Wachezaji vijana wa Arsenal na nafasi yao katika msimu ujao

Wakati Arsenal ikiendelea kujiandaa na msimu mpya wa ligi, kuna baadhi ya wachezaji vijana ambao wameonesha matumaini makubwa ya kwamba wanaweza kuwa kwenye mipango ya kocha Unai Emery katika ligi kuu na michezo mingine,leo nakuletea wachezaji  vijana wa Arsenal na nafasi zao katika timu.

Konstantinos Mavropanos

Beki huyu mwenye umri wa miaka 20 alisajiliwa mwezi wa kwanza mwaka huu, mipango ilikuwa ni kumpeleka kwa mkopo, lakini alifanikiwa kumvutia Wenger katika mazoezi na kumfanya abadili mawazo na kumbakisha kikosini.

Tayari ameshaichezea Arsenal katika michezo mitatu ya ligi kuu ya Uingeleza,Alicheza vizuri tulipofungwa na Manchester United,pia alicheza vizuri tulipowafunga Burnley goli 5-0 na alipewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Leicester.

Ni kijana mwenye nguvu na kipaji cha hali ya juu,ila sidhani kama yupo tayari kucheza katika kikosi cha kwanza,Kama Koscienly atapona mapema na ukichukulia ujio wa Sokratis,Uwepo wa Chambers na Mustafi anaweza kuwa chaguo la tano ama la sita (akishindana na Rob Holding).

Sinoni akipata nafasi katika kikosi cha kwanza ila naamini ataacheza sana kwenye Europa league na mmoja wapo kati ya Mustafi au Holding.

Na kama Koscienly atapona kabla ya kuanza mwaka mpya mmoja wapo kati yake na Holding ataenda kwa mkopo katika dirisha la usajili la mwezi wa kwanza.

Reiss Nelson

Na yeye ni kama  Mavropano, mashabiki wa Arsenal walikuwa na matumaini makubwa na nafikiri hajacheza kwa kiwango kikubwa kama mashabiki wengi wa Arsenal walivyotegemea.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 anauwezo wa kucheza kama winga na kama kiungo mshambuliaji wa kati, nafasi ya kiungo mshambuliaji hawezi kuipata kwani pale kuna Mesut Özil, Aaron Ramsey na Mkhitaryan.

Nafasi ya winga mpaka sasa haieleweki nani atacheza, Kuna Iwobi,Mkhitaryan,Welbeck  na Lucas Perez,nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza ni finyu.

Kama Mavropanos, nategemea atapata nafasi ya kucheza katika hatua ya makundi ya kombe la Europa League na kama atafanya vizuri kuliko Iwobi na Welbeck anaweza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Iwapo atashindwa kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Europa League anaweza akatolewa kwa mkopo kwenda kwenye timu ya daraja la kwanza mwezi wa kwanza mwakani.

Jeff Reine-Adelaide

Jeff alianza vizuri kuichezea Arsenal, lakini majeraha ya mara kwa mara yamemfanya ashindwe kuonesha kiwango chake, pamoja na kuwa na umri mkubwa kumzidi Nelson (Jeff ana miaka 20), kwa sasa Nelson ni bora kuliko Jeff, labda afanye vizuri sana kwenye mechi za kirafiki, sioni nafasi ya Jeff kwenye kikosi cha sasa.

Eddie Nketiah

Mchezaji huyo alijipatia umaarufu mkubwa mwaka jana baada ya kufunga magoli mawili yaliyoisaidia Arsenal kushinda dhidi ya Norwich.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga kwa sasa ni mshambuliaji wa nne katika timu ya Arsenal, akiwa nyuma ya Auba,Lacazzete na Danny Welbeck.

Welbeck anaingia katika mwaka wake wa mwisho, na kuna tetesi za kwamba anatakiwa na Everton,akiondoka Welbeck kuna mambo mawili yanaweza kutokea, moja Arsenal wanaweza kusajili mshambuliaji mwingine au mbili Unai Emery anaweza kubaki na Nketiah kama mshambuliaji wa akiba.

Ainsley Maitland-Niles

Huyu haendi kokote, mwaka jana alicheza michezo 28 na mwaka huu nategemea atacheza idadi kama hiyo ama zaidi, amepewa mkataba mpya na amebadilisha jezi na kupewa namba 15,ni dhahiri ya kwamba yupo kwenye mipango ya mwalimu.

 

Emile Smith Rowe

Akiwa na umri wa miaka 17 Emile Smith Rowe, huu unaweza ukawa ni mwaka ambao dogo huyu akaichezea timu ya wakubwa.

Alikuwa katika kikosi cha Arsenal kilichoifunga Boreham Wood na pia alicheza katika mchezo wa juzi wa kirafiki, na kuna taarifa ya kwamba atakuwemo kwenye kikosi kinachoelekea Singapore kwa ajili ya michezo ya kombe la kimataifa.

Smith Rowe alikuwa katika kikosi cha timu ya vijana wa Arsenal iliyofika fainali ya kombe la FA kwa timu za vijana, ambapo alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri kabisa katika michuano hiyo.

Wachunguzi wa manbo ya soka wanadai ya kwamba mchezaji huyo ni muunganiko wa Mesut Ozil na Alex Oxlade-Chamberlain kutokana na uwezo wake wa kupasua ukuta wa timu pinzani kwa kupiga pasi zenye macho na pia ana uwezo mkubwa wa kukimbia akiwa na mpira.

Sioni nafasi yake kwenye timu, ila naamini ya kwamba mkopo kwenda kwenye timu yenye ushindani hasa katika nusu ya kwanza ya msimu ujao.

Hao ndio wachezaji vijana wa Arsenal ambao wanaweza kufanya vizuri msimu ujao wakiwa na timu ya wakubwa, wengine nawaona wakibaki katika timu ya vijana, ama kutolewa kwa mkopo.

Speak Your Mind

*