kama tutaona Auba na Laca wakianza kama washambuliaji wa kati, naamini mmoja atakuwa akianza kama mshambuliaji na mwingine kama winga au mmoja akianza mwingine anasubiri benchi.

Safu kali ya ushambuliaji

Arsenal ilifanikiwa kufunga katika kila mchezo iliocheza katika michezo ya kujipima nguvu, hii ni dalili njema kwani wachezaji walionekana kucheza kwa hali ya juu.

Unne mtakatifu wa Özil,Mkhitaryan,Auba na Laca ulionekana ukishirikiana vizuri ambapo walikuwa wakifunga na kuasist bila matatizo, kwangu mimi tatizo ni moja tu, ni vigumu kuwaanzisha wote wanne kwa wakati mmoja ingawa kwenye mechi dhidi ya Lazio kuna wakati kupindi cha pili wote wanne walikuwa uwanjani na wote tuliona kilichotokea.

Safu ya Ulinzi bado inahitaji maboresho

Moja ya sababu kubwa ya Arsenal kufanya vibaya ni kukatika kwa safu yake ya ulinzi hali iliyopelekea timu kufungwa magoli mepesi sana, wengi tulitegemea ya kwamba kusajiliwa kwa Sokratis kungeondoa tatizo hilo,na hadi mchezo wa mwisho wa kirafiki tatizo hilo lilikuwa bado lipo.

Mimi ninachoamini ni kwamba Mustafi, Chambers na Sokratis wote wana uwezo mzuri tu, ila tatizo ni kwamba hawajazoea kucheza upande wa kushoto wa beki ya kati, hivyo wanamuacha beki wa kushoto bila msaada na kusababisha mashambulizi mengi kupitia upande huo.

Holding ana uwezo wa kucheza upande wa kushoto ila sidhani kama amekomaa kiasi cha kucheza kila mchezo,Mavro bado hajazoea soka la kiingeleza na Koscienly ni majeruhi hadi mwaka mpya.

Hapa Unai anaweza kufanya mambo matatu, moja kumchezesha mmoja kati ya Sokratis na Mustafi nafasi hiyo na kuomba wasifanye makosa,mbili kumchezesha Rob Holding na kutegemea makosa kutoka kwa mchezaji kijana au kuingia sokoni na kuleta beki wa kati mwenye uwezo wa kucheza upande wa kushoto(LCB).

Timu ina makipa wazuri

Arsenal ilimsajili Bernd Leno ili kuongeza nguvu katika upande wa makipa na katika mechi hizi za kirafiki naweza kusema ya kwamba nimeridhika na makipa wote watatu.

Petr Cech ndiye kipa aliyepata mikiki mikiki mingi kwenye hizi mechi,aliokoa penati katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid (kwenye penati tano tano) na pia aliokoa penati ya Morata katika mchezo dhidi ya Chelsea kabla ya kuokoa tena katika penati tano tano kwenye mchezo huo, nilimuona Cech aliyebadilika, akiwapanga mabeki na pia anaonekana ya kwamba mwili umejengeka zaidi kutokana na mazoezi kwangu mimi ndiye aliyekuwa kipa bora wa Arsenal katika michezo hii ya kirafiki.

Bernd Leno pia alicheza vizuri ingawa yeye hakupata nafasi ya kuokoa michomo mingi kama Cech, lakini alinifurahisha sana linapokuja suala la kutawanya mipira na pia kucheza mpira kwa miguu, hiki ni kitu muhimu sana kama Arsenal itacheza counter attack. Kwani uwezo wake wa kujua ampe mpira mchezaji gani hata kabla hajadaka ni siraha kubwa ambayo itaifanya Arsenal iwakute wabeki wengi hawajajiandaa, mfano mzuri ulikuwa ni goli la Özil dhidi ya PSG kaliangalie vizuri utaona ninachokuambia.

Martinez na yeye alicheza vizuri hakufanya makosa yeyote ila kwa sasa nadhani atakuwa kipa wa tatu ama atatolewa kwa mkopo Cech na Leno ni bora kuliko yeye.

Kwangu mimi ningependa Leno awe kipa wa kwanza na Cech msaidizi.

Mattéo Guendouzi

Kwangu mimi Mattéo Guendouzi ndiye aliyekuwa mchezaji bora katika mechi za kirafiki, uwezo wake wa kupiga pasi kwa utulivu wa hali ya juu, kupokonya mipira bila kufanya madhambi na kuanzisha mashambulizi ni vitu ambavyo ni vigumu kuviona kutoka kwa mtoto wa miaka 19.

