Usajili wa Arsenal dirisha dogo la usajili-Mtazamo wangu

Dirisha dogo la usajili kwa mwaka huu lilifungwa alhamisi iliyopita na ufuatao ni mtazamo wangu kuhusu usajili wa Arsenal katika dirisha hili.

Usajili wa Arsenal dirisha dogo la usajili-Mtazamo wangu

Baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa Alhamisi iliyopita na Arsenal kufanya usajili wa mchezaji mmoja tu baada ya kiungo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi Denis Suarez akijiunga na timu kutoka Barcelona kwa mkopo wenye dhamani ya paundi milioni 2.

Taarifa zilizopo ni kwamba Arsenal wanaweza kumnunua mchezaji huyo moja kwa moja kwa dau la paundi milioni 18 katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Usajili wa Denis Suarez ni moja ya sajili za akili ambazo timu kama Arsenal inatakiwa kuzifanya, kwani mchezaji huyo akichemka watakua wametumia paundi milioni 2 tu na ikitokea afanya vizuri watampata kwa paundi milioni 20 tu, katika soko la sasa la wachezaji huwezi ukapata mchezaji wa bei poa zaidi ya hapo.

Suarez, mwenye umri wa miaka 25 ni mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi mbali mbali uwanjani, ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na amekuwa akifanya vizuri kila alipopewa nafasi, ingawa hakupata nafasi kubwa katika timu ya Barcelona.

Kuna baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanaouponda usajili huo na kudai ya kwamba Arsenal ina wachezaji wengi kwenye nafasi yake na mimi nina neno moja kwao, si kweli. soma sababu hapa chini.

Unai Emery anapenda kubadili mifumo kutokana na mchezo unavyoenda na mara nyingi amelazimika kubadilisha wachezaji wakati wa mapumziko, hii ni kutokana na wachezaji wengi kukosa uwezo wa kucheza nafasi nyingi kwa ufanisi ule ule, kwa mfano kiwango cha Ôzil akicheza kama winga ni tofauti kabisa na kiwango cha Ôzil akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Denis Suarez anaweza kucheza nafasi nyingi kwa ufanisi ule ule.

Pia Arsenal hii haina wachezaji wengi wenye uwezo wa kukokota mpira, kwa sasa ndani ya kikosi cha kwanza ni Alexi Iwobi tu anayeweza kuifanya hiyo kazi, hivyo ujio wa Denis Suarez mwenye uwezo wa kufanya hivyo utabadilisha jinsi Arsenal wanavyofanya mashambulizi.

Hii ndiyo sababu pamoja na Arsenal kuwa na matatizo katika nafasi nyingine lakini walikuwa sokoni kutafuta winga mwingine kama Yannick Carrasco na Ivan Perišić.

Katika dirisha hili la usajili tulishuhudia Arsenal ikijaribu kwa hali na mali kutafuta winga baada ya kuwapo na taarifa za kutaka kuwasajili Ivan Perišić na Yannick Carrasco, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na Arsenal kukosa pesa na hivyo kushindwa kufikia makubariano na timu zilizokuwa zinawamiliki wachezaji hao.

Kama kuna nafasi ambayo mashabiki wengi wa Arsenal walikuwa wanategemea kuona usajili mpya ilikuwa ni nafasi ya beki wa kati. Kuumia kwa Rob Holding, Sokratis na Koscienly kuliifanya timu kuwa katika hali ngumu, kuongeza mchezaji mpya hata kwa mkopo katika nafasi hiyo kulionekana kama jambo la busara, lakini kulikuwa na sababu ya msingi kwa nini Arsenal hawakufanya hivyo.

Katika mahojiano na waadhishi wa habari, kocha mkuu wa Arsenal Unai Emery alisema ya kwamba Arsenal ina mabeki wengi ndani ya kikosi hicho, alisema ya kwamba majeraha ya wachezaji wengi yalikuwa ni ya muda mfupi, na kama wangesajili mchezaji mpya na wale wa zamani kupona kila mchezaji angetaka kucheza na hali hiyo ingeleta matatizo mbeleni, ukiisoma hiyo kauli kwa makini utagundua ya kwamba kuna ukweli ndani yake.

Arsenal ina mabeki wa kati sita wenye mikataba mpaka mwaka 2020 au zaidi ya hapo ( hapa tunamhesabia na Calum Chambers ambaye ametolewa kwa mkopo). Hii namba ni kubwa kuliko timu zote 6 kubwa za ligi kuu ya Uingeleza.

Kusajili mchezaji mpya katika kipindi hiki ilikuwa ni vigumu kwa sababu kubwa mbili, moja mshahara na ada ya uhamisho na pia mchezaji mpya angetaka ahakikishiwe nafasi ya kucheza, hivyo walijaribu kutafuta mchezaji ambaye angeweza kuja kwa mkopo hadi mwisho wa msimu na walikosa.

Pamoja na hayo Arsenal watategemea kupona haraka kwa Sokratis na Koscienly kutoka kwenye majeraha ya muda mfupi na kuomba ya kwamba wawe fiti katika mechi zote zilizobakia za msimu huu.Mustafi yupo fiti na Konstantinos Mavropanos ameshapona na yupo tayari kuanza kucheza.

Arsenal hawajatumia pesa nyingi katika  dirisha hili la usajili lakini tukiwa wakweli hakuna timu kubwa iliyotumia pesa( ukiondoa Chelsea ambao nao walimsajili Gonzalo Higuain kwa mkopo).

Usajili wa Denis Unaleta maana ukichukulia na ukweli wa kwamba anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani na pia ana uwezo wa kucheza katika mifumo tofauti ambayo Unai Emery anatumia.

Cha msingi ni Arsenal kuhakikisha inamaliza ndani ya timu nne bora na kupata nafasi ya kushiriki katika ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao, na nina imani kubwa tutaona usajili wa maana hasa kwenye nafasi ya ulinzi katika dirisha lijalo la usajili wakati Arsenal itakapopata pesa.

 

Speak Your Mind

*