Usajili Wenye utata wa Cedric Soares

Usajili Wenye utata wa Cedric Soares

Katika dirisha dogo la usajili Arsenal ilisajili mabeki wawili, Pablo Mari na Usajili Cedric Soares, wote wawili bado hawajacheza mchezo wowote wakiwa na jezi za Arsenal.

Aliongea na waandishi wa vyombo vya habari kabla ya mchezo wa kesho dhidi ya Newcastle United, kocha mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta alisema ya kwamba anategemea ya kwamba Mari atacheza alhamisi dhidi ya Olimpiacos na alipoulizwa kuhusu Soares hakukua na jibu la moja kwa moja na ingawa aliweka wazi ya kwamba mchezaji huyo bado hajaanza mazoezi na wachezaji wenzie.

Hapo ndipo unapokuja wasiwasi wangu, kama wiki mbili baada ya kusajiliwa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi na mpaka leo bado hajaanza mazoezi na haijulikani ataanza lini mazoezi hayo.

Kama Arsenal walijua ya kwamba mchezaji huyo alikuwa na majeraha ya muda mrefu kwa nini walimsajili?

Kwa kawaida mchezaji akitoka kwenye majeraha ya muda mrefu atahitahi wiki tatu au nne kuwa fiti, ukichukulia ya kwamba ni mchezaji mpya na bado hajazoeana na wenzake hadi awe tayari kucheza zinaweza kupita wiki 6.

Hali inayofanya kama ataanza mazoezi wiki ijayo tunaweza kuanza kumuaona ndani ya uzi wa Arsenal mwezi wa nne, na ligi inaisha mwezi wa tano na hivyo kukosa sehemu kubwa ya michezo muhimu.

Najua anaweza akapona na akawa msaada mkubwa kwa timu lakini kwa sasa hali inaonekana tofauti na huu unaweza ukawa usajili mbaya kwa Arsenal.

Usajili huu umenikumbusha usajili wa kiungo kutoka Swenden, Kim Kallstrom ambaye alisajiliwa ili kukabiliana na tatizo la majeruhi na alipofanya vipimo na kugundulika ya kwamba alikuwa majeruhi, Arsene Wenger aliamua kumsajili hivyo hivyo na matokeo yake alicheza dakika 135 tu katika mashindano yote.

Lengo kubwa la kufanya mabadiliko ya kimuuondo na uongozi ndani ya Arsenal ilikuwa ni kuepusha sajili kama hizi na kama bado timu inaendelea kufanya makosa yale yale inakuwa ni vigumu mmno kusonga mbele.

Inawezekana Cedric Soares akapona na kuwa sehemu kubwa ya ushindi ya Arsenal na kuisaidia timu kubeba kombe au kucheza katika ligi ya mabingwa Ulaya, lakini hadi hapo itakapodhibitika vinginevyo huu unabakia kuwa ni usajili wenye utata na ikitokea akashindwa kutoka mchango kwenye timu kuna watu watatakiwa wajibu maswali kadhaa.

Tupia Maoni Yako Hapo Chini