Kwa dau la paundi milioni 7 tu naamini hapa Arsenal walilamba dume, najua ilikuwa ni michezo ya kirafiki na ningependa kumuona atacheza vipi kwenye mechi zenye ushindani mkubwa, na sintoshangaa kama ataanza jumapili ijayo dhidi ya Manchester City.

Pia madogo Smith Rowe na Reiss Nelson walinivutia sana.

Hayo ndiyo mambo matano niliyoyaona  katika mechi za kirafiki. Je wewe uliyeagalia mechi za kirafiki, ni mambo gani uliyoyaona yaliyokuvutia na ambayo hukuyapenda , tupia maoni yako hapa chini.

Wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia

Wakati kombe la dunia likiendelea nchini Urusi, leo nimeamua kukuletea ninavyoona mimi kuhusu ushiriki wa wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia.

Wachezaji wa Arsenal katika kombe la dunia

Arsenal ina jumla ya wachezaji 9 wanaoziwakilisha nchi zao katika fainali hizi za kombe la dunia na nikiwa mkweli wengi wao hawajafanya vizuri sana.

Kati ya wachezaji hao tisa, watano tu ndio walioanza katika raundi ya kwanza na wanne wameanza katika raundi ya pili.

Mchezaji wa kwanza wa Arsenal kufanya vizuri katika fainali za mwaka huu alikuwa ni Granit Xhaka, baada ya kufunga bonge la goli la kusawazisha wakati Switzerland ilipocheza dhidi ya Serbia.Baadaye Switzerland walishinda mchezo huo kufuatia goli la pili lililofungwa na Xherdan Shaqiri.

Pia katika mchezo huo Xhaka aliingia katika matatizo na fifa wakati akishangilia hilo goli, amepigwa faini ya dola elfu 10 kwa kosa la kuchanganya siasa na soka.

Katika kikosi hicho pia kuna mchezaji mpya wa Arsenal,Lichsteiner ambaye alicheza vizuri katika mechi zote mbili na alinifurahisha sana katika mechi ya kwanza kwani aliweza kumzuia kwa ufanisi mkubwa mchezaji kutoka Brazil,Neymar.

David Ospina  aliisaidia timu yake ya Colombia kushinda kwa goli 3-0, katika mchezo wa kwanza timu yake ilifungwa huku Ospina akicheza vibaya lakini katika mchezo wa juzi alibadilika baada ya kufanya kazi ya ziada kuzuia ya wachezaji wa Poland.

Pia katika mchezo huo aliumia huku nafasi za kufanya mabadiliko zikiwa zimeisha na bado alifanikiwa kuokoa mpira wa shuti kali uliopingwa na Lewandoski katika dakika za mwisho za mchezo huo.

Mohamed Elneny yeye amecheza michezo yote mitatu akiwa na timu yake ya taifa ya Misri lakini kwa bahati mbaya walifungwa katika michezo yote huku Elneny akishindwa kung’ara.

Nacho Monreal yeye bado hajacheza hata dakika moja moja katika michuano hiyo ya kombe la dunia, hali ambayo pia imemkuta Dany Welbeck ambaye hakugusa mpira wakati Uingeleza wakiifumua Panamá goli 6-1.

Mesut Özil ambaye alianza wakati Ujerumani walipofungwa na Mexico, hakucheza katika mchezo wa pili walipoishinda timu ya Sweden goli 2-1.

Alex Iwobi akiiwakilisha Nigeria aliingia dakika za mwisho wakati tai hao wa kijani walipoifunga timu ya Iceland kwa jumla ya magoli 2-0.Iwobi alianza katika mchezo wa kwanza ambapo walifungwa goli 2-0 dhidi ya Croatia.

Joel Campbell hakucheza wakati timu yake ya taifa ya Costa Rica ilipofungwa katika muda wa nyongeza na Brazil,Joel Campbell aliingia kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa kwanza ambapo hakuna la maana alilolifanya.

Huo ndio mchango wa wachezaji wa Arsenal mpaka sasa katika kombe la dunia, Je kwako wewe ni mchezaji gani wa Arsenal aliyefanya vizuri mpaka sasa? tupia maoni yako hapa chini.